Na Mwandishi Wetu
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeandika historia mpya baada ya kuingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya QS World University Rankings (QS WUR) 2027, hatua inayokitambulisha rasmi miongoni mwa vyuo vikuu bora duniani na kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya elimu ya juu, utafiti na ubunifu.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na taasisi ya QS, UDSM imeorodheshwa katika kundi la nafasi 1201–1400 duniani, mafanikio ambayo viongozi wa chuo wanasema ni ushahidi wa ubora unaoendelea kujengwa katika elimu, utafiti na uzalishaji wa maarifa yenye mchango kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 15, 2026 Jijini Dar es salaam kuhusu mafanikio hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Prof. Nelson Boniface, amesema hatua hiyo si mafanikio ya chuo pekee bali ni mafanikio ya Taifa zima, kwani viwango vya kimataifa vya vyuo vikuu vimekuwa kipimo muhimu cha uwezo wa nchi katika kuzalisha wataalamu, kufanya tafiti, kuendeleza ubunifu na kushindana katika uchumi unaotegemea maarifa.
Amesema kuingia kwa UDSM katika mfumo wa QS kunatoa fursa kubwa ya kuongeza ushirikiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji katika elimu na utafiti, pamoja na kuongeza hadhi ya Tanzania mbele ya wanafunzi, watafiti, waajiri, wawekezaji na washirika wa maendeleo duniani.
Prof. Boniface ameeleza kuwa toleo la QS World University Rankings 2027 lilikuwa na ushindani mkubwa ambapo zaidi ya vyuo vikuu 8,800 kutoka mataifa mbalimbali vilifanyiwa tathmini, lakini ni vyuo 1,504 pekee vilivyokidhi vigezo na kuingizwa katika orodha rasmi ya QS.
Mbali na kuingia katika orodha hiyo, UDSM imeonyesha ubora mkubwa katika baadhi ya viashiria muhimu vya kimataifa. Chuo kilipata alama 85.3 katika kipengele cha Employment Outcomes, na kushika nafasi ya 131 duniani, jambo linaloonyesha kuwa wahitimu wake wanakubalika na kuthaminiwa na waajiri katika sekta mbalimbali nchini na kimataifa.
Aidha, chuo kilifanya vizuri katika kipengele cha International Research Network, kinachoonesha nguvu ya ushirikiano wake wa kimataifa katika tafiti na ubunifu.
Kwa mujibu wa Prof. Boniface, mafanikio hayo yanaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema kuorodheshwa kwa UDSM kunachangia utekelezaji wa nguzo za dira hiyo kwa kuongeza ushindani wa Tanzania katika uchumi wa maarifa, kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kimataifa, pamoja na kuimarisha tafiti, mageuzi ya kidijitali na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Prof. Boniface ameongeza kuwa mafanikio hayo pia yanaakisi utekelezaji wa Dira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 2061, inayolenga kukifanya chuo hicho kuwa taasisi inayotambulika duniani kwa ubora katika elimu, utafiti, ubunifu na huduma kwa jamii.
Hata hivyo, amesema tathmini ya QS imebainisha maeneo ambayo chuo kitaendelea kuyaboresha ili kuongeza ushindani wake duniani. Maeneo hayo ni pamoja na kuongeza athari za machapisho ya kisayansi kupitia rejea za tafiti (citations), kuimarisha sifa ya chuo katika jumuiya ya kimataifa ya wasomi, kuongeza idadi ya wanafunzi na wahadhiri wa kimataifa pamoja na kuimarisha shughuli za uendelevu.
Amesema UDSM tayari imeandaa mkakati wa maboresho wa mwaka 2027–2030, utakaolenga kuimarisha ubora wa utafiti, ushirikiano wa kimataifa, ubunifu, matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuboresha viashiria vinavyotumika katika tathmini za QS.



