Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Dkt. Jabiri Bakari imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja kupitia Dawati maalum la Huduma kwa Wateja, likiwa na lengo la kuhakikisha wananchi na wadau wa sekta ya usafiri wa anga wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati.
Akizungumza katika Banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja wa TCAA, Bw. Rashid Mngoya, alisema dawati hilo limeanzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka.
Bw. Mngoya alisema kupitia dawati hilo, wateja na wadau wanaweza kupata ufafanuzi kuhusu huduma za TCAA, kuwasilisha maoni, hoja na changamoto, pamoja na kuelekezwa kuhusu taratibu mbalimbali zinazohusiana na sekta ya usafiri wa anga.
Alieleza kuwa Dawati la Huduma kwa Wateja ni sehemu muhimu ya jitihada za TCAA za kuwa karibu zaidi na wateja wake na kuhakikisha masuala yanayowasilishwa yanapokelewa, kufanyiwa kazi na kupatiwa majibu kwa wakati.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati. Dawati hili linatoa fursa kwa wananchi na wadau kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka na kupata msaada kuhusu huduma wanazozihitaji,” alisema Bw. Mngoya.
Na kuongeza kuwa TCAA imejipanga kuendelea kuisimamia sekta ya usafiri wa anga kwa weledi na ufanisi, huku ikihakikisha viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama, ulinzi na ubora wa huduma vinazingatiwa.
Awali akizungumzia maboresho mengine yanayotekelezwa na Mamlaka, Meneja Uhusiano wa TCAA, Bw. Ally Changiwa, alisema TCAA imeendelea kuboresha mifumo yake ya mawasiliano na utoaji wa taarifa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wadau.
Bw. Changiwa alisema miongoni mwa maboresho hayo ni tovuti ya TCAA, ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ikiwa imeongezewa taarifa nyingi zaidi, hatua inayolenga kuwezesha watumiaji wengi zaidi kupata taarifa kwa urahisi.
Aliongeza kuwa tovuti hiyo pia imeboreshwa kwa kuwekwa sehemu ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara, ambayo inatoa majibu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kusimamiwa na TCAA.
Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, TCAA inaendelea kutoa elimu na ufafanuzi kwa wananchi kuhusu majukumu yake, huduma za kiudhibiti, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege nyuki, pamoja na masuala mengine yanayohusu sekta ya usafiri wa anga.
Ushiriki huo unaakisi dhamira ya TCAA ya kuimarisha mawasiliano na wadau, kuongeza uelewa wa umma na kuendelea kutoa huduma zinazochangia usalama, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga nchini.








