Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa mkoa wa Tanga umekaa kimkakati katika kukuza na kuchangia katika pato la Taifa kutokana na kuwa na fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo Bandari ya Tanga, viwanda na sekta ya utalii.

Mhe. Balozi Omar alisema hayo leo tarehe 13 Julai, 2026, alipokutana kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Balozi Omar alisema Mkoa wa Tanga una nafasi muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa kutokana na kuwa lango muhimu la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na mchango wake mkubwa katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, kwa kuwa ina fursa zote za kiuwezeshaji ikiwemo Bandari.

Alisisitiza umuhimu wa wananchi kuchangamkia fursa hizo zikiwemo zile zinazotokana na utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali zinazohusu kuwawezesha kiuchumi vijana, wanawake na makundi maalumu kupitia mikopo ya Halmashauri, uanzishwaji wa biashara baada ya Serikali kuondoa sharti la kulipa kodi kwa biashara mpya zinazofunguliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, pamoja na kunufaika na sekta ya ununuzi wa umma.

“Katika Sekta ya ununuzi wa umma tumeweka masharti kwa biashara au kandarasi zote zinazo anzia shilingi bilioni 50 kushuka chini zitawahusu wazawa pekee, hivyo watanzania wachangamkie fursa hizo” alisisitiza Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wake, Dkt. Batilda Buriani alisema kuwa Mkoa wa Tanga ni mkoa wa kimkakati kwa kuwa una miundombinu muhimu ikiwemo bandari, reli, barabara na nishati ambayo itasaidia Tanzania kufikia azma ya kuwa na uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.

Aliishukuru Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuupatia mkoa wa Tanga kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kuboresha miundombinu ya uwekezaji na huduma za wananchi ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Tanga, Bandari ya Tanga, barabara, vituo vya afya na elimu na kwamba hatua hiyo imeufungua kiuchumi mkoa huo.

Aidha, Dkt. Batilda alimshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea mkoa huo na kumkaribisha rasmi katika ziara yake, ambayo itahusisha kutembelea shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na miradi inayotekelezwa na Serikali kwa ajili ya wananchi mkoani humo.