Mnamo Juni 29, 2026 TAKUKURU Wilaya ya Siha imefungua shauri la uhujumu uchumi namba 14596/2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Siha ikiwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Dkt. Donatus Boniphace Tsete.

Dkt. Tsete anashtakiwa kwa makosa ya kughushi, kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo, ufujaji na ubadhirifu na kuisababishia Hospitali ya Kibong’oto hasara ya fedha Tsh. 5,550,000/=.

Mshtakiwa anadaiwa kufanya makosa hayo akiwa daktari wa binadamu katika Hospitali ya Kibong’oto iliyopo wilayani Siha.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali anayeiwakilisha Jamhuri Bw. Bernard Ndamallya ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Elibahati Petro kuwa mshtakiwa alilipwa fedha hizo kwa njia ya masurufu kwa ajili ya kulipa wadau wa programu ya DR TB Mentorship katika Wilaya ya Iringa, Mkoa wa Iringa mwaka 2021 badala yake hakuwalipa wadau wa programu hiyo ila alighushi saini zao kuonesha wamelipwa kiasi hicho cha fedha kwa tarehe mbalimbali za mwezi Julai 2021.

Baaada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikana mashtaka yote na Mahakama ilimpa masharti ya dhamana ambayo aliyatimiza na yupo nje kwa dhamana.