Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbarali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amekabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 349 kwa kikundi cha vijana cha Ukwavila kinachojishughulisha na shughuli za kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya leo Julai 12, 2026.
Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya uwezeshaji kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 200 iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuongeza fursa za ajira, kuimarisha ujasiriamali na kuinua uchumi wa vijana nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Nanauka amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata mitaji itakayowawezesha kuanzisha na kukuza miradi mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda vidogo na biashara, ili kuongeza ajira na kipato kwa vijana.
Mhe.Nanauka ameongeza kuwa mkopo huo kwa kikundi cha Ukwavila utasaidia kuongeza uwezo wa vijana hao katika uzalishaji wa kilimo kwa kutumia mbinu za kisasa, kuongeza thamani ya mazao na kupanua masoko ya bidhaa zao, hatua itakayochangia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, kusimamia miradi yao kwa uwajibikaji na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kuwafikia makundi mengine ya vijana wenye uhitaji.
Programu ya Taifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ya Shilingi Bilioni 200 inaendelea kutekelezwa na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuwawezesha vijana kote Nchini wenye miradi yenye tija kupata mitaji nafuu, kuongeza uzalishaji, kuibua ajira mpya na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.




