Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Zanzibar

Naandika makala hii muda mfupi baada ya kutoka kwenye viwanja vya Ikulu, Zanzibar, ambako yamefanyika maridhiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo. Maridhiano haya yamefungua ukurasa mpya kiasi kwamba Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, hadharani mbele ya kadamnasi akamtambua Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Sitanii, huu umekuwa mkutano wa wazi wa kwanza kwa Othman Masoud na Dk. Mwinyi kukutana katika jukwaa moja tangu uchaguzi ulipomalizika Oktoba 29 mwaka jana. Najua tangu wiki iliyopita msomaji umeshasikia mengi yaliyojiri kutokana na mkutano huu. Yapo machache ninayoamini hujayasikia, ndiyo maana nataka kukufikirisha juu ya yaliyojiri Zanzibar.

Vyama hivi viwili vilikuwa na uhasama mkubwa kiasi kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman, alikataa kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baadhi ya nafasi katika Baraza la Mawaziri la Dk. Hussein Mwinyi ziko wazi hadi leo kwa sababu ACT-Wazalendo waligoma kuingia serikalini. Lakini wakati hayo yote yakitokea, hatukusikia kelele nyingi. Naam, kuna watu walidhani Zanzibar mambo yako shwari.

Sitanii, ndiyo maana wakati wa vurugu za Oktoba 29 mwaka jana, pamoja na hali ya kutokubaliana kati ya ACT na CCM, baadhi ya watu walitoka Bara na kukimbilia Zanzibar. Zanzibar imeonekana kuwa shwari muda wote baada ya uchaguzi, kumbe kuna wazee walikuwa wanatimiza maandiko matakatifu kwamba “uzee ni dawa.”

Othman ameuambia umma uliokuwapo kuwa vyama vya siasa vinaweza kutokubaliana, lakini njia pekee ya kumaliza sintofahamu zao ni mazungumzo. Amesema unaweza kulalamikia uwepo wa giza, lakini suluhisho ni kuwasha taa kuliondoa giza, na taa yenyewe ni mazungumzo.

Kupitia makala zangu nyingi nimekuwa nikisema hata kama tutapigana vita, tukiuana au kutendeana vyovyote iwavyo, njia pekee itakayotutoa katika mkwamo huu ni mazungumzo.

Rais Samia Suluhu Hassan amepigilia msumari wa mwisho katika hoja hii kwa kusema, “Maridhiano si udhaifu.” Huu ni mwendelezo wa kauli zake ambapo siku za nyuma amepata kutwambia yeye kama Mama ataendelea kunyoosha mkono wa maridhiano. Kumbe ni katika hili nasema kilichoanzia Zanzibar kinapaswa kuendelezwa hata Bara.

Ni siri iliyo wazi kuwa CCM na CHADEMA kwa sasa hawapikiki chungu kimoja. Mwenyekiti wa CHADEMA yuko ndani anakabiliwa na kesi ya uhaini ambayo, akitiwa hatiani, adhabu yake ni kifo. Ni wazi wafuasi wa CHADEMA hawawezi kufurahi hata chembe kuona mwenyekiti wao anakabiliwa na hatari hiyo ikiwa atashindwa kesi ambayo wengi wanaamini anaweza kuishinda.

Jingine ambalo nikushirikishe, msomaji, ni kwamba Zanzibar kuna wazee kama ilivyo Tanzania Bara. Mzee Amani Abeid Karume na Mzee Ali Mohamed Shein walipoona mambo yanaharibika waliingilia kati. Waliamua kukutana na pande mbili na kuzieleza faida na hasara za vurugu za kisiasa. Kumbe tangu Novemba mwaka jana walikuwa wakishauriana na pande zote mbili, jambo lililosaidia kutuliza joto lililokuwa linafukuta.

Hawakuwa peke yao. Wapo akina Mzee Juma Duni Haji (Babu Duni) ambao nao walishiriki kutafuta mwafaka. Tumesikia itaundwa Tume ya Kisheria kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa. Tume hii italenga kuondoa sintofahamu za mara kwa mara zinazotokea wakati wa uchaguzi. Dk. Karume na Dk. Shein wamefanya kazi kubwa mno. Wawili hawa wamechangia kuhakikisha amani inaimarika Zanzibar na sasa matunda ya juhudi hizo yanaonekana wazi.

Sitanii, katika historia ya mataifa mengi duniani, migogoro ya kisiasa haijawahi kumalizwa kwa nguvu bali kwa mazungumzo. Zanzibar nayo imepitia vipindi vya misuguano ya kisiasa iliyosababisha taharuki, mgawanyiko wa kijamii na kudhoofisha shughuli za maendeleo. Hivyo, kila fursa ya kujenga maridhiano kati ya CCM na ACT-Wazalendo inapaswa kuungwa mkono kwa sababu manufaa yake yanakwenda mbali zaidi ya maslahi ya vyama vya siasa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa maridhiano si dalili ya udhaifu bali ni ishara ya uongozi wenye busara unaoweka mbele maslahi ya taifa. Kauli hiyo ina uzito mkubwa kwa sababu viongozi wenye maono hutambua kuwa ushindi mkubwa si kumshinda mpinzani, bali ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani, utulivu na matumaini.

Mtazamo huo unakamilishwa na kauli ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, aliyesisitiza kuwa katika mgogoro wowote suluhisho ni mazungumzo na si kupigana. Hii ni falsafa inayotambulika duniani kote. Mazungumzo hufungua milango ya kuelewana, hujenga kuaminiana na kutoa nafasi kwa kila upande kusikilizwa. Badala ya kuongeza majeraha ya kisiasa, mazungumzo hujenga mazingira ya uponyaji na ushirikiano.

Zanzibar imejifunza kupitia historia yake kuwa kila uchaguzi unapomalizika wananchi hubaki kuwa ndugu, majirani na washirika wa maendeleo hata kama hawakubaliani kisiasa. Hakuna chama kinachoweza kuijenga Zanzibar peke yake. Serikali inaweza kuwepo, lakini maendeleo ya kweli yanahitaji ushiriki wa wananchi wote bila kujali tofauti zao za kisiasa. Ndiyo maana maridhiano yanapaswa kuonekana kama msingi wa maendeleo ya muda mrefu.

Mazingira ya kisiasa yenye utulivu huongeza imani ya wawekezaji, huimarisha sekta ya utalii na kuvutia biashara mpya. Zanzibar inapokuwa na amani, uchumi hukua kwa kasi zaidi na vijana hupata fursa nyingi za ajira. Badala ya kutumia nguvu na rasilimali kushughulikia migogoro ya kisiasa, taifa linaelekeza nguvu zake katika kuboresha elimu, afya, miundombinu na huduma nyingine za kijamii.

Viongozi wa CCM na ACT-Wazalendo wana nafasi ya kuandika ukurasa mpya wa historia ya Zanzibar kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi kuliko tofauti za kisiasa. Walifanya hivyo wakati wa CUF chini ya Maalim Seif Sharif Hamad. Ushindani wa kisiasa ni sehemu ya demokrasia, lakini ushindani huo haupaswi kuwa sababu ya kuvunja mshikamano wa wananchi. Vyama vinaweza kutofautiana katika sera, lakini vinapaswa kukubaliana kwamba amani ni msingi wa maendeleo.

Ni muhimu pia wananchi waunge mkono juhudi zozote za mazungumzo na kujiepusha na lugha za chuki zinazoweza kurudisha nyuma hatua zilizopatikana. Maridhiano hayaondoi ushindani wa kisiasa, bali yanaweka utaratibu wa kushindana kwa hoja, kuheshimiana na kukubali kuwa maslahi ya Zanzibar yako juu ya maslahi ya chama chochote. Maridhiano si kibali cha kuiba kura au kutangaza aliyeshindwa kuwa mshindi. Yanalenga kuweka uwanja sawa wa kisiasa.

Sitanii, kauli ya Rais Samia kwamba maridhiano si udhaifu, pamoja na msimamo wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, kwamba suluhisho la migogoro ni mazungumzo na si kupigana, zinapaswa kuwa dira kwa viongozi na wananchi wote. Zanzibar yenye maridhiano ni Zanzibar yenye umoja, utulivu na maendeleo endelevu. Huo ndiyo urithi bora ambao kizazi cha sasa kinaweza kuuacha kwa vizazi vijavyo.

Nafahamu maumivu waliyopitia CHADEMA na nafahamu hasira walizonazo wana-CCM kwa kuona CHADEMA kinatishia uwepo wao madarakani. Naamini Tanzania Bara tunao wazee akina Jakaya Kikwete, Pius Msekwa, Jaji Joseph Warioba, Abdulrahman Kinana na wengine ambao wakiamua kuzungumza na pande mbili zinazosisigana, kama walivyofanya Dk. Karume na Dk. Shein, Tanzania bila uhasama inawezekana.

Binafsi naona kilichoanzia Zanzibar, CCM na CHADEMA kinawahusu. Mazungumzo kati ya CCM na CHADEMA yaanze haraka. Tunahitaji Tanzania isiyokuwa na matishio ya maandamano. Tanzania isiyosemwa vibaya na wabia wetu wa maendeleo na nchi wahisani. Tunayo nafasi ya kuzuia uhasama bila kusubiri mashinikizo yatakayoweza kuishia katika umwagaji damu.

Tuzungumze. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827