Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Nafahamu kwa sasa nchi yetu ina joto la kisiasa. Joto linapanda kutoka kila kona. Linapanda kutoka vyama vya upinzani, linapanda kutoka ndani ya chama tawala kuelekea mwaka 2030, maana huo ndio ukweli, na yatupasa kuwa wakweli. Linapanda kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kuwa ndani na Marekani na washirika wake kutupelekea moto. Mambo ni mengi.
Sitanii, katika yote hayo, naomba msomaji uniazime sikio lako. Naomba tuzungumze kwa utuo na tukubaliane kukubaliana au kutokubaliana, lakini angalau tuwe na taarifa zinazofanana. Kwa vyovyote itakavyokuwa, nieleze ombi langu kuu mwanzo kabisa.
Nathamini maisha ya binadamu. Sitamani kilichotokea Oktoba 29, 2025 kitokee tena Julai 7, 2026. Tunakumbuka tulipoteza maisha ya Watanzania wenzetu 518 kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Jaji Chande.
Hiki si kitu chema. Najua ipo siku sote kwa nyakati tofauti tutarejea kwa Muumba wetu. Huu ni wajibu tusioweza kuukiuka siku tukiitwa na Mungu.
Nisichotamani, ni sisi kwenda kabla ya kuitwa, kwa maana wakati usio mwafaka. Kijana anayefariki dunia katika maandamano, vurugu au vyovyote utakavyo kuyaita, angeweza kuwa kiongozi mkubwa kwa taifa hili siku za usoni, ila kubwa zaidi ni tegemeo la familia yake. Inauma sana.
Sitanii, katika kutathmini uongozi wa taifa, ni muhimu kutenganisha matatizo ya kihistoria na juhudi za viongozi waliopo madarakani. Naomba niseme bayana na kwa uwazi bila kuuma maneno kuwa si haki kumhukumu Rais Samia Suluhu Hassan kwa sera, uamuzi na changamoto zilizojengwa kwa miongo mingi kabla ya yeye kuingia madarakani.
Baada ya Azimio la Arusha, Tanzania ilijenga zaidi ya mashirika ya umma 500 pamoja na viwanda mbalimbali vya kimkakati vilivyokuwa uti wa mgongo wa uchumi. Viwanda vya nguo kama Mwatex, Kilitex, Sunguratex na vingine, vilitoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi.
Hata hivyo, katika mchakato wa ubinafsishaji, baadhi ya wazawa waliokabidhiwa mali hizo walishindwa kuzisimamia na kuziendeleza. Wengine walitafuna rasilimali hizo wakidhani wanaiibia serikali, bila kutambua kuwa walikuwa wanaharibu fursa za wananchi wenzao.
Kama viwanda na mashirika hayo yangeendelezwa kwa maono ya Mwalimu Julius Nyerere, leo Tanzania ingeweza kuwa na ajira nyingi zaidi na changamoto ya ukosefu wa kazi kwa vijana isingekuwa kubwa kama ilivyo sasa.
Mzigo wa makosa hayo ya kihistoria unamwangukia Rais Samia, ambaye anapaswa kukabiliana na athari zake katika mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia na matarajio makubwa ya wananchi.
Nyerere aliona mbali. Alijua kuwa idadi ya vijana inaongezeka mwaka hadi mwaka. Akaanzisha mashirika ya umma. Akaanzisha viwanda. Wakubwa waliokabidhiwa wakavitafuna!
Sitanii, kwa kipindi kirefu kuanzia mwaka 2014, ajira mpya serikalini zilisitishwa, huku kupandisha watumishi vyeo na mishahara kukisimama kwa muda. Hali hiyo ilisababisha wahitimu wengi wa vyuo vikuu na kada nyingine kumaliza masomo yao bila kupata ajira, jambo lililoongeza mbinyo wa vijana wanaotafuta kazi nchini.
Rais Samia alipoingia madarakani, alifungua ukurasa mpya kwa kurejesha ajira serikalini, kupandisha watumishi vyeo, kuongeza mishahara na kuajiri vijana zaidi ya 70,000 ndani ya miaka minne iliyopita katika sekta mbalimbali za umma. Hatua hizo zimeanza kupunguza shinikizo lililokuwa limejijenga kwa miaka mingi.
Mbali na hilo, serikali yake imewekeza kwa kiwango kikubwa katika ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, hospitali na miundombinu mingine ya kijamii. Katika sekta ya miundombinu, ujenzi wa madaraja ya Msimbazi/Kigogo, Jangwani na Mkwajuni ni sehemu ya suluhisho la kisayansi la kukabiliana na mafuriko ya mara kwa mara jijini Dar es Salaam yaliyokuwa yakisababisha kufungwa kwa barabara na hasara kubwa kwa wananchi.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna mambo ambayo wananchi wanatarajia kuona yakikamilishwa. Taifa linahitaji maridhiano ya kisiasa ya kudumu, kumalizika kwa kesi zinazotafsiriwa kuwa za kisiasa, kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba mpya, na kuhakikisha vyama vya siasa vinafanya shughuli zake kwa uhuru ndani ya sheria.
Aidha, ni muhimu kuhakikisha hakuna mwananchi anayepotea katika mazingira yasiyoeleweka na kwamba haki za mpigakura na mpigiwa kura zinalindwa ipasavyo. Amani na mshikamano wa taifa ni mtaji mkubwa wa maendeleo na vinapaswa kupewa kipaumbele cha juu.
Sitanii, kama ambavyo serikali yake ilivyofanikiwa kudhibiti changamoto ya makundi ya kihalifu ya ‘Panya Road’ jijini Dar es Salaam, wananchi wengi wanaamini kuwa kwa utashi wa kisiasa na ushirikiano wa wadau wote, changamoto nyingine za kijamii na kisiasa zinaweza kutatuliwa.
Ni vema kumpa Rais Samia nafasi ya kuendelea kushughulikia kero zilizopo kwa kutumia mbinu za kisasa na suluhisho za kisayansi, huku tukimtathmini kwa yale aliyoyafanya na anayoyafanya sasa, badala ya kumbebesha lawama za makosa yaliyotokea katika vipindi tofauti vya historia ya taifa letu.
Sitanii, nafahamu msomaji umeishayasikia mambo mengi. Jambo moja nilisisitize kuwa wazo ninalolisikia kuwa tuichome moto nchi tuanze upya, sidhani kama ni sahihi. Kubomoa ni rahisi kuliko kujenga. Tuangalie nchi kama Ukraine, Iraq, Libya, Afghanistan na nyingine zilizoingia katika vita ya kweli leo zikoje. Wamepigana sana, ila mwisho wa siku wamerejea kwenye meza ya mazungumzo.
Nahitimisha makala hii kwa ombi kwa Watanzania. Naomba tusirejee ya Oktoba 29, 2025. Kwamba pande mbili zipimane msuli, haina masilahi kwa taifa letu. Uhai wa Watanzania ni muhimu kuliko mtu mmoja au wawili kuingia Ikulu.
Cha msingi, haki itamalaki. Asionewe mtu, anayeshinda uchaguzi atangazwe na mwenye kesi inayotafsiriwa kuwa ya kisiasa ifutwe. Naomba tusiandamane Julai 7, 2026, tulinde uhai. Rais Samia ameishaanza kusahihisha makosa ya kihistoria. Tumpe nafasi. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827

