Na DK. Reuben Lumbagala, Tanga
Suala la utunzaji mazingira ni la muhimu kutokana na umuhimu wake kijamii, kimazingira na kiuchumi. Mwanadamu ambaye ni sehemu ya mazingira anapaswa kuhakikisha anayatunza ili kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri na salama kwa kuishi.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumetokea majanga katika mazingira. Binadamu amekuwa akiharibu mazingira, hali inayochangia mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mbalimbali duniani.
Mathalani, mabadiliko hayo yamesababisha upungufu wa mvua katika maeneo mbalimbali na hivyo kusababisha upungufu wa chakula hasa katika maeneo yanayotegemea kilimo cha mvua.
Kutokana na madhara ya uharibifu wa mazingira, juhudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali, mashirika, taasisi na wadau mbalimbali kuhakikisha madhara hayo yanapungua kama si kumalizika kabisa kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa likiwemo suala la upandaji miti katika sehemu mbalimbali.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeamua kuwa sehemu ya utunzaji mazingira nchini. Hatua iliyochukuliwa na Mamlaka hii ni kupanda miti 3,850 nchi nzima katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Julai 1, 1996.
Miti hiyo, ikiwemo ya matunda, imepandwa maeneo mbalimbali zikiwemo taasisi za elimu kama shule. Upandaji wa miti hiyo ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa mazuri, salama, tulivu na yenye kuchochea maendeleo ya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Juni 28, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda ameshiriki zoezi la upandaji miti katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja ya Jijini Dar es Salaam, ambapo miti 30 ilipandwa shuleni hapo.
Katika tukio hilo, Kamishna Mwenda amewashukuru wananchi kwa kulipa kodi kwa maendeleo, ambapo upandaji miti hiyo ni alama ya walipakodi shuleni hapo.
“Walipakodi wamechangia kiasi kikubwa katika kuliletea maendeleo Taifa, miti hii ni alama kwa wanafunzi kuwa wazazi wao wanalipa kodi, hivyo nao kubakia na ujumbe. Huko mbele watakuja kuwa walipakodi, ni muhimu sote kutambua ulipaji kodi ni jukumu la kila mmoja,” amesema Mwenda.
TRA KUGHARAMIA UTUNZAJI WA MITI HIYO KWA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA
Katika kuonyesha upekee wa zoezi hilo la upandaji miti, Kamishna Mwenda amesema TRA itatoa fedha kwa kipindi cha mwaka mmoja, iwe ni motisha katika maeneo yote yaliyopandwa miti hiyo ili miti hiyo itunzwe na hatimaye ikue kutimiza malengo ya kupandwa kwake.
Aidha, kwa taasisi za elimu kama shule, Mwenda amesisitiza kuwa, Mamlaka ya Mapato, itatoa fedha kwa wanafunzi na walimu watakaosimamia utunzaji wa miti hiyo kufanikisha mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na utunzaji mazingira.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Miaka 30 ya TRA; Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea kwa Taifa Letu.”





