Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
WATOTO waishio na kufanya kazi mitaani wapatao 4,200 wanatarajiwa kuokolewa kupitia mradi wa miaka mitatu utakaowarejesha kwenye familia zao, kuwapatia elimu, huduma za afya na stadi za maisha ili kuwawezesha kujenga maisha bora.
Kati ya watoto hao, ni pamoja na halmashauri tano za Mkoa wa Pwani ambazo sasa zimeingizwa kwenye utekelezaji wa mradi wa Children in Street Situations (CiSS) Project 2026–2028.
Meneja wa mradi huo kutoka SOS Children’s Villages, Damas Damas, alisema mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni 6.3 ulianza kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza kuanzia mwaka 2023, na baada ya kupata matokeo mazuri umeongezwa katika mikoa ya Pwani na Arusha kwa kipindi cha 2026–2028.
Alieleza hadi sasa watoto 1,901 wameokolewa, huku 1,017 wakirejeshwa na kuunganishwa na familia zao, ambazo pia zinawezeshwa kiuchumi ili ziweze kuwahudumia watoto hao.
Damas alifafanua Mkoa wa Pwani umeathirika na changamoto hiyo kutokana na kuwa lango linalounganisha mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa, Kigoma na Mwanza.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa ushirikiano kati ya SOS Children’s Villages, Serikali kupitia halmashauri na Idara za Ustawi wa Jamii.
Akimwakilisha mgeni rasmi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Ukio Kusirye, alisema maandalizi ya awali yamekamilika katika halmashauri zote na sasa mradi unaingia hatua ya utekelezaji, huku Serikali ikiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha.
Alisema katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 2026, Mkoa wa Pwani ulirekodi watoto 36 waishio mitaani na kwamba mradi huo unatarajiwa kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kusirye, sababu kuu zinazowasukuma watoto kuishi mitaani ni migogoro ya kifamilia na kutengana kwa wazazi inayochangia kati ya asilimia 70 hadi 80 , umaskini, malezi ya mzazi mmoja, ukatili wa kijinsia na ukosefu wa makazi.
Alisema mazingira hayo huwafanya watoto kuwa katika hatari ya kubakwa, kulawitiwa, kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, kupata magonjwa ya akili na kuambukizwa magonjwa mbalimbali.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Pwani, Eliudy Malesa, aliitaka jamii kushirikiana na mamlaka husika pamoja na familia kuepuka migogoro isiyo ya lazima ili kuzuia watoto kukimbilia kuishi mitaani.







