Na Mwandishi Wetu, Kondoa
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kidini katika kuboresha huduma za jamii, hususan sekta za elimu, afya na malezi, kwa kutambua mchango mkubwa wa taasisi hizo katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Akwilapo ameyasema hayo Juni 28, 2026, mkoani Dodoma aliposhiriki Harambee ya Ujenzi wa Nyumba za Walimu katika Shule ya St. Peters and St. Paul Secondary School iliyopo Wilaya ya Kondoa. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Askofu Given Gaula, pamoja na viongozi na waumini wa kanisa hilo.
Katika hafla hiyo, Waziri huyo alishiriki pia ibada maalumu ya kumsimika mfadhili kutoka Uingereza, Bw. Peter Ruxton, kuwa Lay Canon wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya elimu na shughuli za kanisa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Akwilapo alisema Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais ya kuimarisha ushirikiano na madhehebu mbalimbali ya dini kwa lengo la kuboresha huduma za jamii zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
“Rais amekuwa akituambia kuwa ataendelea kushirikiana na madhehebu ya dini, na azma yake ni kuboresha huduma za jamii,” alisema Dkt. Akwilapo.
Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Kanisa la Anglikana katika sekta ya elimu, akibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu, kanisa hilo linaendesha shule za awali 39, shule za msingi 40, shule za sekondari 17, vyuo vya kati 17 pamoja na chuo kikuu kimoja.
Alieleza kuwa taasisi hizo zimeendelea kutoa mchango muhimu katika kuwajengea vijana maarifa, maadili, uzalendo na hofu ya Mungu, mambo ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
Aidha, Dkt. Akwilapo aliipongeza Dayosisi ya Kondoa kwa juhudi zake za kupanua huduma za elimu kwa kuongeza idadi ya shule, akieleza kuwa hivi karibuni shule nyingine itazinduliwa katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt Given Gaula, amesema ili kumtia moyo mfadhili anayesaidia maendeleo ya kanisa ikiwemo ujenzi wa shule waumini wa kanisa hilo wanapaswa kuchanga fedha kwa ajili ya maendeleo ya ujenzi wa nyumba za walimu.
‘’Shule zinazoendeshwa na kanisa la Angilikana hapa Kondoa zimeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watoto kwa kutoa elimu bora bila ubaguzi wa dini au itikadi’’. amesema
Jumla ya shilingi milioni tano zilichangwa katika hafla hiyo ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono mfadhili anayejenga nyumba za walimu katika Shule za St. Peters and St. Paul Secondary School iliyopo Wilaya ya Kondoa
Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo alimpongeza Bw. Peter Ruxton baada ya kusimikwa kuwa Lay Canon, akisema ametoa mchango wa kipekee katika maendeleo ya elimu na shughuli za kanisa kwa miaka mingi.
Alisema Serikali inathamini mchango wa mfadhili huyo, ambaye amesaidia kujenga na kuendeleza shule mbalimbali pamoja na kuchangia maendeleo ya taasisi za kidini zinazotoa huduma kwa jamii bila ubaguzi.
Naye Askofu Dkt Given Gaula alisema Bw. Ruxton amekuwa mshirika muhimu wa Dayosisi ya Kondoa, akibainisha kuwa karibu asilimia 97 ya shule zinazomilikiwa na dayosisi hiyo zimejengwa kwa msaada wake.
Aidha, amesema mfadhili huyo amechangia ununuzi wa mabati kwa makanisa mengi yaliyopo vijijini na kusaidia miradi mingine ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za kidini na wadau wa maendeleo unaendelea kuwa chachu muhimu katika kuimarisha elimu, kuboresha ustawi wa jamii na kuharakisha maendeleo ya taifa.











