WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania waendelee kuhimizana kuhusu ulinzi wa Taifa na kamwe wasipuuze viashiria vya uvunjifu wa amani.
“Tuendelee kuhimizana kuhusu suala la ulinzi wa Taifa letu. Ulinzi wa Taifa letu ni wa kila Mtanzania na amani yetu ni ya kila Mtanzania.”
“Sasa hivi hatupaswi kupuuzia viashiria vya uvunjifu wa amani hapa nchini. Hatutakiwi kuvipuuza kwa sababu vimetuachia doa,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumapili, Juni 28, 2026) katika ibada maalumu ya kilele cha harambee iliyofanyika kwenye usharika wa Amani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, mjini Singida.
Harambee hiyo ambayo ni ya nne kufanyika, ililenga kukusanya sh. bilioni 1.4 kwa ajili ya kuboresha vituo vya huduma za afya, kuimarisha vituo vya huduma za elimu, utumishi na uinjilisti vya Dayosisi hiyo ambavyo vinapaswa kukamilika ifikapo Desemba, mwaka huu.
Jumla ya sh. bilioni 1.331 zilikusanywa zikiwa ni fedha taslimu na ahadi. Waziri Mkuu amesema sh. milioni 69 zilizobakia, zitakamilishwa ndani ya wiki ijayo kutokana na ahadi zilizotolewa na watu mbalimbali na timu aliyoiunda yeye ili isimamie kukamilishwa kwa ahadi hiyo.
Mapema, akitoa mahubiri kwenye ibada hiyo, Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dkt. Alex Gehazi Malasusa alisema kupitia harambee hiyo, washarika wamepewa nafasi ya kumrudishia Mungu shukrani kwa ukarimu aliowatendea maishani mwao.
“Kila tunachokifanya kinapaswa kimtukuze Mungu, mali na fedha zetu ziwe za halali, zisitokane na kuwakanyaga wengine. Mali na fedha zetu zitawaliwe na Mungu,” alisisitiza.
Naye, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kati, Dkt. Cyprian Hilinti alisema kanisa hilo linaendelea kutekeleza jukumu la kuwaombea viongozi wa nchi kila Jumapili ikiwemo kuombea amani baina ya kabila na kabila, wakulima na wafugaji na vyama kwa vyama.
“Tunatamani kuona msamaha ukipatikana katika nyanja tofauti. Msamaha ni dawa,” alisema.
Alisema tangu waanze harambee hiyo miaka minne iliyopita, majimbo nane yamezaliwa, sharika mpya 27 zimezaliwa, wamepata washarika wapya 17,364 na wachungaji wapya 65.
Kwa upande wa huduma za jamii, Askofu Hilinti alisema wamefanikiwa kusajili shule mpya mbili za sekondari, shule moja ya msingi inayofundisha kwa Kiingereza (English medium) na akatumia fursa hiyo kuwashukuru washarika wote wa Dayosisi hiyo kwa kujitoa kwao katika kipindi chote hicho.







