Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imesisitiza kuwa mjadala kuhusu deni la Taifa unapaswa kuongozwa na uhalisia wa kiuchumi badala ya propaganda, ikieleza kuwa mikopo inayochukuliwa si mali ya mtu mmoja mmoja bali ni deni la Serikali linalowekezwa katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha Watanzania wote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 28, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali haikopi fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida au kugawana, bali huzielekeza kwenye sekta za kimkakati kama umeme, reli, barabara, maji, afya, elimu, kilimo na usafiri ambazo zinaongeza uzalishaji wa uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Msigwa amesema hadi Machi mwaka huu deni la Serikali lilifikia Sh trilioni 114.34, ambapo Sh trilioni 75.89 ni deni la nje na Sh trilioni 38.44 ni deni la ndani, huku akisisitiza kuwa tathmini ya uhimilivu wa deni inaonyesha Tanzania bado iko ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa.
Ameeleza kuwa uwiano wa deni kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.7, chini ya ukomo wa asilimia 55, jambo linaloonyesha nchi bado ina uwezo wa kukopa na kulipa bila kuhatarisha uchumi.
“Serikali haikopi pesa ili kugawana kama njugu,tunakopa kwa ajili ya kujenga uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi. Deni hili ni la Serikali, si deni la mtu mmoja mmoja,” amesema.
Msigwa amesema hoja kwamba Tanzania isikope haina msingi kwa kuwa hata mataifa makubwa duniani hutumia mikopo kufadhili miradi ya maendeleo, akiongeza kuwa kinachopaswa kuhojiwa si ukubwa wa deni bali fedha hizo zimefanya kazi gani.
Ametaja mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ulioigharimu Serikali zaidi ya Sh trilioni 6.5, ambao umeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuondoa tatizo la mgao lililokuwa likikwamisha ukuaji wa viwanda na uwekezaji.
Katika sekta ya usafiri, amesema uwekezaji katika reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege mpya 15 za ATCL, pamoja na maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam umeongeza ufanisi wa uchumi, huku bandari ikiongeza shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 16.27 hadi milioni 27.76 ndani ya miaka minne.
Kwa mujibu wa Msigwa, mapato ya ndani yanaendelea kuimarika ambapo bajeti ya mwaka 2026/27 yenye thamani ya Sh trilioni 62.33, asilimia 74.2 itagharamiwa na mapato ya ndani, hatua aliyoitaja kuwa ushahidi wa kujenga uchumi unaojitegemea.
Amesema wastani wa makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umefikia karibu Sh trilioni 3 kwa mwezi, tofauti na takribani Sh bilioni 25 zilizokuwa zikikusanywa kabla ya kuanzishwa kwa TRA mwaka 1995.
Kwa upande wa uchumi, Msigwa alisema ukuaji wa uchumi ulifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki katika kiwango salama cha asilimia 3.4.
Amewataka Watanzania kupuuza taarifa zinazolenga kupotosha kuhusu deni la Taifa na badala yake kutazama matokeo ya uwekezaji huo katika miradi mikubwa ya maji, umeme, barabara, afya, elimu, kilimo na miundombinu mingine ambayo imeendelea kubadilisha maisha ya wananchi.
Amesisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana nchini leo yametokana na matumizi ya mikopo yenye tija pamoja na ongezeko la mapato ya ndani, akisema Serikali itaendelea kutumia mikopo kwa tahadhari ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.







