Na Mwandishi Wetu

UJUMBE wa walimu na viongozi wa elimu kutoka Mkoa wa Dodoma wapatao 40 umeondoka kwenda Korea Kusini kujifunza, namna ya kufundisha, kusimamia shule na kutumia teknolojia katika elimu.

Ujumbe huo unatarajiwa kushiriki programu ya mafunzo na ziara ya kielimu ya siku nne kamili nchini Korea Kusini, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa walimu walioonesha utendaji bora na kufanikisha ongezeko la ufaulu wa wanafunzi katika Mkoa wa Dodoma.

Mratibu wa safari hiyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Molle alisema walimu hao waliondoka juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Juni 27, 2026, kuelekea Seoul, Korea Kusini, kupitia Doha, Qatar.

Alisema ziara hiyo ya kimasomo itafanyika kwa siku nne, ambapo walimu na viongozi wa elimu wanatarajiwa kushiriki katika mafunzo, kubadilishana uzoefu na kujifunza kuhusu matumizi ya teknolojia, ubunifu, uongozi wa shule na mbinu za kisasa za ufundishaji.

Alisema katika ziara hiyo ya siku nne, ujumbe unatarajiwa kujifunza namna Korea Kusini inavyotumia teknolojia, ubunifu, nidhamu na usimamizi bora katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.

Alisema walimu wanatarajiwa kupata uzoefu kuhusu matumizi ya vifaa na mifumo ya kidijitali darasani, maandalizi ya masomo, ushirikishwaji wa wanafunzi na ufuatiliaji wa maendeleo yao ya kitaaluma.

Alisema kabla ya safari hiyo, walimu na viongozi wa elimu waliomo katika ujumbe walipatiwa mafunzo maalumu ya maandalizi ambapo walielezwa kuhusu mazingira ya Korea Kusini, utamaduni wa nchi hiyo, nidhamu, utunzaji wa muda na wajibu wao kama wawakilishi wa Mkoa wa Dodoma na Tanzania.

Alisema mbali na kushiriki katika udhamini, taasisi ya Global Education Link imeratibu maandalizi mbalimbali ya ujumbe na kutoa mwongozo muhimu kwa washiriki kabla ya kuondoka nchini.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mollel aliwataka washiriki kutumia safari hiyo kama fursa ya kujifunza na kurejea na maarifa yatakayoweza kuleta mabadiliko yanayoonekana katika shule za Mkoa wa Dodoma.

Alisisitiza kuwa lengo la safari si kufika na kutembelea Korea Kusini pekee, bali kupata uzoefu wa kimataifa kuhusu matumizi ya teknolojia katika elimu, mbinu za kisasa za ufundishaji, usimamizi wa shule na mikakati ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipatiwa maelezo kuhusu jiografia, uchumi, maendeleo ya teknolojia, hali ya hewa, utamaduni, mila na mfumo wa elimu wa Korea Kusini.

Pia walielekezwa kujiandaa kisaikolojia na kimwili, kuheshimu muda, kufuata ratiba rasmi na kuzingatia sheria na utamaduni wa nchi watakayotembelea.

Mollel alisema safari hiyo ni matokeo ya jitihada za Mkoa wa Dodoma za kutambua, kuthamini na kuwapa motisha walimu walioonesha utendaji mzuri katika kutekeleza majukumu yao na kuwasaidia wanafunzi kupata matokeo bora.

Alisema mpango huo ulitokana na Mkutano wa Wadau wa Elimu wa Mkoa wa Dodoma uliofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mollel alisema mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa Serikali, walimu, maofisa elimu, viongozi wa shule, taasisi za umma, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo ya elimu.

Molle alisema katika mkutano huo, walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya kitaaluma zilitambuliwa na kupongezwa kutokana na mchango wao katika kuinua kiwango cha elimu mkoani Dodoma.

Alisema mpango wa kuwapeleka walimu Korea Kusini ulianzishwa kama sehemu ya kutoa motisha kwa walimu walioonesha kujituma, nidhamu, uwajibikaji na mafanikio katika kufundisha na kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri.

Alisema safari hiyo imefanikishwa kupitia ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na wadau mbalimbali wa elimu, wakiwamo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Benki ya NMB na Global Education Link.

Alisema ushirikiano huo unaonesha namna Serikali na wadau wanavyoweza kuunganisha nguvu katika kutambua utendaji bora na kutoa fursa za maendeleo ya kitaaluma kwa walimu.