Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe.Kanali Yahya Ramadhan Kido, ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kagera kwa kufanikisha usambazaji wa bidhaa za afya kwa wakati zenye thamani ya shilingi bilioni 29 ambayo ni sawa na 86% ya lengo walilojiwekea katika mwaka wa fedha 2025/2026.Hatua hiyo imewezesha kuinua hali ya utoaji huduma katika mikoa inayohudumiwa na kanda hiyo, ambayo ni Kagera na Geita.
Mhe.Kanali Kido ametoa pongezi hizo wakati akifungua kikao cha Wateja na Wadau wa MSD Kanda ya Kagera kwa mwaka 2026, ambapo amesema kutokana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuongeza fedha za ununuzi wa bidhaa za afya, Kanda ya MSD Kagera imefanikisha upatikanaji wa huduma zake kwa mikoa wa Kagera na Geita kwa wastani wa as 75.8% kutoka 64% za mwaka jana hivyo kuboresha hali ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Aliongeza kuwa MSD Kagera imefanikiwa kusambaza bidhaa za afya kwa ufanisi mara sita kwa kila kituo mwaka wa fedha 2025/2026, hatua iliyoongeza hali ya upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya na kupunguza malalamiko ya wananchi wa mikoa ya Kagera na Geita.
Mhe. Kido amesema upatikanaji wa bidhaa za afya umeendelea kuongezeka katika mikoa ya Kagera na Geita, ambapo kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 87.6 kwa Mkoa wa Kagera na asilimia 86 kwa Mkoa wa Geita. Alisema mafanikio hayo yanadhihirisha maboresho yanayoendelea kufanywa na serikali katika mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya kupitia MSD ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Pamoja na mafanikio hayo, Kanali Kido alieleza kuwa MSD Kagera bado inakabiliwa na changamoto ya ukusanyaji wa madeni, ambapo hadi Juni 20, 2026, Mkoa wa Kagera ulikuwa unadaiwa shilingi bilioni 7.3 huku Mkoa wa Geita ukidaiwa shilingi bilioni 2.0, na kufanya jumla ya deni kufikia shilingi bilioni 9.3, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya shilingi milioni 800 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka viongozi wa halmashauri na vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanatumia vyanzo vyao vya mapato kulipa madeni hayo kabla ya kuanza mwaka mpya wa fedha, akisisitiza kuwa kutolipa madeni kunadhoofisha uwezo wa MSD wa kuendelea kusambaza bidhaa za afya kwa wakati.
Aidha, Mkuu wa huyo wa Mkoa aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wafamasia wa ngazi zote kuimarisha usimamizi wa matumizi ya bidhaa za afya ili kudhibiti upotevu na kuhakikisha rasilimali za serikali zinatumika kwa tija.













