Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU), kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili waliokuwa wakitorosha mifugo 254 kwenda nchi jirani kwa njia ya magendo.

Akitoa taarifa hiyo , Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini (STPU), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ( SACP)Simon Pasua, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika Kijiji cha Olkesumet, Kata ya Sinonik, Wilaya ya Longido, Mkoani Arusha, wakiwa na mifugo hiyo ambayo ni ng’ombe 70 pamoja na mbuzi na kondoo 184.

Kamanda Pasua amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.

Aidha, amewataka wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kote nchini kuzingatia sheria na kuwa wazalendo kwa kulipia ushuru wa usafirishaji wa mifugo bila shuruti huku akisisitiza kuwa ulipaji ushuru kwa usafirishaji wa mifugo, hususan inayopelekwa nje ya nchi, ni wajibu wa kisheria na si hiari.

Katika hatua nyingine, Kamanda Pasua ametoa wito kwa wananchi, hasa wanaoishi maeneo ya mipakani, kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu uhalifu wa mifugo, ikiwemo utoroshwaji kwa njia ya magendo.

Akasisitiza Pia vitendo vya utoroshaji wa mifugo vinachangia kuikosesha Serikali mapato, pamoja na kusababisha ukiukwaji wa taratibu na haki za wanyama, hivyo ni muhimu jamii kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na uhalifu huo.