Na Mwandishi Wetu, Jamhuri, Shinyanga

Waziri wa Nishati na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kiserikali, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Manispaa ya Kahama kuongeza kasi ya ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ili likamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo Agosti 9, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo na kubaini kuwa, licha ya taarifa kuonesha mradi umefikia asilimia 80, hali halisi ya utekelezaji hairidhishi na haioneshi kiwango hicho cha maendeleo.

Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, hivyo fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Ameitaka Manispaa ya Kahama kukaa pamoja na mkandarasi na kupitia changamoto zote zinazokwamisha utekelezaji wa mradi huo, ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka na ujenzi uendelee kwa kasi inayostahili.

“Fedha hizi Shilingi bilioni 6.7 si fedha kwa ajili ya Halmashauri kuzichukua na kukaa nazo, ni fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Kahama kwa huduma bora za afya. Tunatamani kuona fedha hizi zinaongeza thamani kwa wananchi wa Kahama, hivyo mhakikishe mnasimamia jengo hili likamilike kwa wakati,” amesema Mhe. Ndejembi.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewapongeza viongozi wa Manispaa ya Kahama kwa hatua wanazochukua katika kutenga na kuelekeza rasilimali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga Shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) pamoja na Jengo la Vipimo katika Hospitali hiyo.

Mhe. Mhita amesema uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha miundombinu na huduma za afya nchini, akieleza kuwa Rais anatambuliwa kwa msisitizo mkubwa anaouweka katika kuboresha afya ya mama na mtoto.

Amesema fedha hizo zimekuwa chachu kwa Mkoa na Halmashauri kuongeza juhudi na kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za afya, huku akimhakikishia Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa Mkoa utaendelea kuusimamia kwa karibu mradi huo hadi utakapokamilika.

Aidha, Mhe. Mhita amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuendelea kuuwezesha Mkoa wa Shinyanga katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, hususan katika sekta ya nishati, ikiwemo mradi wa umeme unaoendelea katika Wilaya ya Kishapu.