Na Allan Kitwe, JmahuriMedia, Sikonge

SHIRIKA la Umeme (TANESCO) wilayani Sikonge Mkoani Tabora limepewa muda wa siku 14 kuhakikisha umeme unafikishwa kwenye Kituo cha Afya Kiloleli ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa jana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Wazo Michael Mwang’onda alipokuwa akitoa salamu za mwenge kwa wakazi wa Kata ya Kiloleli Wilayani humo.

Amesema kuwa serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

‘Kituo kimekamilika kwa asilimia kubwa yamebakia mambo machachetu, wananchi sasa wanaweza kupata huduma, nguzo naona ziko hapa, nimeambiwa hakuna transfoma, TANESCO na wapa wiki 2 umeme uwe umefika hapa’, ameagiza

Mwang’onda amesisitiza kuwa dhamira ya Mheshimiwa Rais kutoa fedha za ujenzi wa Kituo hicho ni kusaidia wananchi wapate huduma karibu na maeneo yao nasio kutembea umbali kwenda Kata jirani.

‘Hizi fedha ni nyingi sana, kazi iliyobaki ni ndogo tu, Meneja wa TANESCO Wilayani hapa nataka ndani ya siku 14 umeme uwake kwenye Kituo hiki, na nipewe taarifa’, ameeleza.
Kiongozi huyo amefafanua kuwa kila taasisi ya umma ipo kwa ajili ya kutumikia wananchi, kama nguzo na umeme upo hapa hapa wawekeeni umeme ndani ya siku 14, aidha aliwataka kutunza miundombinu ya mradi huo.
Awali akisoma taarifa ya mradi kwa Kiongozi huyo kwani abaya Mkurgenzi Mtendaji wa Halmashauri Seleman Pandawe, Mtendaji wa Kata Khamis Abas ameeleza kuwa kukamilika kwake kutawaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu.

Mbunge wa Jimbo hilo Mhandisi Amos Maganga amemshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 3 katika Jimbo hilo.
Amebainisha wazi kuwa Mheshimiwa Rais anajali sana wananchi ndiyo maana ameendelea kuboresha miundombinu ya afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali mpya ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora.