Na Mwandishi wa OTR, Dar es Salaam

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuimarisha mikakati ya kutafuta vyanzo mbadala vya mitaji ili kuongeza uwezo wake wa kutoa mikopo kwa wakulima wengi zaidi na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Wito huo ulitolewa Dar es Salam, Jumamosi, Novemba 7, 2026, na Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Ojambi Masaburi, wakati wa ziara ya Kamati katika benki hiyo, iliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), yenye jukumu la kusimamia uwekezaji wa Serikali katika taasisi na kampuni za umma.

Mhe. Masaburi alisisitiza umuhimu wa benki hiyo kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali kwa kutumia njia mbalimbali za kuongeza mtaji, ikiwemo utoaji wa hisa, hati fungani na kuingia katika ubia wa kimkakati.

Alisema hatua hizo zitawezesha TADB kuimarisha mtaji wake na kupanua wigo wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu, hususan kwa wakulima na wafugaji wa maeneo ya vijijini wanaohitaji mitaji ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji.

Aidha, aliitaka benki hiyo kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma zake ili wakulima wengi zaidi waweze kuzitumia kuongeza uzalishaji na kipato, na hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Elibariki Kingu, alisema mafanikio ya TADB hayapaswi kupimwa kwa faida ya kifedha pekee, bali pia kwa matokeo ya uwekezaji wake katika kuboresha maisha ya wakulima.

Alisisitiza kuwa benki hiyo inapaswa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata mikopo, teknolojia na mbinu bora za uzalishaji.

Akifafanua hoja hiyo, alitoa mfano wa mkulima wa alizeti ambaye kwa kutumia mikopo na teknolojia bora anaweza kuongeza uzalishaji kutoka magunia 20 hadi 35 kwa ekari.

Vilevile, alishauri TADB kuelekeza nguvu zaidi kwa wakulima wanaozalisha mazao mashambani badala ya kutegemea zaidi wafanyabiashara wa mazao.

“Mnapaswa kujenga uhusiano wa moja kwa moja na wakulima katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji,” alisisitiza.

Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, alisema Serikali itaendelea kuiunga mkono TADB kwa kuimarisha mtaji wake, kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha na kushirikiana na washirika wa maendeleo ili kuongeza uwezo wa benki hiyo kutekeleza majukumu yake.

Alieleza kuwa TADB ina nafasi muhimu katika kuendeleza mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji na uchakataji hadi masoko.

“Serikali itaendelea kushirikiana na benki hiyo katika kutatua changamoto zinazoikabili na kuimarisha utendaji wake,” alisema Bi. Mauki.

Awali, akiwasilisha taarifa ya benki hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TADB, David Nghambi, alisema mtaji wa wanahisa wa benki hiyo umeongezeka kutoka Sh76.7 bilioni mwaka 2020 hadi Sh553.2 bilioni kufikia Septemba 2026.