* Ahamasisha majasiriamali kutumia fursa ya Maonesho hayo kukuza masoko na ajira
*Bidhaa za Wajasiriamali wa Tanzania Zatia Fora
Na OWM (KAM) – Kigali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema maonesho ya Jua Kali yameendelea kuwa chachu ya kukuza biashara, masoko, kuimarisha umoja na ushirikiano na utengamano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mhe. Sangu amesema hayo Novemba 6, 2026, jijini Kigali, Rwanda, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku maalum ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Maonesho ya 26 ya Nguvu Kazi au Jua Kali yanayofanyika nchini humo.
Sangu amesisitiza ubunifu na kueleza kuwa ni muhimu katika kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za wajasiriamali katika masoko ya ndani na kimataifa.
“Bidhaa zinazooneshwa katika maonesho haya ni ushahidi wa uwezo mkubwa na ubunifu wa wajasirimali wa Afrika Mashariki, hivyo niwahamasishe kutumia fursa zilizopo kuboresha zaidi bidhaa zenu na kuongeza thamani ili ziweze kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi,” amesema
Amesema, maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupanua masoko, kukuza biashara na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Kadhalika,Waziri Sangu amesema sekta hiyo ina nafasi kubwa katika kukuza maendeleo ya uchumi wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa yanatoa ajira kwa wananchi wengi na kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi pamoja na viwanda mbalimbali.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Dkt. Habib Kambanga amesema Maonesho hayo ya Jua Kali yamekuwa na manufaa makubwa kwa Wajasiriamali kuweza kujifunza na kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kimataifa.
Kwa upade wake Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Forodha, Biashara na Fedha ni Bi. Annette Mutaawe amesema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itahakikisha inaondoa vikwazo vya biashara ili kuleta kuwawezesha wajasiriamali kufanya biashara na kukuza masoko yao.
Akizungumza kwa niaba ya wajasiliamali, Mwenyekiti wa Wajasiriamali wa Wadogo na wa Kati wa Ukanda Afrika Mashariki, Bw. Josephat Rweyemamu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwawezesha kushiriki maonesho hayo ya Jua Kali nchini Rwanda.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa jitihada inazotufanyia sisi wajasiriamali, Tanzania ni nchi ya amani na amani ndio mtaji mkubwa wa biashara. Bila amani huwezi kufanya biashara, tunashukuru nchi yetu Tanzania imeendelea kudumisha amani ambayo imewezesha wajasiriamali kufanya biashara,” amesema
Akitoa ushuhuda kuhusu maonesho hayo, Mjasiriamali wa Kukausha Mbogamboga na Matunda, Asia Tunduku alisema maonesho hayo yamemwezesha kuitangaza biashara yake ambapo kwa sasa anasafirisha bidhaa zake katika nchi ya Kenya. Pia amesema atatumia fursa ya maonesho hayo ya 26 ya Jua Kali yanayofanyika nchini Rwanda kuongeza wigo wa soko ukanda wa Afrika Mashariki.






