*Sasa tunauza saruji Msumbiji, Comoro na Zanzibar
*Bandari yaanza kupokea magari na mitambo ya ujenzi wa barabara

Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Mtwara

Wafanyabiashara na watumiaji wa Bandari ya Mtwara wamesema maboresho yaliyofanywa na Serikali, yakiwamo ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300, ununuzi wa vifaa vya kisasa na kuongeza rasilimali watu, yamerahisisha shughuli zao za biashara na kuongeza ufanisi wa bandari hiyo.

Wamesema maboresho hayo yameongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli na mizigo mbalimbali, huku yakifungua fursa za ajira na biashara kwa wakazi wa Mtwara na maeneo mengine nchini.

Kiwanda cha Dangote
Ofisa Lojistiki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Stephen Nhwagay, anasema majukumu yake ya kila siku ni kusimamia malori yanayosafirisha saruji kutoka kiwandani kwenda bandarini, ambako hupakiwa kwenye meli na kusafirishwa maeneo mbalimbali.

Anasema baada ya maboresho ya bandari hiyo, kampuni imeongeza uwezo wa kuwahudumia wateja wake, hasa wa Msumbiji, Comoro na Zanzibar, kwa kuwafikishia saruji kwa wakati.


“Kilichoongezeka baada ya maboresho ni kwamba tumeweza kusafirisha tani nyingi za saruji kwa wakati mmoja. Ukiangalia hapa, katika gati hili tunaweza kupakia saruji kwenye meli mbili hadi tatu kwa wakati mmoja, huku nyingine zikisubiri.

“Kama magati mengine hayana meli za korosho au makaa ya mawe, tunaweza kuhudumia meli nne kwa wakati mmoja,” anasema.

Anasema kwa wiki wanaweza kupakia meli tano, huku idadi ya malori yanayohitajika kutegemea ukubwa wa meli husika.

“Meli kubwa inaweza kuhitaji malori 150, nyingine 148 au 54. Lori moja linabeba tani 30 za saruji, sawa na mifuko 600,” anasema.

Anaongeza kuwa kampuni inaendelea kuwahudumia wateja wake kwa wakati na kwa ufanisi, huku malori yanayosafirisha saruji yakitumia gesi.

Kwa mujibu wa Nhwagay, Zanzibar ndiyo soko kubwa zaidi la saruji yao, ambako husafirisha wastani wa meli nne hadi tano kwa wiki.

Anasema meli moja inaweza kubeba tani 13,800 za saruji, sawa na mzigo wa malori 460, ambao huandaliwa na kupakiwa kwa wastani wa siku nne hadi tano.

“Ushauri wangu ni kuwakaribisha watumiaji wengine wa bandari. Sasa hivi kuna maboresho makubwa, japokuwa zipo changamoto ndogondogo ambazo uongozi wa bandari unaendelea kuzifanyia kazi.

“Serikali iongeze ukubwa wa magati. Ninaamini kuna uwezekano wa kujenga magati mengine. Watu waje kutumia fursa zilizopo. Kuna magari yanashushwa na msimu wa korosho unakuja. Bodaboda na mama lishe nao wanapata nafasi nzuri za kufanya biashara,” anasema.

Anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho ya bandari hiyo, lakini anasema barabara ya Mtwara hadi Dar es Salaam ina mashimo mengi yanayoathiri usafirishaji.

Anaomba ukarabati wa barabara hiyo uharakishwe ili kuongeza ufanisi wa shughuli za biashara.

Mawakala wa meli
Mshauri Elekezi wa Kampuni ya Inchcape Shipping Services (T) Ltd, Julius Mtenda, anasema kabla ya maboresho ya bandari hiyo, kampuni yao ilikuwa ikihudumia meli moja pekee.

“Sisi ni mawakala wa meli. Kwa muda mrefu tulikuwa katika mradi wa gesi kati ya mwaka 2011 na 2015. Tulipomaliza, tukawa tunapata kazi ya kuhudumia meli moja tu.

“Sasa hivi, baada ya maboresho, tunashughulikia kampuni ya Amicop inayosafirisha saruji kwenda Msumbiji baada ya kuipakia hapa Mtwara.

“Kuanzia hapo tukawa na shughuli nyingi zaidi. Kwa sasa tunahudumia meli tatu kwa mwezi, na si vibaya. Zamani changamoto kubwa ilikuwa kuchelewa kupakia mizigo, lakini sasa hatuchelewi,” anasema.

Mtenda anasema maboresho hayo yana manufaa makubwa kwa sababu bandari sasa ina magati manne baada ya kujengwa kwa gati jipya, pamoja na mashine za kisasa za kupakia na kupakua makontena.

Anawashauri wafanyabiashara kutumia Bandari ya Mtwara badala ya kusubiri kwa muda mrefu mizigo yao kushushwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Pia anaishauri Serikali kuendelea kuongeza vifaa na kuhakikisha vinafanya kazi wakati wote ili kuboresha huduma.

“Uongozi wa Bandari ya Mtwara ni msikivu. Tunapokuwa na changamoto, wanatusikiliza na kuzitatua,” anasema.

Naye Esthersia Malya wa Kampuni ya Joyous Shipping Services Ltd anasema ameshuhudia hatua mbalimbali za maboresho ya bandari hiyo na anaipongeza Serikali kwa kuzingatia mahitaji yanayotokana na ukuaji wa shughuli zake.

Anasema ujenzi wa gati jipya na ununuzi wa vifaa vya kisasa umeongeza uwezo wa bandari kushusha makontena, magari na mizigo mingine.

“Tumeona maboresho yakiendelea, kuanzia vifaa hadi mifumo inayorahisisha na kuharakisha kazi.

“Kabla tulitegemea shehena chache, lakini sasa tunapokea mafuta, magari na mizigo ya aina mbalimbali. Haya ni matunda ya maboresho yaliyofanyika.

“Ajira nazo zinaongezeka. Kwa mfano, mimi nahudumia meli kubwa zinazokwenda Zanzibar, Comoro, Madagascar na Msumbiji. Hapa nyuma yangu kuna meli ya Mtanzania ambayo mabaharia wake ni wazawa kabisa. Kwa hiyo, nao wananufaika na maboresho haya,” anasema.

Anaongeza kuwa ongezeko la meli bandarini limefungua fursa kwa makuli, madereva, wafanyabiashara na watoa huduma wengine.

“Kwa sababu meli zinakuja na kushusha mizigo kwa ufanisi na kwa muda mfupi, hata wazawa wanaohudumia soko la ndani wananufaika. Mizigo mingi inayoshushwa hapa inakwenda kutumika katika miradi ya hapa nchini.

“Makuli wanaofanya kazi bandarini nao wananufaika kwa sababu karibu kila siku kuna meli ya makaa ya mawe inayopakiwa,” anasema.

Malya anasema madereva pia wamepata fursa za kusafirisha magari yanayoshushwa bandarini kwenda kwa wateja katika nchi jirani, zikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda na Malawi.

Anasema maboresho ya bandari yanaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mingine, hasa barabara.

“Tunafaidika kwa sababu sasa hivi miundombinu inaboreshwa. Kwa mfano, barabara ya kutoka Mtwara Mjini kupitia Newala hadi Masasi inawekwa lami. Barabara ya Mnazi Mmoja kwenda Masasi nayo inajengwa kwa njia mbili.

“Safari za ndege zimeongezeka. Sasa tunazo hadi Jumapili, wakati mwanzoni tulikuwa na safari mbili tu. Yote hayo yamechangiwa na maboresho ya bandari kwa sababu watu wanakuja na kutoka kila siku. Ni maboresho tunayoyaona kwa macho,” anasema.
Malya anasema kampuni yao imekuwa ikifanya kazi bandarini hapo tangu kulipokuwa na gati moja, lakini sasa idadi imeongezeka hadi manne.

“Tumeona kasi ya maendeleo. Kwanza namshukuru Rais Samia kwa sababu TASAC (Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania) ilipitisha sheria iliyotuwezesha sisi mawakala kufanya biashara kwa uhuru.

“Tangu hapo tumekuwa na uwezo mkubwa wa kuwashawishi wateja wetu kutumia Bandari ya Mtwara.

“Tumewahakikishia wateja kuwa huduma zinapatikana hapa, nao wameitikia wito. Kwa sasa meli kubwa zinahudumiwa, hasa katika msimu wa korosho.

“Msimu huu tumehudumia meli za makontena na zile zinazobeba mizigo kwa wingi. Hata sasa wateja wameanza kufanya booking za meli hizo. Tunaona neema iko mbele yetu na tunaitumia ipasavyo,” anasema.

Anawashauri wafanyabiashara wanaodhani kuwa Bandari ya Dar es Salaam ndiyo pekee yenye fursa za biashara kuitembelea Bandari ya Mtwara.

“Njooni Mtwara muone maboresho yaliyofanyika. Fursa ni nyingi. Sasa hivi kuna mahitaji makubwa ya malazi, maegesho ya magari na maeneo ya kuhudumia mizigo nje ya bandari.

“Tunapoelekea, mizigo itaongezeka zaidi. Tunawakaribisha wafanyabiashara kuwekeza Mtwara,” anasema.

Kwa mujibu wa Malya, saruji ndiyo shehena kubwa inayohudumiwa na kampuni yao, ikifuatiwa na korosho. Pia wameanza kupata uzoefu wa kuhudumia meli zinazobeba magari.

“Saruji nyingi inakwenda Zanzibar, Comoro na Msumbiji. Tunaendelea kuwashawishi wateja wengine, wakiwamo wa Mogadishu, ambao wanahitaji meli za kusafirisha mizigo kwenda nchini mwao.

“Ushauri wangu ni tupende vya kwetu. Rais Samia anajitahidi kututumikia Watanzania na kutuwezesha,” anasema.

Anaongeza kuwa ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao utasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Mtwara na kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena mbalimbali.

“Binafsi ninafurahia hatua hiyo. Pia barabara ya kwenda Dar es Salaam ijengwe na kukamilika haraka ili wateja wawe na uhakika zaidi, hasa wanaosafirisha magari,” anasema.
Pamoja na mafanikio hayo, Malya anashauri kuongezwa kwa mashine zenye uwezo mkubwa, vifaa vidogo vya kuhudumia mizigo na nyavu za kufungia korosho ili kuongeza kasi ya utoaji huduma.

Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Nahodha Maritime Promotion Ltd, Omari Hassan, anasema zamani bandari hiyo ilikuwa ikihudumia meli chache, lakini maboresho na shughuli za Kiwanda cha Dangote vimechangia kuifanya kuwa kitovu muhimu cha uchumi katika ukanda wa kusini.

“Wamepanua bandari kwa ajili ya makontena. Zamani tulikuwa tunapakia makontena na saruji, lakini baada ya maboresho meli zimeongezeka.
“Maboresho yamesaidia kukuza uchumi wa ukanda wa kusini. Huku tunalima mazao yanayosafirishwa nje ya nchi, yakiwamo korosho, ufuta na mbaazi. Hilo ndilo lengo la kujenga Bandari ya Mtwara,” anasema.

Hassan anasema mabadiliko ya teknolojia na miundombinu yamewezesha meli kubwa kuanza kufika Mtwara zikiwa na magari na mitambo mbalimbali.

Anasema pia maboresho hayo yameongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaofanya kazi zinazohusiana na bandari.

“Sisi tunasafirisha saruji ya Dangote kutoka Mtwara kwenda Zanzibar, Msumbiji na Comoro, jambo ambalo zamani halikuwa katika kiwango hiki.

“Hapo ndipo ajira kwa vijana zinapatikana. Kwa mfano, meli moja inayopakia saruji inaweza kuwa na vijana 300 wanaofanya kazi hiyo. Wakimaliza, kila mmoja anapata ujira wake kulingana na kitengo chake,” anasema.

Hata hivyo, anasema pamoja na maboresho, bado kuna changamoto ya uhaba wa magati kutokana na kuongezeka kwa meli na mizigo.

Anasema shehena za saruji, makaa ya mawe, korosho, mbaazi, magari na bidhaa nyingine zimeongezeka, hivyo vifaa vilivyopo vinahitaji kuongezwa.

“Vifaa vikiongezeka, meli za Comoro zinaweza kukaa siku moja tu. Meli inakuja leo, tunapakia ndani ya saa 24 na inaondoka.

“Huo ndiyo uboreshaji tunaoutaka, japokuwa hali ya sasa ni nzuri zaidi kuliko zamani.

“Kipindi cha nyuma, tulipokuwa na gati moja, kwa mwaka mzima tulihudumia meli 20. Sasa tunapata meli 50 hadi 70 kwa mwaka. Changamoto kubwa iliyobaki ni kuongeza vifaa,” anasema.

Hassan anasema kazi kuu za bandari ni kupakia na kupakua mizigo, hivyo upatikanaji wa vifaa vya kutosha ni jambo la msingi.
“Vifaa vikiwa vya kutosha, kila kitu kitakuwa sawa. Zamani, wakati kulikuwa na gati moja, meli inaweza kuchukua hadi siku 10 kupakia mzigo.

“Hali hiyo ilikuwa inatutesa na ndiyo maana tulihudumia meli chache kwa mwaka. Baada ya maboresho, idadi ya meli imeongezeka,” anasema.

Anaongeza kuwa sasa meli moja inaweza kufika bandarini hata mara nne kwa mwezi kupakia mizigo, tofauti na ilivyokuwa zamani.

“Bahati nzuri si vijana wa Mtwara pekee wanaofanya kazi hapa. Wapo kutoka Mwanza, Singida, Arusha na maeneo mengine ya nchi. Kila mmoja anapata riziki kulingana na shughuli yake.

“Waliosoma na wasiosoma wanapata fedha. Kuna madereva wa magari yanayoshushwa na kupelekwa nchi jirani, waendeshaji wa mitambo ya kushusha makontena na makuli wa kada mbalimbali,” anasema.

Mawakala wa forodha
Msimamizi wa Kampuni ya Maxima Clearing and Forwarding Ltd, Venance Mrema, anasema kati ya mwaka 2020 na 2025 wameshuhudia maboresho makubwa ya Bandari ya Mtwara ambayo yameongeza fursa za biashara.
“Kwa upande wetu, mawakala wa forodha na wadau wengine wa bandari, shughuli za kiuchumi na biashara za kampuni zetu zimekua kutokana na maboresho haya,” anasema.

Mrema anasema mojawapo ya mabadiliko ni utaratibu wa kupakia makasha ya korosho nje ya bandari badala ya kufanya shughuli hiyo ndani, hatua inayotarajiwa kuongeza nafasi ya kuhudumia mizigo mingine.

“Yapo mabadiliko makubwa yaliyofanyika mwaka 2025. Upakiaji wa makasha ya korosho uliokuwa ukifanyika ndani ya bandari sasa unakwenda kufanyika nje.

“Hii itatoa nafasi ya mizigo mingi zaidi kushushwa Bandari ya Mtwara, jambo ambalo siku za nyuma halikuwezekana kwa kiwango hiki,” anasema.

Anaongeza kuwa zamani mawakala wa forodha walitegemea zaidi mizigo inayosafirishwa nje ya nchi, lakini sasa wanahudumia pia mizigo inayoingia nchini na ile inayokwenda nchi jirani.

“Wakala wa forodha ni kampuni zinazohusika na kuandaa nyaraka za mizigo inayosafirishwa nje ya nchi au kuingia nchini kupitia mipaka ya angani, ardhini na majini, kama Bandari ya Mtwara.

“Tunahakikisha nyaraka zimeandaliwa kwa usahihi na kuthibitishwa na mamlaka husika, kama TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na taasisi nyingine kulingana na aina ya mzigo,” anasema.

Mrema anasema maboresho ya bandari na maendeleo ya ushoroba wa kusini yamechangia ukuaji wa kampuni za uwakala wa forodha kutokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara.

“Kwa upande wetu, kazi zimeongezeka. Kabla ya maboresho, mizigo iliyoingia kutoka nje ya nchi kupitia bandari hii ilikuwa michache.

“Sasa shughuli zetu na kipato chetu vimeongezeka. Meli nyingi zaidi zinafika Mtwara kwa sababu nafasi ya kuhudumia mizigo imeongezeka,” anasema.

Anasema zamani meli ilipofika bandarini ingeweza kukaa karibu mwezi mzima ikisubiri kukamilisha upakiaji wa mizigo, lakini sasa muda umepungua kutokana na maboresho ya miundombinu na vifaa.

Kwa miaka ya karibuni, anasema mizigo inayosafirishwa zaidi nje ya nchi ni korosho na ufuta, huku shehena zinazoingia zikijumuisha magari, mitambo na bidhaa nyingine mbalimbali.

Mrema anapendekeza kujengwa eneo maalumu la kuhudumia madini kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji katika ukanda wa kusini.

“Tunatamani kujengwe eneo jingine la kuhudumia madini kwa sababu katika ushoroba wa kusini, kuanzia Lindi hadi Mtwara, kuna migodi iliyoanza shughuli za uchimbaji wa nikeli na madini mengine.

“Madini hayo yanaweza kusafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara, kwa hiyo mazingira yanapaswa kuandaliwa ili kuyahudumia,” anasema.

Anaipongeza Serikali, hasa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa hatua ya kuelekeza korosho za ukanda wa kusini kusafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.

Pia anasema ujenzi wa Bandari ya Kisiwa cha Mgao utakuwa na manufaa kwa kutenganisha shehena za aina mbalimbali.

“Ujenzi wa bandari hiyo utasaidia kuhudumia bidhaa kama saruji na makaa ya mawe, huku bidhaa nyingine, hasa za chakula, zikiendelea kuhudumiwa hapa.

“Kuwapo kwa saruji, makaa ya mawe na bidhaa za chakula kwa wakati mmoja kunaweza kusababisha baadhi ya wateja kuacha kusafirisha mizigo yao kupitia bandari hii,” anasema.

Mrema anasema wanapata ushirikiano mzuri kutoka taasisi zinazohusika na shughuli za bandari na forodha.

“Tunashukuru kwa ushirikiano mzuri wa kiutendaji kutoka taasisi zote, ikiwamo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, TRA, TBS, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na nyingine zilizopo katika mnyororo wa shughuli zetu,” anasema.