*Maboresho yaongeza uwezo wa bandari kupokea, kuhudumia shehena za korosho, saruji, magari, mbaazi, ufuta, mafuta na makaa ya mawe
Na Dennisi Luambano, JamhuriMedia, Mtwara
Maboresho ya Bandari ya Mtwara yaliyogharimu Sh bilioni 157.8 yameanza kufungua ukurasa mpya wa biashara katika ukanda wa kusini, huku kampuni zinazotumia bandari hiyo zikieleza kuongezeka kwa mizigo, kasi ya utoaji huduma na fursa za ajira
Uwekezaji huo umeongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo kutoka tani 400,000 hadi tani milioni 2.6 kwa mwaka, hatua inayotajwa kuongeza mvuto wake kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Tanzania.
Maboresho hayo yaliyokamilika Desemba 31, 2020, yameongeza uwezo wa bandari kupokea na kuhudumia shehena mbalimbali, zikiwamo korosho, mbaazi, ufuta, mafuta na makaa ya mawe.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, baadhi ya wadau wanazitaja changamoto zinazohitaji ufumbuzi, zikiwamo uhaba wa vifaa vya kisasa, vumbi la makaa ya mawe, ubovu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo na hitaji la kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa.
Katika mahojiano maalumu na JAMHURI yaliyofanyika mkoani Mtwara, wadau wa biashara na usafirishaji wameeleza namna maboresho hayo yalivyobadilisha shughuli zao na matarajio yao ya baadaye.

Makontena yaongezeka, ajira zafunguka
Msimamizi Mwandamizi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Makanjiro Ltd, Abdallah Darusi, anasema ongezeko la shughuli katika Bandari ya Mtwara limeifanya kampuni yao kupanua maeneo ya kuhifadhi na kuhudumia makontena.
Anasema kampuni hiyo ilipoanza shughuli zake mwaka 2024/2025 ilihudumia makontena 3,900, lakini idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 5,914.
Darusi anaeleza kuwa kampuni hiyo ilianza kama kituo cha kupokea, kupanga na kuhifadhi mizigo ya makontena, kinachofahamika kama Container Freight Station (CFS), kabla ya kuanza mchakato wa kupata vibali vya kuwa bandari kavu.
Anasema mwanzoni walikuwa na yadi yenye ukubwa wa mita za mraba 11,000, lakini kutokana na ongezeko la shughuli wameongeza yadi nyingine mbili, moja ikiwa na ukubwa wa mita za mraba 36,000.
“Pia tumeongeza yadi nyingine ya tatu. Hizo zote ziko chini yetu na mwaka huu tunatarajia operesheni zetu zitaongezeka baada ya bandari kuboreshwa.
“Bandari ya Mtwara inahitaji sisi tupokee mizigo ya ICD. Tunatarajia wakati wowote mambo yakiwa sawa tutapokea mizigo ya kuagiza kutoka nje kupitia ICD yetu,” anasema.
Darusi anasema kampuni hiyo inasubiri kukamilika kwa vibali ili kupanua shughuli zake rasmi kama bandari kavu.
Anaeleza kuwa mzigo mkubwa wanaoushughulikia ni korosho zinazokwenda nje ya nchi, huku upanuzi wa maeneo ya kuhifadhi makontena ukiwapa nafasi ya kuongeza wateja.
“Sasa hivi tuna uhakika wa kupokea makontena mengi zaidi kwa sababu tuna maeneo makubwa ya kuyahifadhi. Tukiyapokea tunapakia mzigo kabla ya kusafirishwa.
“Msimu wa korosho umefika na kila mtu atakuwa bize. Vijana wanapata ajira na idadi ya wafanyakazi wetu imeongezeka tofauti na msimu uliopita,” anasema.
Anaongeza kuwa kuimarika kwa shughuli za bandari kumechangamsha biashara katika ukanda wa kusini, huku kampuni nyingi zikitarajia kunufaika na ongezeko la shehena.
Darusi anawashauri wafanyabiashara kutumia Bandari ya Mtwara, akieleza kuwa ina nafasi ya kupunguza muda wa kusubiri huduma.
“Zamani meli nyingi zikifika Bandari ya Dar es Salaam zinakaa nje kwa muda mrefu kusubiri nafasi ya kuingia bandarini.
“Lakini sasa meli ikitoka China inaweza kuja kushusha moja kwa moja Mtwara bila ucheleweshaji mkubwa. Bandari inafanya kazi kwa saa 24,” anasema.
Mauzo ya nje yapaa, vumbi latia doa
Meneja Uendeshaji wa Export Trading Group Ltd, Dismas Mtui, anasema maboresho ya Bandari ya Mtwara yameongeza uwezo wa kampuni hiyo kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi.
Anaeleza kuwa kati ya mwaka 2012 na 2018 kampuni hiyo ilikuwa ikisafirisha kati ya tani 1,000 na 2,000 za mazao mchanganyiko, lakini kwa sasa kiwango kimefikia tani 52,000.
Mazao yanayosafirishwa ni pamoja na korosho, mbaazi na ufuta, huku masoko makubwa yakitajwa kuwa India na Vietnam.
Hata hivyo, Mtui anasema ongezeko la shughuli za makaa ya mawe bandarini limeibua changamoto ya vumbi, ambalo linaathiri usafirishaji na uchakataji wa mazao ya chakula.
“Makaa ya mawe yana vumbi jingi na kutokana na hali hiyo sasa tunasafirisha korosho peke yake, tena zisizobanguliwa.
“Tunaomba katika msimu wa korosho usafirishaji wa makaa ya mawe usitishwe kwa muda kwa sababu wakati wa kupakia korosho, makaa ya mawe nayo yanapakiwa na vumbi linaingia kwenye korosho,” anasema.
Mtui anaeleza kuwa kampuni hiyo imelazimika kufunga kiwanda chake cha kubangua korosho kutokana na changamoto hiyo.
“Tuna kiwanda hapa tumekifunga kwa sababu ya vumbi la makaa ya mawe. Huwezi kubangua korosho katika mazingira haya na ukibainika kibali chako kinaweza kufutwa. Kwa mwaka tulikuwa tunabangua tani 5,500,” anasema.

Anaamini ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao, unaotarajiwa kukamilika Septemba 2027, utasaidia kupunguza tatizo hilo kwa kuhamishia huko shughuli za makaa ya mawe na saruji.
Anasema hatua hiyo itatoa nafasi kwa kampuni zinazoshughulikia mazao ya chakula kufanya kazi katika mazingira salama zaidi.
“Makaa ya mawe yakihamishwa kwenda Kisiwa Mgao itatusaidia sisi wasafirishaji wa mazao. Vumbi hili linatutesa, si wasafirishaji tu, hata majirani wanaoishi karibu na bandari,” anasema.
Mtui anaongeza kuwa kiwanda chao kitahitaji kukaguliwa upya kabla ya kurejea katika shughuli za kubangua korosho.
Vifaa na barabara bado changamoto
Pamoja na kupongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa makontena, Mtui anasema Bandari ya Mtwara bado inahitaji kuongezewa vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo.
Anadai kuwa baadhi ya mashine zinazotumika si mpya na zinapoharibika husababisha kuchelewa kwa shughuli za wateja.
“Unakuta ICD nyingi zinaleta makontena, lakini wakati wa kushusha mashine moja inafanya kazi na nyingine zimeharibika.
“Tangu mwaka 2012 tulijaribu kuomba mashine mpya za kunyanyua makontena. Zinaletwa kutoka Dar es Salaam au Tanga, lakini wakati mwingine zinafanya kazi kwa muda mfupi na kuharibika,” anasema.
Anaeleza kuwa hali hiyo hulazimisha mafundi kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara kufanya matengenezo, jambo linaloongeza muda wa kusubiri huduma.
Mtui pia anataja ubovu wa barabara katika eneo la gati namba tatu kuwa changamoto inayohitaji kushughulikiwa.
“Tunaomba barabara itengenezwe kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika. Wafanyakazi wa bandari wako vizuri na wanafanya kazi kwa saa 24. Kwa hilo tunawapongeza,” anasema.
Mafuta yashushwa kwa kasi zaidi
Meneja wa Bohari ya Mafuta ya GM Tanzania Ltd, Paul Massawe, anasema maboresho ya bandari yameongeza ufanisi wa kupokea mafuta kutoka melini na kuyahifadhi katika matenki yao.
Anaeleza kuwa awali kampuni hiyo ililazimika kusimamia yenyewe shughuli nyingi za upakuaji mafuta, lakini sasa uongozi wa bandari umeimarisha huduma kwa wateja.
“Kwa kweli tumetoka mbali. Meli za mafuta zilipoanza kuja tulifanya kila kitu hadi mafuta kufika katika matenki yetu.
“Baadaye uongozi wa bandari ukaanza kuhakikisha shughuli hizo zinafanywa kwa utaratibu wa kuwahudumia wateja, kama ilivyo katika bandari nyingine kubwa,” anasema.
Massawe anasema maboresho hayo yamepunguza muda wa kuhudumia meli, huku kampuni yake ikiwekeza katika mabomba yanayoongeza kasi ya kupokea mafuta.
Anaeleza kuwa awali mafuta ya aina tofauti yalipitishwa katika bomba moja, ambalo lilihitaji kusafishwa kabla ya kupokea bidhaa nyingine.
Hata hivyo, kampuni hiyo imeweka bomba la inchi 12 kwa ajili ya dizeli, huku petroli ikiendelea kupita katika bomba la inchi nane.
“Zamani tulikuwa tunapokea tani 250 za dizeli kwa saa, lakini sasa tunapokea tani 600 kwa saa. Hiyo inapunguza muda wa meli kukaa bandarini na gharama za kutumia gati na miundombinu ya bandari,” anasema.
Wateja wa nchi jirani waongezeka
Massawe anasema kampuni hiyo ilipoanza kutoa huduma mwaka 2015 ilihudumia zaidi wateja wa Mtwara, lakini kuanzia Septemba 2025 imeanza kuvutia wateja wengi zaidi.
Anazitaja Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi na Uganda kuwa miongoni mwa nchi ambazo wateja wake wanatumia huduma za mafuta kupitia Mtwara.
“Unaweza kushangaa lori la mafuta linatoka Mtwara, linakwenda Dar es Salaam na kuendelea na safari ya Uganda kwa sababu ya kuepuka msongamano wa Bandari ya Dar es Salaam,” anasema.
Anaeleza kuwa ongezeko la shughuli limeongeza ajira katika kampuni hiyo kutoka wafanyakazi watano hadi 18 wa kudumu na wanane wa mikataba.
Kwa sasa, bohari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 54 za petroli na lita milioni 18 za dizeli, jumla ya lita milioni 72.
Massawe anasema ushauri wa Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, uliwahamasisha kuwekeza katika miundombinu kabla ya kusubiri kuongezeka kwa wateja.
“Alituambia tusisubiri fursa ya biashara ije. Tuandae miundombinu kwanza, ndipo fursa itakapokuja,” anasema.
Anaongeza kuwa matumizi ya mitambo ya kisasa ya kupima ujazo wa mafuta yamesaidia kuboresha udhibiti wa kiasi kinachopokelewa na kuwezesha ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Gati maalumu la mafuta lahitajika
Pamoja na mafanikio hayo, Massawe anapendekeza kujengwa kwa gati maalumu la mafuta lenye urefu wa mita 300 na kina kinachozidi mita 13.
Anasema gati linalotumika sasa linahudumia mizigo mchanganyiko, hivyo meli za mafuta wakati mwingine hulazimika kusubiri meli nyingine zimalize kupakua.
“Gati hilo linatumika kwa mizigo mchanganyiko. Meli ya mafuta ikifika na kukuta meli nyingine inashusha mizigo, inalazimika kusubiri,” anasema.
Meneja Msaidizi wa Bohari ya Mafuta ya GM, Respicious Haki, anasema kampuni hiyo inalenga kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi mafuta hadi lita milioni 200 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027.
Anaeleza kuwa upanuzi huo utategemea mahitaji ya soko na mgawanyo wa matenki ya petroli na dizeli.
“Mahitaji ya kuhifadhi mafuta yanaongezeka. Wateja wamekuwa wengi na wakati mwingine wanapokuja tunakosa nafasi, hivyo lazima tuongeze uwezo,” anasema.
Haki anapendekeza pia kuanzishwa kwa huduma ya kujaza mafuta kwenye meli, inayofahamika kama bunkering, ili kuongeza mapato na fursa za ajira.
Anasema baadhi ya meli zinazofika Mtwara hulazimika kupata huduma hiyo katika bandari nyingine, ikiwamo Mombasa.
Aidha, anashauri kuongeza kina cha gati namba tatu kutoka mita 9.5 hadi angalau mita 13 ili kuruhusu meli kubwa zaidi kuhudumiwa.
“Pia tunaomba kuongezewa mfumo wa mabomba kwa takribani mita 30 ili kuunganisha njia za mafuta kutoka melini hadi ardhini. Mfumo huo utatusaidia kushusha bidhaa mbili kwa wakati mmoja,” anasema.
Kwa wadau hao, maboresho ya Bandari ya Mtwara yameongeza fursa za biashara, lakini uwekezaji zaidi katika vifaa, miundombinu na utenganishaji wa mizigo unatajwa kuwa muhimu ili bandari hiyo itumike kikamilifu na kuchochea uchumi wa ukanda wa kusini.


