Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imepanua matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali katika udhibiti wa usafiri wa barabara na reli katika kipindi cha miaka mitano ya fedha kuanzia 2021/22 hadi 2025/26, ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni, ufuatiliaji wa mabasi, tiketi mtandao na udhibiti wa teksi mtandao.
Akizunguza na wahariri leo Septemba 24, 20206 Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dk Habibu Suluo amesema idadi ya leseni za usafirishaji iliongezeka kutoka 239,953 mwaka 2021/22 hadi 590,468 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 146.1. Ongezeko kubwa lilionekana katika magari ya kukodi, ambayo leseni zake zilifikia 322,081 kutoka 61,975 katika kipindi hicho.
Amesema kuwa mamlaka pia imeimarisha matumizi ya mfumo wa Railway and Road Information Management System (RRIMS), unaowezesha utoaji wa leseni, usajili wa madereva, malipo na huduma nyingine kwa njia ya mtandao. Mfumo huo umeunganishwa na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwamo TRA, TIRA, NIDA, GePG, Polisi na BRELA, huku waombaji wakiwa na uwezo wa kupata leseni zilizoidhinishwa bila kufika ofisini.
“Katika usalama wa mabasi, idadi ya magari yaliyounganishwa na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) iliongezeka kutoka 5,979 mwaka 2021/22 hadi 14,743 mwaka 2025/26. Aidha, matumizi ya vitufe vya utambuzi wa madereva (i-buttons) yaliongezeka kutoka madereva 256 mwaka 2022/23 hadi 13,829 mwaka 2025/26.
“LATRA pia imeendeleza huduma za tiketi mtandao kupitia Core e-Ticketing System (CeTS), inayounganisha huduma za tiketi za mabasi na treni za TRC. Katika kipindi cha miaka minne, mifumo ya tiketi ilihudumia abiria milioni 62.18, huku malipo ya nauli yakifikia takribani Sh trilioni 2.13, ingawa asilimia 95.3 ya abiria bado walitumia fedha taslimu’ amesema.
Amesema kuwa kwa upande wa rasilimali watu, madereva 15,547 walifanya mtihani wa uthibitishaji kupitia Drivers Testing System kati ya 2022/23 na 2025/26, ambapo 8,642 walifaulu. Wakati huo huo, wahudumu 7,216 walipata mafunzo na kufaulu kozi maalumu ya saa 60 iliyoandaliwa kwa kushirikiana na taasisi za mafunzo.
Katika sekta ya teksi mtandao, LATRA imesajili na kuidhinisha kampuni 22, huku vyombo vyenye leseni kupitia mifumo hiyo vikifikia 23,532. Kati yake, pikipiki za magurudumu mawili ni 11,407, pikipiki za magurudumu matatu 8,083 na magari 4,042, hatua inayoonesha kuongezeka kwa huduma za usafiri zinazotegemea teknolojia.
Kwa upande wa reli, LATRA ilifanya jumla ya kaguzi 275 katika kipindi cha miaka mitano, zikiwemo kaguzi 143 kwa TRC na 132 kwa TAZARA. Ukaguzi huo ulihusisha miundombinu, mifumo ya ishara na mawasiliano, vichwa vya treni, mabehewa na uendeshaji, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha usalama na ubora wa huduma za reli.
LATRA pia imepanua huduma zinazomfikia mwananchi moja kwa moja kupitia LATRA App na Passenger Information System (PIS), zinazomwezesha msafiri kupata taarifa za nauli, kuhakiki leseni na kufuatilia mwenendo wa mabasi. Aidha, katika kipindi hicho Mamlaka iliandaa vipindi 649 vya elimu kwa umma kupitia televisheni na mitandao ya kijamii kuhusu haki na wajibu wa abiria na watoa huduma.
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto inayobaki ni kuhakikisha mifumo na teknolojia zilizowekezwa zinatafsiriwa kuwa huduma bora kwa mwananchi. Kwa msafiri, kipimo cha mafanikio ya udhibiti ni usalama wa safari, upatikanaji wa taarifa sahihi, uwazi wa nauli, nidhamu ya madereva na wahudumu pamoja na kushughulikiwa kwa wakati kwa malalamiko.








