
Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, wametakiwa kujiandaa kutumia fursa za biashara, uwekezaji na utalii zitakazofunguliwa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ikiwemo biashara ya bidhaa zinazohitaji usafirishaji wa haraka kama matunda, mboga mboga, samaki, kuku na maua.
Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Septemba 24, 2026, kuhusu utekelezaji wa mradi huo unaoendelea kwa kasi na ambao unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema kukamilika kwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kutaiwezesha Dodoma kuwa na lango muhimu la usafiri wa anga kwa safari za ndani na kimataifa, hatua itakayosaidia kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, huku ikitoa nafasi zaidi kwa wafanyabiashara na wawekezaji kushiriki katika shughuli mbalimbali zitakazochochewa na uwepo wa uwanja huo.
Amesema Mradi huo unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), unalenga kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo na kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga katika ngazi ya kitaifa na kikanda.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unajengwa kwa hadhi ya Daraja la 4E kwa viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ukiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka pamoja na ndege kubwa aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 350.
Amesema ujenzi wa mradi huo unatekelezwa kupitia vifurushi viwili, ambapo Package 1 inahusu miundombinu na imefikia asilimia 89.02, huku Package 2 inayohusu majengo ikiwa imefikia asilimia 78.37.
Katika Package 1, ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege umefikia asilimia 98, taxiways asilimia 99 na apron asilimia 99, huku barabara za kuingia kiwanjani, barabara za ndani na maegesho ya magari zikifikia asilimia 75.
Kwa upande wa majengo,amesema ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, kituo cha huduma za zimamoto asilimia 88, kituo kikubwa na vituo vidogo vya umeme asilimia 71, huku jengo la huduma za hali ya hewa likifikia asilimia 87.
Ametaja Kazi zinazoendelea ni pamoja na umaliziaji wa majengo, ufungaji wa mifumo ya umeme, mitambo, TEHAMA na mawasiliano pamoja na vifaa vya ukaguzi wa mizigo na huduma za abiria.
Mtendaji Mkuu amesema barabara ya kurukia na kutua ndege itakuwa na urefu wa mita 3,600 na upana wa mita 45, ikiwa na mabega yenye upana wa mita 7.5 kila upande, huku miundombinu ikiandaliwa kuwezesha uwanja huo kutumika mchana na usiku katika majira yote ya mwaka.
” Package 1 inatarajiwa kukamilika Novemba 27, 2026, huku Package 2 ikitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026 na mradi huu tayari umetoa jumla ya ajira 9,059 kwa Watanzania katika kipindi chote cha utekelezaji, ambapo Package 1 imetoa ajira 3,571 na Package 2 ajira 5,488, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47,”ameeleza.
Kwa kuzingatia fursa hizo, amewataka wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kujiandaa kutumia mazingira mapya ya biashara na uwekezaji yatakayojitokeza baada ya kukamilika kwa uwanja huo.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu huyo amesema TANROADS inaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na utabiri wa hali ya hewa kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.
Amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na taasisi nyingine, Wakala unaendelea kukagua barabara, madaraja, makaravati na mitaro, kusafisha mifumo ya maji na kuandaa vifaa na wataalamu kwa ajili ya mwitikio wa haraka pale maeneo yatakapoathirika.
Amesisitiza wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua kubwa, akitumia ujumbe “Mvua ikiongezeka, tahadhari iongezeke,” pamoja na msemo “Kawia ufi ke.”








