📌 Yatambuliwa kwa kuzingatia Sheria na Taratibu za ulipaji kodi
📌 Utambuzi waakisi uwajibikaji wa REA katika utekelezaji wa miradi ya nishati
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umetunukiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Cheti cha Mlipakodi Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 kwa Taasisi za Umma, ikiwa ni kutambua kiwango bora cha Wakala katika kuzingatia taratibu za ulipaji kodi.
REA imeendelea kutekeleza matakwa ya kikodi kwa kuzingatia sheria na taratibu katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na utekelezaji wa maujukumu yake ikiwemo miradi ya nishati vijijini.
Utambuzi huo unaakisi dhamira ya Wakala ya kuendelea kuimarisha uwajibikaji na kuzingatia matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa vyeti hivyo jijini Dodoma, mgeni rasmi, Naibu Kamishna wa Operesheni, Idara ya Walipakodi Wakubwa, Bi. Eva Raphael, amesema hatua hiyo inalenga kutambua na kuthamini taasisi zilizoonesha kiwango kizuri cha uzingatiaji wa sheria na taratibu za kodi katika Mwaka wa Fedha 2025/26.
Bi. Raphael amezihimiza taasisi kuendelea kuzingatia matakwa ya kisheria na kuhakikisha kodi zinalipwa kwa wakati ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Hafla hiyo imewakutanisha Wakurugenzi wa Fedha, Wahasibu Wakuu pamoja na watumishi kutoka Idara za Fedha katika taasisi mbalimbali.



