Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Karatu
Wakulima wadogo katika Wilaya ya Karatu wamepokea ukombozi mpya wa kiuchumi kufuatia utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya Umwagiliaji unaofadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), mradi huu unalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa maji, hasa katika Kata ya Baray ambayo ni kitovu cha uzalishaji wa zao la kitunguu kinachousambazwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha furaha na matumaini mapya imetanda miongoni mwa wakulima wa Kanda ya Datoga baada ya kukamilika kwa uchimbaji wa visima viwili vitakavyohudumia hekta 66.5 za kilimo.
Mkulima Gilbert Makirija, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dk. Lameck Karanga, alieleza jinsi walivyokuwa wakisota kwa kusubiri maji ya umwagiliaji kwa siku 11 hadi wiki tatu. Kwa sasa, uwepo wa visima hivyo pamoja na miundombinu ya usambazaji hadi shambani na matanki ya kuhifadhia maji unawahakikishia uzalishaji endelevu na kuinua kipato cha familia zao.
Afisa Kilimo wa Kata ya Baray, Bw. Jaffet Petro, alibainisha kuwa ukosefu wa maji ulikuwa kikwazo kikubwa kwani kati ya hekta zaidi ya 5,600 zinazofaa kwa kilimo, ni hekta 3,000 pekee zilizokuwa zikitumika huku zaidi ya hekta 2,600 zikibaki hohehahe. Hali hii sasa inakwenda kubadilika kwani maji ya uhakika yatayawezesha maeneo hayo yaliyotelekezwa kuanza kuzalisha, jambo litakaloongeza tija ya mazao na kuimarisha uchumi wa kata hiyo na mkoa kwa ujumla.
Akiangazia kasi ya utekelezaji, Dk. Lameck Karanga alieleza kuwa ndani ya wiki mbili tu tangu Ziara ya Waziri wa Kilimo alipopokea kero ya wananchi, tayari visima 11 vimeshachimbwa kati ya 30 vilivyopangwa kwa wilaya nzima katika vijiji vya Dumbechand, Jobaj, Mbuga Nyekundu na Laghangareri.
Akimshukuru Rais Samia kwa upendo na uwekezaji huo wa kimkakati, Mkuu wa Wilaya aliwasihi wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili ilete tija endelevu kwa kila mwananchi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Arusha, Mhandisi Willium, mradi huu wa visima 30 unahusisha kata za Baray, Chemchem, Mang’ola, Endamaghan, Daa na Rhotia, ukiwa na visima vyenye kina cha mita 80 hadi 110 na uwezo wa kutoa lita 30,000 hadi 45,000 za maji kwa saa. Mpango huo unahusisha upimaji, usanifu, uwekaji wa pampu, matanki ya lita 10,000 na mifumo ya usambazaji, huku pia ukitoa fursa za ajira za kudumu kwa vijana sita wenye utaalamu wa ufundi bomba katika kila eneo la mradi.









