Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia watu 25 kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu na kuwajeruhi wengine wawili katika matukio yanayodaiwa kuchochewa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP), Marco Chilya, baada ya kufika katika maeneo yaliyoathiriwa na kujionea uharibifu wa mali uliotokana na vurugu hizo, ikiwemo kuchomwa kwa ofisi za Serikali na kuharibiwa kwa gari la Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Chilya, kati ya watuhumiwa 25 waliokamatwa, wanane wanahusishwa na matukio ya mauaji huku 17 wakihusishwa na vurugu, ambapo wafugaji ni 10 na wakulima 15 na kwamba operesheni na upelelezi vinaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wengine.
Kamanda Chilya alisema kuwa mfululizo wa matukio hayo ulianza Septemba 17, 2026, katika Kijiji cha Mrusha, Tarafa ya Lukumbule, baada ya mfugaji Shimbi Upole Shimbi, miaka 45, kutoa taarifa kuwa ng’ombe wake 180 waliporwa na kundi la wananchi wanaodaiwa kuwa wakulima na kuondoka nao kuelekea Kijiji cha Chikomo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa mfugaji huyo akiwa na ndugu zake walianza kuwatafuta ng’ombe hao na kufanikiwa kuwapata 179 katika pori la Kijiji cha Chinunje, Kata ya Mbesa, Tarafa ya Nalasi, huku ng’ombe mmoja pamoja na mchungaji Msanja Shimbi Upule wakiwa hawajaonekana.
Alieleza zaidi kuwa Septemba 18, 2026, wafugaji walimtafuta mchungaji huyo na kumkuta ameuawa, mwili wake ukiwa umezamishwa kwenye matope katika Mto Chermambo, Kijiji cha Chinunje na baada ya tukio hilo, wafugaji walivamia Vijiji vya Chikomo na Chinunje, ambapo Mohamed Kasim Chabwela( 58), aliuawa na watu wawili, Yusuph Yasin Bakili( 42) na Rashid Ally Ahmad,( 49) kujeruhiwa.
Chilya alisema Septemba 21, 2026, hali ilizidi kuwa tete baada ya wanakijiji wa Mbesa kupata taarifa kuwa mkulima mwenzao aliyekuwa akiishi mashambani ameuawa na kitu chenye ncha kali,ndipo Kikao cha wanakijiji kiliitishwa kujadili tukio hilo kilivunjika bila mwafaka na baadaye kuzuka vurugu zilizoshuhudia kuchomwa kwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mbesa, Ofisi ya Kijiji cha Airport Mbesa na nyumba ya Serikali aliyokuwa akiishi Afisa Kilimo na Mifugo.
Katika vurugu hizo, mali nyingine za Serikali ziliharibiwa, ikiwemo jembe la trekta, huku gari la Polisi likivunjwa kioo.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, kupora au kuchinja mifugo na kuingiza mifugo katika mashamba na kuharibu mazao, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika na matukio hayo.








