Na Cletus Sanga, WAF – Arusha

WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya waziri Mkuu – TAMISEMI na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaofadhiliwa na serikali ya Marekani imeendelea kuimarisha mwitikio dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa kuendesha zoezi la kuigiza hali halisi ya mlipuko, likilenga kupima uwezo wa wataalamu wa afya na mifumo ya uratibu katika kutoa mwitikio wa haraka, salama na wenye ufanisi endapo kutatokea tishio la ugonjwa huo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo juzi, Mratibu wa zoezi na Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Bi. Theresia Haule, amesema mazoezi ya aina hiyo ni muhimu katika kupima uwezo wa wataalamu wa afya kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika mazingira yanayofanana na hali halisi ya mlipuko wa Ebola.

Haule alisema zoezi hilo linasaidia kubaini maeneo yenye mafanikio na yale yanayohitaji kuimarishwa ili kuhakikisha mifumo ya utoaji huduma inakuwa tayari kutoa mwitikio wa haraka na wenye ufanisi wakati wowote panapotokea dharura ya afya ya umma.

Ameongeza kuwa kupitia zoezi hilo, wataalamu wa afya wameendelea kuimarisha uelewa wa taratibu za kukabiliana na Ebola, ikiwemo utambuzi wa wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo, utoaji wa taarifa kwa wakati, udhibiti wa maambukizi, matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi pamoja na uratibu wa huduma kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani kutoka CIHEB Tanzania, Dkt. Edgar Lusayo, aliesema mazoezi ya kuigiza hali halisi ya mlipuko wa Ebola ni sehemu muhimu ya kuendelea kujenga uwezo wa wataalamu wa afya na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo katika kujiandaa kukabiliana na dharura za afya ya umma.

Dkt. Lusayo aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo ya utayari na mwitikio wa magonjwa ya mlipuko kwa kutoa msaada wa kiufundi, mafunzo na uwezeshaji wa mazoezi ya vitendo, hatua itakayochangia kulinda afya za wananchi na kuimarisha usalama wa afya nchini.