Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Same
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same, imetoa mrejesho wa matokeo ya Uchunguzi wa Chanzo cha nyufa za ardhini na uharibifu wa baadhi ya majengo katika Kijiji cha Marieni, Kata ya Chome, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kufuatia uchunguzi uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na majanga, hususan wakati huu kuelekea kuanza kwa msimu wa mvua hususan mvua za El Nino.
Akiongoza kikao hicho Kijijini Marieni, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Rukia Zuberi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, amesema taarifa iliyowasilishwa na wataalamu kutoka GST imekuja kwa wakati muafaka, kwani itasaidia kuchukua hatua za mapema dhidi ya majanga asili ya jiolojia ambayo tayari yameanza kujitokeza katika Kijiji cha Marieni.
Amesema Taarifa hiyo, iliyowasilishwa na Wataalamu wa GST wakiongozwa na Bw. Gabriel Mbogoni (Mjiolojia Mwandamizi) kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST, imeeleza kwa kina maeneo yaliyoathirika kutokana na mabadiliko ya kijiolojia, huku ikibainisha baadhi ya kaya zilizoathirika pamoja na maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na madhara.
Mhe. Rukia Zuberi, amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyoathirika, pamoja na yale yaliyoainishwa kwenye taarifa hiyo kuwa ni hatarishi, kuyahama maeneo hayo mara moja na kutafuta makazi katika maeneo salama.
Amesisitiza kuwa hatua hii ni muhimu, ili kujikinga na hatari zaidi, ikiwemo kuangukiwa na nyumba ambazo baadhi yake tayari zimeonesha nyufa katika kuta, huku nyingine kuta zikiwa zimepishana kutokana na kujongea kwa tabaka la ardhi kuelekea bondeni.
Aidha, ameiagiza timu ya watendaji wa kata na wilaya kuanza mara moja mchakato wa kutafuta maeneo salama kwa ajili ya wananchi ambao makazi yao yameainishwa kuwepo katika eneo lenye hatari ya kukumbwa na madhara.
Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi katika kata nyingine kuchukua hatua za tahadhari katika maeneo yao, badala ya kusubiri hadi madhara yatokee.
Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST, Bw. Gabriel Mbogoni, amesema eneo la Marieni, liko katika Bonde la Ufa la Pangani ambalo ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.
Uchunguzi ulibaini kuwepo kwa tabaka kubwa la udongo wa mfinyanzi unaotokana na kumeng’enywa kikemikali (chemical weathering) kwa miamba ya msingi (basement rocks), kutokana na hali ya kitropiki ya eneo la Milima ya Chome.
“Hali ya hewa ya kitropiki ya eneo la Chome, pamoja na uwepo wa misimu yenye mvua kubwa au za muda mrefu, huongeza unyevu wa udongo na shinikizo la maji kwenye nafasi kati ya chembechembe za udongo. Hali hii hupunguza nguvu ya ukinzani wa tabaka la udongo na hivyo kuchangia kupungua kwa uthabiti wa miteremko” Alisema Bw. Mbogoni.
Ameongeza kuwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kinachofanyika kwa muda mrefu, ukataji wa miti pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu zinachangia kuongeza kiasi cha maji ardhini, na kufanya udongo kuwa na unyevunyevu mwingi na kuchochea kasi ya mabadiliko ya kijiolojia kwenye eneo hilo.
Bw. Mbogoni amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi huo, eneo la Marieni kwa sasa si salama kwa makazi na shughuli nyingine za binadamu, kutokana na uwezekano wa kutokea kwa maporomoko ya ardhi ambayo ni vigumu kutabiri kwamba yatatokea lini.
Sambamba na tukio hilo, Wataalamu wa GST walitoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari dhidi ya El Niño, walieleza namna El Nino inavyoweza kuhusiana na mwenendo wa mvua, pamoja na hatua muhimu za kuchukua kabla, wakati na baada ya mvua ili kupunguza athari za majanga yanayoweza kujitokeza. Wamewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na maelekezo kutoka mamlaka husika na kuchukua tahadhari mapema ili kulinda maisha na mali.








