Mwandishi wetu,Dodoma

Mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu nchini(THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni(MAIPAC) wamewataka wanahabari nchini, kuandika habari za mazingira zitakaleta matokeo chanya katika jamii.

THRDC na MAIPAC, wametoa wito huo,katika ufunguzi wa Mafunzo hayo yanafanywa chini ya mradi unaodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO,) katika mradi wa “Kuwawezesha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania kuwa na Athari Endelevu,” ambao unalenga kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari za mazingira kuchangia uwajibikaji wa mazingira, uelewa wa umma, ulinzi wa haki za binadamu na utawala endelevu wa mazingira kwa kuwahusisha waandishi wa mikoa ya Dodoma,Singida,Mbeya,Morogoro na Iringa.

Akifungua Mafunzo hayo,Mratibu wa kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa leo,Septemba 22,2026,jijini Dodoma amesema kuna changamoto nyingi za Mazingira nchini ambazo haziandikwi na kuleta matokeo.

Wakili Ole Ngurumwa anasema,tatizo la kusambaa taka mitaani,Uharibifu wa misitu na Vyanzo vya maji pamoja na uwekezaji usiozingatia athari za mazingira ni changamoto kubwa kwa sasa nchini.

“Rais Samia alisema Dar es Saalam ni chafu mimi nasema inanuka kwani uchafu umesambaa kila kona”anasrma.

Mkurugenzi wa MAIPAC,Mussa Juma anasema Dunia kwa sasa ipo katika kipindi kigumu kutokana na uharibifu wa mazingira na wanahabari wana wajibu kusaidia kutumia vyombo vyao vya habari.

Juma anasema, kwa sasa Tanzania kuna tushio kubwa la Mvua za El-Nino,lakini pia kuna maeneo ukame umeathiri maisha ya watu na mifugo lakini ni habari chache zenye tija zinazoandikwa.

“Kupitia mradi huu nendeni mkaandike habari za uchunguzi ,kubainisha changamoto za mazingira na mueleze suluhisho na ubunifu ili kusaidia jamii”amesema

Amesema Dunia inakabiliwa pia na changamoto.za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamepunguza upatikanaji wa chakula,yameleta mafuriko maeneo mengi na pia kuibua migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.

Mkuu wa Kitengo cha Utetezi,THRDC Wakili Paul Kisabo akitoa mada katika mafunzo hayo,aliwaelimisha wanahabari sheria mbali mbali za ndani na kimataifa ambazo zinatumika katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

Wakili Kisabo aliwataka wanahabari kuandika na kuchunguza habari za mazingira bila hofu ili kusaidia jamii na kama wakikabiliwa na changamoto watapata utetezi.

Mafunzo hayo yanashirikisha wanahabari 35 ambapo awali wanahabari 35 wa mikoa ya kanda ya kaskazini walipata mafunzo na wengine 35 wa Kanda ya Ziwa walipata mafunzo hayo kupitia mradi huo wa THRDC na MAIPAC unaodhaminiwa na UNESCO.