Na Mwandishi Wetu

HOSPITALI ya Shifaa imeanzisha madarasa kwaajili ya kutoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora na mtindo wa maisha ikiwa ni jitihada za kukabiliana na changamoto ya kisukari ambacho kimekuwa chanzo cha magonjwa mengi sugu.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Daktari bingwa mbobezi wa homoni na tezi wa Hospitali ya Shifaa ya Kinondoni, Dk Singla Mosha, wakati akizungumzia magonjwa sugu

Alisema miongoni mwa maradhi wanayotibu ni kisukari na kwamba kitu cha muhimu ambacho wamekuwa wakitilia mkazo ni kutambua kuwa shida ya ugonjwa wa kisukari ndiyo msingi wa matatizo mengi ya kiafya.

Alisema Katika matibabu ya sukari na magonjwa mengine sugu, eneo ambalo halijapewa nafasi yake ipasavyo na msisitizo wa kutosha ni suala la lishe na mtindo wa maisha.

Alisema Shifaa imejikita sana katika kuonesha umuhimu wa lishe na mtindo wa maisha katika kukabiliana na changamoto hiyo ya kisukari ambacho ndicho chanzo cha matatizo mengi ya maradhi sugu kwenye jamii.

Alitoa mfano kuwa sukari ndiyo imekuwa changamoto ya mafuta kwenye ini, maradhi ya kushindwa kupata ujauzito, uzito uliopitiliza, kiharusi, maradhi ya moyo, maradhi ya figo na mengineyo.

“Maradhi hayo yote niliyotaja ukiangalia kwa sehemu kubwa kabisa chanzo chake ni maradhi ya kisukari ambayo chanzo chake hasa ni shida ya lishe isiyo sahihi na mtindo mbovu wa maisha,” alisema na kuongeza

“Ukiaangalia muda ambao mgonjwa anakutana na daktari hautoshi kufahamishwa kuhusu mtiririko wa mtindo wake wa maisha na lishe kwa hiyo Shifaa imeanzisha madarasa ambayo tunafanya kama sehemu kamili ya kuonana na daktari ambapo watakaa kwa muda mrefu kuzungumza,” alisema

Alisema Shifaa imeanzisha madarasa hayo kwaajili ya kuwaelimisha wagonjwa ambao inawahudumia kwenye maeneo ambayo hayajapewa msisitizo wa kutosha ambayo ni lishe na mtindo wa maisha.

Alisema kwa kipindi ambacho wameshafanya madarasa hayo wameshaona matokeo makubwa sana kwenye matokeo ya wagonjwa waliokuwa wakiwahudumia.

Dk Mosha alisema elimu ya afya kwenye mitandao ya kijamii imekuwa ikiwachanganya watu kwani wengi wanaofanya hivyo hawana utaalamu wa kutosha wa masuala ya afya, wala namna ya kuthibitsha ufanisi na usalama wa ushauri wao, kwani wanafanya hivyo kama biashara.

“Uzuri ni kwamba hapa Shifaa ukija unaonana na daktari mtaalamu wa eneo hilo, tuna maabara yenye ubora wa hali ya juu kabisa, ambayo utapimwa kuthibitisha kuwa mafunzo tunayokupa yanakusaidia au la… Siyo kupewa ushauri tu ukishakutana na daktari unapimwa kuona mabadiliko ya afya yako,” alisema

“Tumekuwa tukiwahudumia wagonjwa wa kisukari aina ya pili, sisi tunasuluhisho la kumpungizia mgonjwa mzigo wa dawa anazolazimika kutumia kwa siku, tumekuwa na wagonjwa waliopimwa na kuonekana wana kisukari aina ya pili lakini tumewaondoa kwenye matumizi ya dawa,” alisema