📌Yapongeza Maendeleo ya Umeme Vijijini
Viongozi wa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) kutoka nchini Zambia leo Juni 29, 2026 wamehitimisha ziara yao ya Siku 9 ya kujifunza na kubadilishana ujuzi nchini kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo miradi ya kufikisha umeme Vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Akizungumza leo Juni 29, 2026 wakati wa kikao majumuisho kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za REA zilizopo Upanga Jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa REA Zambia, Mhandisi Suzyo Silavwe ameshukuru Uongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuratibu vyema ziara yao pamoja na kuwapatia nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Mhandisi Silavwe pia ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga ya kufikisha umeme vijijini.
“Tumekuwa na wakati mzuri na tumeweza kufanya vikao vilivyolenga kubadilishana ujuzi na uzoefu. Tumejifunza mengi lakini pia tulipata nafasi ya kutembelea miradi inayotekelezwa na REA Tanzania ambapo tumeona maendeleo makubwa,” amesema Mhandisi Silavwe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Wilson Nyamanga pamoja na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu wamesema kuwa ujio wa ugeni huo kutoka REA Zambia ni ishara ya kutambuliwa kwa mafanikio yaliyofikiwa nchini katika kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi vijijini.












