Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media
Dar es salaam
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imetunukiwa tuzo ya Huduma Bora kwa Wateja katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), ikiwa ni kutambua mchango wake wa kutoa huduma za afya zenye ubora na elimu kwa wananchi waliotembelea banda lake.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa JKCI, Dkt. Thabiti Kombo Ramadhan, alisema taasisi hiyo ilitoa huduma kwa wananchi zaidi ya 1,200 waliofika katika banda lao, ambapo 510 walifika kwa ajili ya kujua namba zao za afya kupitia vipimo mbalimbali.
Amebainisha kuwa matokeo ya uchunguzi huo yalibaini kuwa zaidi ya asilimia 47 ya waliopimwa walikuwa na shinikizo la damu na kisukari bila wao kufahamu, huku asilimia 58 ya waliotembelea banda hilo wakipata ushauri na huduma kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
“Katika maonesho haya sisi kama taasisi tulikuja kuwaonyesha wananchi huduma za kibobezi za matibabu ya moyo. Tulijikita katika kuelezea huduma na tiba zinazotolewa katika matawi yetu yote sita nchini,” alisema Dkt. Ramadhan.
Dkt Ramadhani JKCI ilikuja na kampeni kuu mbili, ikiwemo kampeni ya “Jua Namba Zako”, iliyowezesha wananchi kupima afya zao kwa kuangalia shinikizo la damu, sukari, mafuta mwilini, afya ya moyo pamoja na uwiano wa uzito na urefu ili kubaini hatari za magonjwa yasiyoambukiza mapema.
Aidha, alisema taasisi hiyo pia iliendesha kampeni ya kuchaja pamoja na kupima homa ya ini, ambapo zaidi ya wananchi 50 walijitokeza kupata huduma hizo wakati wa maonesho.
Dkt. Ramadhan amesema uwepo wa banda la JKCI katika Maonesho ya 50 ya Sabasaba umechangia kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi wanapougua ndipo waende hospitalini.
Aliongeza kuwa elimu iliyotolewa kupitia banda hilo imeongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kinga, utambuzi wa mapema wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza, hatua ambayo inaweza kusaidia kuokoa maisha ya wengi.


