Miongoni mwa habari zilizopewa umuhimu wa juu katika matoleo yaliyopita ya Gazeti la JAMHURI, zilihusu zabuni za mabilioni ya shilingi kwenye Awamu ya Tatu ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini.
Mradi huo ulio chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) una thamani inayokaribia Sh trilioni moja. Asilimia zaidi ya 95 ya fedha hizo zinatokana na kodi ya Watanzania wenyewe.
Awamu ya Tatu ya Mradi huu inalenga kufikisha umeme wa gridi katika vijiji 3,559 vilivyo kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara.

 

Pamoja na nia nzuri ya Serikali katika kuhakikisha miji na vijiji vyote nchini vinapata huduma ya umeme, kumebainika kuwapo kwa viashiria vya ukosefu wa uadilifu kwa baadhi ya watumishi wa REA na kampuni zilizoomba zabuni.
Kuna kampuni zilizoghushi nyaraka ili ziwe na sifa za kuziwezesha kushinda zabuni; kuna mgongano wa maslahi kwa baadhi ya wakurugenzi, maofisa na watumishi wa REA; na pia kuna mashinikizo kutoka kwa watu wenye ukwasi wakiwamo wanasiasa.

Tumefuatilia suala la REA kwa kuamini kuwa fedha zinazotumika kwenye kazi hiyo ni fedha za Watanzania wenyewe, kwa hiyo ni vizuri kampuni zinazopewa dhima hiyo ziwe na sifa za uadilifu na utendaji kazi mzuri.

 

Tunaunga mkono nia njema ya REA, Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwawezesha Watanzania kutekeleza miradi hii.
Pamoja na nia hiyo nzuri yenye kulenga kuwakomboa Watanzania kiuchumi, bado tunaamini REA hawapaswi kutoa zabuni kwa kigezo tu cha Utanzania. Tunazo taarifa zisizotiliwa shaka kuwa baadhi ya kampuni zilizovurunda kwenye Awamu ya Kwanza na ya Pili, zimeendelea kupewa kazi kwenye Awamu hii ya Tatu. Hili suala sharti lifuatiliwe na mamlaka zinazohusika. Uzalendo haumaanishi kuwapa kazi wazalendo wasiokuwa na sifa au uwezo.

 

Pili, mianya ya rushwa bado ipo kwenye utoaji zabuni. Mathalani, kitendo cha kampuni kupewa kazi kisha ndipo itakiwe kuwasilisha nyaraka REA kutoka CRB, ni mwanya mkubwa wa rushwa. Haiwezekani, kwa mfano, kampuni iliyohakikishiwa kazi ya Sh bilioni 50, ikashindwa kupata cheti kutoka CRB cha kuiwezesha kupewa zabuni hata kama haina sifa!

Tunaahidi kuendelea kufuatilia suala la REA na maeneo mengine, tukilenga kuisaidia Serikali katika kuhakikisha kuwa fedha za Watanzania zinaleta matunda yaliyokusudiwa. Mwisho, wale walioghushi hawapaswi kuachwa hivi hivi. Sharti washitakiwe kwa mujibu wa sheria.

By Jamhuri