Wizara ya Elimu ijitathmini suala la vitabu vya kiada na ziada

Wakati Serikali ikiendelea kutekeleza mpango wa elimu bure kuanzia awali mpaka kidato cha nne, mradi ambao unaigharimu serikali takribani Sh bilioni 19 kila mwezi, imebainika vitabu vya kiada na ziada zinavyosambazwa na serikali vimejaa makosa.

 

Tayari wizara hiyo imeshasambaza zaidi ya vitabu milioni 15.79 nchi nzima, vitabu hivyo ni kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi hapa nchini.

 

Vitabu hivyo vimechapishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania, taasisi ambayo iko chini ya wizara ya elimu. Makosa ambayo wabunge wameyapigia kelele wakati wa kupitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, yanamkera yeyote anayewatakia mema watoto wetu.

 

Ni wakati sasa serikali kuvirudisha vitabu vyote vya kiada na ziada ili vipitiwe upya, huku wahusika waliopitisha na kuruhusu kuchapishwa kwa vitabu hasa vile vya lugha ya kiingereza ambavyo ndivyo vimepigiwa kelele sana na wabunge, wachukuliwe hatua.

Athari za vitabu hivyo vilivyojaa makosa, ziko dhahiri kwa wanafunzi. Mfano kitabu cha Kiingereza cha darasa la tatu, kinaeleza Dodoma ni ‘mji mkubwa wa Tanzania’ badala ya Makao Makuu ya nchi.

 

Serikali isikae kimya, vyombo vya ulinzi na usalama viwachunguze wahusika na baada ya hapo hatua zichukuliwe. Maana hapo taifa limepoteza rasilimali fedha kwa kuchapisha vitabu hivyo, huku ikionesha dhahiri maudhui yake hayakuhaririwa vizuri.

Kibaya zaidi ni kwamba, vitabu hivyo vya kiada na ziada ambavyo vimekuwa vikitumika kwenye shule za umma, vimekuwa vinatoa elimu potofu kwa watoto wetu. Huo ni usaliti mkubwa katika mfumo wa elimu yetu ambao mamlaka zimekuwa zinajitahidi kuurudisha katika msitari.

 

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ameliambia Bunge kwamba atafanya mabadiliko makubwa ndani ya Taasisi ya Elimu Tanzania, sisi tunasema mabadiliko pekee hayatoshi, wahusika wanatakiwa kuwajibika na kuwajibishwa kwa uzembe walioufanya.

1786 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons