Taasisi ya iliyowasilisha serikalini ankara (invoice) iliyoongezewa dola milioni 49, sawa na Sh bilioni 114 ni Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania (TGFA), JAMHURI linathibitisha.

Habari zisizotiliwa shaka kutoka vyanzo vya uhakika, zimesema TGFA ambao wana jukumu la kununua ndege zote zinazoendeshwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kwa sasa wanapumulia mashine baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukizwa na ongezeko la fedha hizo ambazo alihoji mkataba ulikuwa unasemaje.

Hayo yalibainika baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia hivi karibuni, akionyesha kuwapo ongezeko la gharama ya kununua ndege wakati wa kulipia mkupuo wa mwisho kwa ndege ya mizigo aina ya Boeing 767 – 300 iliyopaswa kulipiwa dola milioni 37 sawa na Sh bilioni 86.2, ila ikaongezewa Sh bilioni 114 na kuonyesha zinahitajika kulipwa Sh bilioni 200.2.

Rais Samia alikerwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko hili, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya uongozi wake aliamua kutumia “lugha ngumu” hadharani. Alisema suala hilo halikubaliki na wanaohusika wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuachia nafasi zao. Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, amesema tayari wahusika wanachunguzwa kubaini ukweli.

“Kwa kweli tulipata mshituko mkubwa. Hatukuamini macho na masikio yetu, kusikia mtu anaweza kuongeza bei kwa dola milioni 49. Tunafahamu wapigaji wapo, walau mtu angepiga dola 500,000, ila milioni 49 inatisha. Tunaomba vyombo vya dola vichukue hatua kali kwa wahusika na iwe fundisho kwa wenginge wenye tabia kama hizo,” alisema mmoja wa maafisa wa Serikali aliyeomba asitajwe jina gazetini.

Hata hivyo, Afisa mwingine alisema haamini iwapo shirika kubwa kama Boeing linaweza kufanya mchezo mchafu wa aina hii: “Kama hiyo invoice (Ankara) si sahihi, basi watakuwa wamechakachua invoice iliyotoka kule Boeing, wakaiongeza cha juu. Hapo ni serikali kuwauliza Boeing wenyewe wao wanadai kiasi gani. Lakini pia, ununuzi wa ndege una kanuni zake. Unaweza kukuta bei hii ni sahihi kwani kama kuna vitu hawakuviniingiza kwenye mkataba, Boeing wenyewe saa ya mwisho ndege ikikamilika wanavingiza, hivyo vinaongeza gharama. Ila nasema, tujiridhishe,” amesema mwingine.

Katika ripoti ya CAG, amesema kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuna ndege zisizotumika zilizosababisha gharama Sh bilioni 5.27 na ukosefu wa mapato yaliyotarajiwa ya Sh bilioni 20.35. “Nilibaini ndege mbili za Airbus A220-300 (5H-TCH & 5H-TCI) na Bombardier Q400 zilikuwa hazifanyi kazi kwa muda wa siku 2 mpaka 220 kuanzia tarehe 1 Julai 2021 hadi 30 Juni 2022 kwa sababu ya utendaji duni wa ndege ya Airbus A220-300 na huduma dhaifu za baada ya mauzo za kuhakikisha ndege inafanya kazi kama vile huduma za kwenye injini.

“Uchambuzi wa kifedha umeonesha kuwa ndege zisizotumika zimesababisha kampuni kuingia gharama zisizobadilika kutokana na kukodi na bima jumla ya shilingi bilioni 5.27 na kukosa mapato ya shilingi bilioni 20.35 ambayo yangepatikana endapo ndege ingefanya kazi kwa mwaka mmoja tangu 1 Julai 2021 hadi 30 Juni 2022. Hali hii imeathiri sana ukwasi na sifa ya kampuni, pia kuongezeka kwa idadi ya ratiba za safari za ndege zilizofutwa kunaathiri uaminifu wa wateja juu ya usafiri wa Kampuni ya Ndege Tanzania.

“Ninapendekeza Serikali iiongezee uwezo kwa kuangalia upya shughuli za sasa za Kampuni ya Ndege Tanzania na kufanya matengenezo na ukarabati wa ndege mara kwa mara ili kuepuka ndege kukaa muda mrefu bila kufanya kazi,” anasema CAG Charles Kichere.

Katika ripoti hiyo, Kichere anasema kuna matumizi yasiyoridhisha ya ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner yaliyosababisha hasara ya shilingi bilioni 24.9 na gharama za kudumu za matengenezo shilingi bilioni 5.06. Kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya ndege, matumizi yasiyoidhinishwa ya ndege ni ndege hizi kuwashwa na kuzimwa katika umbali mfupi. Mfano Dreamliner ikitoka Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro inakuwa ni hasara kubwa kwani yenyewe inatakiwe iruke umbali unaoiwezesha kukaa hewani kwa saa angalau nane hadi 10 bila injini kuzima, badala ya dakika 40 za kutoka Dar es Salaam, kwenda Kilimanjaro.

“Wakati wa mapitio yangu ya utendaji kazi na matumizi ya ndege, nilibaini ndege ya Boeing 787-8 ilizalisha mapato ya jumla ya shilingi bilioni 45.67 na kuwa na gharama ya shilingi bilioni 70.57 ambayo ilisababisha hasara ya jumla ya shilingi bilioni 24.9. Kukosekana kwa ufanisi wa uendeshaji kulisababishwa na idadi ndogo ya abiria na idadi ndogo ya safari za kimataifa, kwani ni safari 9 kati ya 18 za kimataifa zilifanyika kutokana na kusimamishwa kwa baadhi ya safari kwa sababu ya vikwazo vya udhibiti wa ugonjwa wa UVIKO-19.

“Zaidi, ukaguzi ulibaini ndege hizo zilisababisha gharama zisizobadilika za shilingi bilioni 5.06 kama gharama za matengenezo ambazo hazikuwa na mapato yanayolingana kutokana na kutofikia masaa ya ndege yanayoweza kutozwa kiwango cha chini. Hii inapelekea ongezeko la madeni ya kampuni ambayo yanaathiri uwezo wa kifedha wa kampuni. Ninapendekeza Kampuni ya Ndege Tanzania kufanya kampeni za kina za masoko ili kuukuza ufanisi wa safari za ndege za kitaifa na kimataifa ambazo hazifanyi vizuri,” amesema.

Ripoti ya CAG inazungumzia dondandugu ambalo ni mkataba wa kukodisha ndege kwa ATCL kutoka kwa TGFA. Karibu asilimia 95 ya hasara inayopata ATCL inatokana na mkataba huu. Mkataba huu ulioingiwa mwaka 2016, umekuwa dude abalo halina mwanzo wala mwisho. Kila Serikali ikinunua ndege mpya, inaiongeza kwenye mkataba huu unaozalisha hasara kwa ATCL.

“Kimsingi, mkataba huu ni mumiani… unainyonya damu ATCL. Shirika hili haliwezi kushindana na Ethiopia Airline au Kenya Airways. Wao kila fedha wanayoipata inaingia kwenye uendeshaji, lakini sisi Tanzania inanunua ndege, bado inakodisha ndege. Bunge liliishaliona hili, ila kwa masilahi ya watu wachache Serikalini, hata baada ya kuwapo mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu na TGFA wenyewe kuonyesha hatari iliyopo, bado hakuna mabadiliko yoyote. Bila mkataba huu kubadilishwa, sahau ATCL kukoma kupata hasara,” amesema mmoja wa wataalam wa masuala ya ndege.

Kwa mujibu wa CAG gharama za ziada za Sh bilioni 19.11 zimetumiwa na ATCL kutokana na Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania kutotekeleza majukumu ya kimkataba. “Ndani ya mwaka 2021/22 Kampuni ya Ndege Tanzania ilikodi ndege 11 kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali ya Tanzania, hivyo kutozwa gharama za matengenezo za dola za Marekani 496 kwa saa moja kwa utendaji kazi wa injini na dola za Marekani 360 kwa maisha ya injini ya mzunguko wa ndege, na kwa mwaka 2021/22 zilifikia shilingi bilioni 25.39 (2020/21 shilingi bilioni 18.56) kiasi hicho kinakusudiwa kwa matengenezo ya ndege wakati zinaharabika na ankara hiyo ilikuwa ni kwa mujibu wamasharti ya mkataba.

“Katika mapitio yangu ya gharama za uendeshaji, nilibaini kuwa, Kampuni ya Ndege Tanzania iliingia gharama ya shilingi bilioni 19.11 kwa ajili ya matengenezo ya ndege katika mwaka huo, ambayo ni sehemu ya akiba ya matengenezo chini ya mkataba wa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania. Katika kiasi hicho, shilingi bilioni 17.51 zilitumiwa kwa matengenezo ya ndani yaliyofanywa na Kampuni ya Ndege Tanzania kwa kutumia ujuzi na uwezo wa wataalamu wake, wakati shilingi bilioni 1.6 zilizobaki zilitumika kwa matengenezo ambayo hayakufanywa na Kampuni ya Ndege Tanzania, yalikuwa chini ya makubaliano ya programu ya usimamizi wa injini wa PW1524G.

“Hata hivyo, gharama zote mbili zilizolipwa na Kampuni ya Ndege Tanzania ni sehemu ya mkataba wa matengenezo yanayotakiwa kugharamiwa na Wakala wa Ndege za Serikali ya Tanzania. Ni maoni yangu kuwa gharama hizi zilizoingiwa mara mbili zimesababishia kuongezeka kwa hasara kwa Kampuni hii.

“Kwakuwa, ulipaji mara mbili wa gharama ambazo ni shilingi bilioni 19.11 kwa watoa huduma na shillingi bilioni 25.39 kwa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania, hasara iliyotokea mwaka huu ingeweza kupungua kutoka shilingi bilioni 35.24 mpaka shilingi bilioni 9.85 (ambayo tumetoa malipo kwa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania). Ninapendekeza Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iharakishe mchakato wa kupitia makubaliano kati ya Kampuni ya Ndege Tanzania na Wakala wa Ndege za Serikali ya Tanzania.

“Mapitio hayo yalenge kufafanua tatizo la malipo mara mbili kwa huduma za matengenezo, ambazo huongeza gharama na madeni kwa Kampuni ya Ndege Tanzania,” amesema CAG Kichere.

JAMHURI limepata taarifa kuwa tatizo hili la kuwapo hesabu mara mbili linatokana na mktaba ulioingiwa. Wakati ATCL wanafanya matengenezo ya ndege na kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku, vitabu vya TGFA ingawa hawafanyi matengenezo vinazidi kuonyesha kuwa ATCL inadaiwa fedha za matengenezo kwa mujibu wa mkataba.

JAMHURI linafahamu kuwa TGFA imekwishawaandikia Ikulu mara mbili kati yam waka 2021 na 2022 kueleza nia ya kufanya marekebisho ya mktaba na ikibidi basi ATCL watozwe dola 1 kwa kila ndege kwa mwaka, lakini zibaki kuwa mali ya TGFA kuendeleza dhana ya kulinda ndege hizo zisikamatwe kudokana na madeni ya zamani wanayodaiwa ATCL.

JAMHURI limeona moja ya barua hizo za mwaka 2002 kwenda Ikulu, ambayo inaomba kufutwa kwa deni la ATCL na kushauri mkataba urekebishwe inayosema: “Makubaliano hayo yanaitaka ATCL kuwa inalipia tozo za ukodishaji ndege na pia kutenga kiasi cha fedha na kukiwasilisha TGFA kwa ajili ya akiba ya matengenezo makubwa.

“Jumla ya kiasi cha fedha kinachoombewa kufutwa ni Dola za Kimalekani (USD) 7,392,671.35 [Sh bilioni 17.22] ambacho kiasi cha Dola za kimarekani 7,337,875,65 [Sh bilioni 17] kinahusika na deni la akiba ya matengenezo makubwa ya Ndege na kiasi kilichobaki cha dola za kimarekani 54,795.70 [milioni 127.6] kinahusika na deni la tozo la ukodishaji.

“Hadi kufikia Juni 2020 jumla ya kiasi cha tozo na fedha ya gharama za matengenezo makubwa kilichozalishwa kutokana na matakwa ya mikataba ni Dola za Kimarekani 27,990,000.00 [Sh bilioni 65.2] na 20,515,293.69 [Sh bilioni 47.8]. Kiasi halisi kilichokwishalipwa kwa upande wa tozo ni Dola za Kimarekani 12,555,000.00 [Sh bilioni 29.2] na fedha za gharama ya matengenzo ni Dola za Kimarekani 1,968,845.20 [Sh bilioni 4.58]. Deni ambalo bado halijalipwa kati ya fedha zinazodaiwa kwa upande wa tozo ni Dola za Kimarekani 15,435,000.00 [Sh bilioni 35.96] na kwa upande wa fedha za akiba ya matengenezo makubwa ni Dola za Kimarekani 18,546,448.49 [Sh bilioni 43.2].

“Kampuni ya ATCL imewasilisha kwetu maelezo na kutoa vielelezo juu ya kushindwa kulipa sehemu ya fedha za tozo, pia kutenga na kisha kuwasilisha sehemu ya fedha za akiba ya matengenezo makubwa kama Mikataba inavyoelekeza. Kwa upande wa fedha za matengenezo makubwa ATCL imeeleza kuwa ililazimika kugharamia yenyewe matengenezo hayo moja kwa moja na kwamba kwakuwa iligharamia kutengeneza ndege yenyewe, ile fedha iliyotarajiwa kuwasilishwa kwenye Wakala kama Mikataba inavyoelekeza inayofikia kiasi cha USD 7,392,671.70 [Sh bilioni 17.2] itolewe kwenye mahesabu na isihesabike kuwa ni deni.

“Wakala pia imepokea maombi ya kusimamisha tozo la ukodishaji wa Ndege zilizokodishwa kwa kampuni hiyo hususani “Boeing 787-8 Dreamliner pamoja na aina ya Airbus A220 tangu ziliposimamisha huduma zake baada ya kuibuka kwa janga la ugonjwa wa korona mwanzoni mwa mwaka 2020.

“Hivyo basi, sababu kuu ya kuwasilisha maombi haya ni kuomba kibali kutoka kwako kutokana na Wakala kutokua na uwezo wa kutekeleza swala hili moja kwa moja kwani katika mikataba iliyoingiwa awali, maeneo haya hayakuainishwa bayana. Vipengele vyote vyenye mapungufu ikijumuisha eneo hili, vimeainishwa katika rasimu ya marekebisho ya mikataba iliyosainiwa tarehe 29 Aprili, 2020 baina ya pande zote mbili ambapo imewasilishwa kwenye mamlaka za juu kwa maamuzi.

“Menejiment ya Kampuni ya Ndege Tanzania imeendelea kuomba na kushauri juu ya utekelezaji wa swala hili mapema wakati tukiendelea kusubiri maamuzi juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa kwani swala hili linaathari mbalimbali ikijumuisha mizania hasi ambayo hupelekea kushuka kwa taswira na hadhi ya kampuni kwenye Soko na sekta kwa ujumla,” inasema sehemu ya barua iliyoandikwa na TGFA kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Kwa mantiki hiyo, kwa vyovyote iwavyo, ATCL kama ikiendelea na mkataba na TGFA wenye “kuikausha damu” haitatokea ikapata faida kutokana na kwamba inadaiwa gharama isizoweza kuzirejesha, wakati imeishazitumia katika matengenezo na uendeshaji wa ndege.

November, 2021 Bunge kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipitisha Azimio la Bunge kuitaka TGFA na ATCL kuoanisha hesabu zao (harmonization) kwa ajili ya kuondoa hasara hewa inayoendelea kuitesa ATCL, lakini inatajwa baadhi ya maafisa katika ofisi kubwa hawajawa tayari kulifanya hivyo, ingawa zamu hii Rais Samia ameelekezwa limalizwe.

JAMHURI lilipowasiliana na Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, amesema: “Haya mambo yana mlolongo mrefu. Kamati ya Bunge imewahi kuyatolea kauli mara mbili na sasa tuyashughulikia, tutakutana tena na Kamati ya Bunge, lakini tuna Imani kubwa na Mhe. Rais Samia kuwa atalipatia ufumbuzi wa kudumu na tunamshukuru sana kwa jinsi alivyoisaidia ATCL,” amesema Matindi.

Shirika la Umeme Tanzania

CAG katika taarifa yake anasema Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) limekuwa na utaratibu wa kuvumia vifaa ambazo havijaidhinishwa na wakala wa vipimo. “Kati ya mita 1,803 za vituo vya umeme vilivyopo katika mikoa 29, taarifa za mita 1,638 (asilimia 90.8) hazikuoneshwa katika mfumo wa usomaji mita moja kwa moja kwa mwaka mzima.

“Na kuongezea mita 52 zilikuwa na usomaji wa nishati iliyopokelewa pekee, wakati mita 80 zilikuwa na usomaji wa nishati iliyosafirishwa pekee. Suala hili ni kinyume na Kanuni Na. 45(1) ya kanuni za sheria ya umeme (Huduma za Ugavi) za mwaka 2019.

“Pia, nilibaini ugumu wa kufuatilia usomaji wa mita kwa mitambo ya kulisha umeme na usambazaji wa umeme (ikiwa ni pamoja na watumiaji wakubwa wa nishati) kutokana na upungufu wa maelezo kuhusu mitambo ya kulisha umeme au vituo vidogo vya umeme katika mfumo wa usomaji mita moja kwa moja.

“Uongozi wa shirika ulielezea sababu kuu za udhaifu huu ni matatizo ya mtandao na mita zilizoharibika kwenye vituo vya umeme. Kwa maoni yangu, ufungaji wa mita katika mitambo ya umeme haukuakisi thamani ya fedha, na kuna uwezekano kuwa baadhi ya mita au mitambo ya umeme imefanyiwa udanganyifu au kughushiwa, hivyo kusababisha wizi wa nishati unaofanywa na wateja (hasa watumiaji wakubwa wa nishati) kwa kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu.

“Ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania lifanye tathmini ya mfumo wa usomaji mita moja kwa moja na mita za umeme zinazowekwa ziendane na mazingira ya sasa ya uendeshaji ili kuzuia upotevu wa nishati,” amesema.

Kati ya taarifa ya kushangaza, mita za umeme 874,019 hazikuthibitishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA). “Katika mwaka wa fedha 2021/22, Shirika la Umeme Tanzania lilinunua na kutumia jumla ya mita 874,019 zenye thamani ya shilingi bilioni 115. Lakini hazikuthibitishwa na Wakala wa Vipimo kitu ambacho kinaweza kusababisha hasara kwa mteja au Shirika.

“Hii ni kinyume na Kanuni ya 22(1) ya Kanuni za Uzani na Vipimo za mwaka 2019 zinazoelekeza kuwa hakuna mita itakayoruhusiwa kutumiwa na mkandarasi au mnunuzi kwa madhumuni ya kupima umeme au gesi inayotolewa au kutumika kwake isipokuwa imethibitishwa kwa mujibu wa Sheria za Umeme Na.10 ya 2008.

“Ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania litekeleze matakwa ya Kanuni za Uzani na Vipimo za Mwaka 2019, ili kuhakikisha mita zinapimwa na kuthibitishwa na Wakala wa Vipimo kabla ya kutumiwa na wateja,” amesema.

TANESCO pia inahusishwa na malipo ya kutunza vyura wa Kihansi katika bustani ya Wanyama ya Marekani kwa Sh milioni 612. “Mwaka 2000 Tanzania ilisafirisha vyura 500 kwenda bustani ya wanyama ya Bronx na Toledo iliyopo Marekani ili kuepuka hatari ya kupotea kwa vyura ambayo ilitokana na utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Kihansi mnamo mwaka 1994.

“Ingawa haiwezekani kubainisha idadi kamili ya sasa ya vyura vinavyosimamiwa nchini Marekani, Shirika la Umeme Tanzania linagharamia dola za Marekani 130,000 [Sh milioni 303] kwa mwaka kwa ajili ya kutunza vyura hao, ambapo inakadiriwa takribani ya dola za Marekani milioni 2.86 [Sh bilioni 6.66] zilitumika kwa miaka yote 22 ya kuhudumia vyura.

“Katika mwaka 2020/21 na 2021/22 ilifanya malipo ya shilingi milioni 611.92 (sawa na dola za Marekani 260,000). Nimebaini kuwa mkataba kati ya Tanzania na bustani za Wanyama za Marekani ulimalizika mnamo Juni, 2020 na kuongezewa muda wa miaka miwili hadi Juni, 2022. Japokuwa hakukuwa na mpango wowote wa kurudisha vyura hao Tanzania ikizingatiwa kuwa tayari miaka 22 imepita tangu vyura 500 wapelekwe kwenye bustani za wanyama za huko Marekani.

“Ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii iweke mpango mkakati wa kurudisha vyura wa Kihansi ili kuepuka gharama kwa Shirika la Umeme Tanzania,” amesema.

Pia, CAG amesema kumekuwapo na ongezeko la riba kwa kucheleweshwa malipo ya madai ya kampuni ya Pan Africa Energy Tanzania Sh bilioni 113.84: “Mkataba wa uuzaji wa gesi kati ya Shirika la Umeme Tanzania na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania ambao unatumia kwa uzalishaji wa umeme katika Ubungo I, Ubungo III na Tegeta uliotiwa saini tarehe 17 Juni 2011 na unatarajia kumalizika Juni 2023, unabainisha riba itaongezeka kwa kiwango cha asilimia 4 zaidi ya kiwango cha LIBOR kila mwaka iwapo Shirika la Umeme Tanzania halitalipa kiasi kinachodaiwa kwa Kampuni na Pan African Energy Tanzania.

“Katika ukaguzi wangu wa wadeni wa Shirika la Umeme Tanzania, nilibaini kuwapo kwa ankara za Kampuni ya Pan African Energy Tanzania ambazo hazijalipwa kwa miaka 10 (kuanzia 2012/13 hadi 2021/22) zenye thamani ya shilingi bilioni 246.74 ambayo inajumuisha riba ya malipo yaliyocheleweshwa ya shilingi bilioni 113.84. Hii imechangiwa na ukosefu wa fedha za kutosha kuwalipa watoa huduma, na kusababisha gharama kuongezeka kwa taasisi.

“Ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania, kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati litafute njia mbadala za ufadhili ili kuhakikisha malipo ya ankara za kila mwezi yanafanyika kwa wakati na kufanya mazungumzo na kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAET) ili isitishe tozo ya riba kwa malipo yanayofuata,” amesema.

CAG pia aligusia Kampuni ya IPTL kuchelewa kukamilisha malipo kwa Serikali baada ya Serikali kushinda kesi – dola za Marekani milioni 148.4 (Sh bilioni 345.77). “Mwaka 1995, Kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL) na Shirika la Umeme Tanzania walitia saini Mkataba wa Kununua Nishati ya Umeme kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umeme.

“Wakati wa usambazaji wa umeme, kulikuwa na mgogoro wa kiwango cha malipo ambao ulisababisha kufungua akaunti ya escrow mwaka 2006 kwa ajili ya kulinda malipo. Mwaka 2012 Shirika la Umeme Tanzania na Kampuni ya Independent Power Tanzania walimaliza mgogoro huo na kiwango cha fedha kutoka akaunti ya escrow zilipelekwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solutions Tanzania ambaye ni mmoja wa wanahisa wa kampuni ya Independent Power Tanzania.

“Kampuni ya Independent Power Tanzania ilikuwa na mkopo Benki ya Standard Chartered Hong Kong ambao kwa upande wao wanadai kuwa kampuni ya Pan African Power Solutions Tanzania walitumia baadhi ya fedha kutoka kwenye akaunti ya escrow kulipa hisa za kampuni ya VIP katika Kampuni ya Independent Power Tanzania, badala ya kutimiza wajibu wa malipo wa Shirika la Umeme Tanzania chini ya PAP na kulipa mkopo.

“Kwa sababu hiyo, mwaka 2016 Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji kiliamua kuwa Shirika la Umeme Tanzania lazima liilipe Benki ya Standard Chartered Hong Kong dola za Marekani milioni 148.4 [Sh bilioni 345.77] pamoja na riba. Kufuatia uamuzi huo, mnamo mwaka 2018 Serikali iliwasilisha kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya kampuni ya Independent Power Tanzania ili kutekeleza hati ya fidia iliyotiwa saini tarehe 27 Oktoba 2013 ambayo inalinda hatua ya Serikali kutoa fedha kwenye akaunti ya Escrow kutokana na madai ya wahusika wa nje.

“Uamuzi wa tarehe 1 Machi 2021 ulikuwa kwa upande wa Serikali na kampuni ya Independent Power Tanzania ilikubali kuilipa Serikali dola za Marekani milioni 148.4 [Sh bilioni 345.77] mnmo tarehe 01 Machi 2021, hata hivyo hadi wakati wa ukaguzi, mwezi Disemba 2022, IPTL hawakuwa wamelipa kiasi kinachodaiwa.

“Ni maoni yangu, ikiwa Serikali italipa madai ya Benki ya Standard Chartered Hong Kong kufuatia uamuzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro bila kupata kiasi hicho kutoka kwa kampuni ya IPTL, itakuwa imefanya malipo mara mbili kwa kuwa malipo ya umeme tayari yalifanywa kwenye akaunti ya escrow, na kampuni ya IPTL ilitoa ahadi kupitia hati ya kulinda madai ambayo iliiondolea Serikali madai yoyote ya Benki ya Standard Chartered Hong Kong.

“Nina mashaka kuwa kuchelewa kwa kampuni ya IPTL kulipa deni lake kunasababisha Serikali kuchelewa kupata fedha za kuilipa Benki ya Standard Chartered Hong Kong. Hali hii inapelekea kuongezeka kwa mkopo kwa sababu ya riba inayoongezeka hivyo kuchafua sifa ya nchi yetu katika jukwaa la kimataifa.

“Ninapendekeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania, ichukue hatua kuhakikisha kampuni ya Independent Power Tanzania inakamilisha malipo ili kuepuka ongezeko la riba ya mkopo.

Juhudi za kuupata uongozi wa TANESCO kuzungumzia hoja hizi, haukuzaa matunda baada ya wahusika kutopatikana hata baada ya kwenda ofisini kwao.

By Jamhuri