Wanafunzi zaidi 60 wa kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Vwawa day iliyopo katika mji wa Vwawa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamenusurika baada ya bweni lao kuteketea kwa moto asubuhi ya April, 14 wakiwa darasani na wengine kwenye mitihani ya kujipima Mock.

Kaimu Kamanda jeshi la Zima moto na uokoaji Mkoa wa Songwe Inspekta Elautery Mremi akiongea na Vyombo vya Habari kwenye tukio hilo amesema wamepata with wa tukio hilo la moto saa tatu asubuhi, ambapo walikuta moto umeunguza bweni zaidi ya asilimia 50.

Amesema wamechelewa kulifikishia taarifa Jeshi la Zima moto ,hali iliyopelekea kukuta vifaa vingi vya wanafunzi hasa, nguo , vitanda magodoro kuteketea kwa moto.

“Tumekuta bweni limeteketea kwa zaidi ya asilimia 50, tulichofanya ni kuokoa mabweni mengine na madarasa yasiteketee, pia tumefanikiwa kudhibiti moto huo kwa asilimia 99” amesema Inspekta Mremi.

Amesema katika tukio hilo hakuna kifo wala majeruhi yeyote na kudai kuwa uchunguzi unaendelea ili kugundua chanzo Cha moto huo, huku Tathmini ya Mali zilizoteketeaikiendelea kufanyiwa Tathmini.

Afisa elimu Mkoa wa Songwe Michael Ligola amesema Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi baada ya tukio hilo wameungana kuwasaidia wanafunzi walioathirika na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwanunulia magodoro na vifaa vya kujifunika.

Amesema wanaendelea kufanya Tathmini ya Mali zote zilizoteketea kwa moto , ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguza chanzo Cha tukio hilo la moto ambalo ni mara ya kwanza kutokea katika shule hiyo.

Aidha Ligola amewataka wanafunzi ambao mabweni yao yapo salama kutoa ushirikiano kwa wenzao ambao ni wahanga wa tukio hilo. Alisema kuwa wenzao wanahitaji misaada mbali mbali ya nguo, daftari za kusoma na vitabu wapewe ushirikiano wa kutosha.

Kwa upande wa mwanafunzi Gospel Andwale kidato Cha sita mhanga wa tukio hilo alisema walikuwa darasani wakapata taarifa ya ghafla kuwa bweni lao linaungua, walipojaribi kwenda kuokoa vifaa vyao walikuta tayari vimeungua.

“Tumebaki na nguo tulizokuwa tumevaa tukiwa darasani , kila kitu kimeungua madaftari, nguo, magodoro na vitabu .tunaomba viongozi wa shule, Wilaya na mkoa watusaidie Ili tuweze kupata baadhi ya mahitaji ambayo ni muhimu” amesema Gospel.

By Jamhuri