Na Mary Gwera,JamhuriMedia,Mwanza

Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Majaji nchini kuwa sehemu ya maboresho ya Mahakama yanayoendelea kufanyika ili kila mmoja afahamu kwa kina kinachoendelea kwa manufaa ya Mhimili huo na umma kwa ujumla.

Akizungumza jana na Majaji hao wakati akiahirisha Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 kilichofanyika kwenye Hoteli ya Malaika jijini Mwanza, Prof. Juma amesema kwamba, suala la maboresho ni endelevu hivyo ni muhimu kila mmoja kujihusisha nalo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizungumza na Majaji wa Mahakama ya Tanzania (hawapo katika picha) wakati akiahirisha kikao cha  Tathmini ya Utendaji wa Mahakama jana tarehe 14 Aprili, 2013 kwenye ukumbi wa mikutano wa Malaika jijini Mwanza. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija.

“Tunapozungumzia maboresho endelevu lazima kila mmoja wetu aelewe kinachoendelea sio kwa kuambiwa tu bali pia kwa kusoma, na kwa bahati nzuri nyaraka nyingi sana za maboresho zipo na maswali mengi sana ambayo yanaulizwa kuhusu maboresho zinapatikana kupitia tovuti na blogu ya Mahakama, hivyo tunapotekeleza shughuli zetu za uondoshaji wa mashauri ni vizuri pia kuyaelewa maboresho,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha,Prof. Juma alipongeza jitihada mbalimbali zilizofanyika zenye kuleta maboresho ndani ya Mahakama huku akitaja baadhi ya Ofisi ndani ya Mhimili huo zikiwemo Kitengo cha Maboresho, Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Idara ya TEHAMA, Kamati ya Jaji Mkuu ya Kanuni na nyingine.

Amesema kwamba Idara/Vitengo/Kamati hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuchagiza maboresho hususani katika usimamizi wa matumizi ya teknolojia, usimamizi wa mashauri, utungaji wa kanuni zaidi ya 75 zilizowezesha kurahisisha baadhi ya taratibu za Mahakama na mengine.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewataka Majaji kuzitumia vyema kanuni zilizotungwa kuangalia namna bora ya kuzitumia kanuni mbalimbali ili zisaidie kuleta maboresho katika huduma ya utoaji haki.

“Kamati ya Jaji Mkuu ya Kanuni ni moja ya Kamati ambayo imefanya vizuri sana katika safari ya maboresho, zaidi ya kanuni 75 zimetungwa hivyo ni muhimu kuendelea kutumia kanuni hizo kuboresha zaidi huduma za haki,” alisisitiza Mhe. Prof. Juma.

Katika kikao hicho cha siku tatu (3) mada mbalimbali zimetolewa ambazo ni pamoja na taarifa ya hali ya utoaji haki Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2022, TEHAMA, Maboresho ya huduma za Mahakama na nyingine, kadhalika Maafisa hao wa Mahakama wamekubaliana kufanya kazi kwa ushirikiano, kuendeleza matumizi ya TEHAMA, kuangalia namna ya kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri vyote vikilenga kuboresha huduma za upatikanaji haki kwa wananchi.

Baadhi ya picha mbalimbali za Majaji wa Mahakama ya Rufani (T) na Mahakama  Kuu ya Tanzania wakimsikilia Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha)  wakati akiahirisha kikao cha 
Tathmini ya Utendaji wa Mahakama jana tarehe 14 Aprili, 2013 kwenye ukumbi wa mikutano wa Malaika jijini Mwanza.

By Jamhuri