Wakazi wa Mtaa wa Kilongawima, Kata ya Kunduchi, wilayani Kinondoni, wameulalamikia uongozi wa kiwanda cha kuoka mikate cha Gulled Industry, kilichopo eneo hilo kutokana na kushindwa kudhibiti harufu mbaya inayotoka kiwandani humo.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wanasema kiwanda hicho kimegeuka kuwa kero kubwa mtaani hapo, baada ya kubadilisha shuguli za awali zilizokuwa zikifanyika hapo za kusuka mota badala yake kuanza kuoka mikate.

“Mwanzoni kiwanda hakikuwa na matatizo yoyote na wakazi wa eneo hili tatizo limekuja kujitokeza baada ya kubadilisha shughuli za awali na kuanza kuoka mikate.”

Wanasema pamoja na kuwa nchi inahitaji uwekezaji lakini uwekezaji usiofuata sheria zilizowekwa na mamlaka husika ni hatari kwa ustawi wa wananchi wa eneo husika na nchi kwa ujumla.

Wanasema wawekezaji hao kutoka nchini Kenya wamekuwa si waungwana, kwani wamekuwa ni ‘jeuri’ utadhani wapo juu ya sheria za nchi, hali inayotishia maisha yao huku mamlaka husika zikiwa kimya.

Wanasema harufu mbaya inayotoka ndani ya kiwanda hicho imekuwa ni tishio kwa maisha yao hasa watoto wadogo, kiasi cha wengine kuanza kupata matatizo mbalimbali ya kiafya kama kukohoa na kuwashwa miili yao.

“Watu hawa shughuli zao nyingi zinafanyika nyakati za usiku, nyakati hizi malori makubwa yamekuwa yakibadilishana kuingia humo ndani na haifahamiki huwa wanaingiza nini ndani humo,” wanasema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Poul Richard, anasema kiwanda hicho kimegeuka kuwa hatari kwa maisha ya wananchi wa eneo hilo kiasi cha wengine kuanza kupata matatizo ya kiafya kama kukohoa na miili yao kuwasha.

“Mwanzo kiwanda kilikuwa kikijihusisha na usukaji wa mota za aina mbalimbali, lakini mara tukaanza kusikia harufu kali ya mikate ikitoka ndani humo, hali ambayo ni hatari kwa wakazi wa eneo husika,” anasema Richard.

Anasema mara baada ya kuchaguliwa katika nafasi aliyonayo, alifanya jitihada za kutaka kukutana na uongozi wa kiwanda lakini hakufaulu baada ya kukumbana na vikwazo mbalimbali vya kukutana na uongozi.

“Kuna siku mimi pamoja na mmoja wa wazee wa hapa ofisini, tulienda katika kiwanda hicho kwa lengo la kutaka kuonana na uongozi lakini hatukuruhusiwa kuingia ndani pamoja na kujitambulisha,” anasema Richard.

Anasema uongozi wake umefanya kila linalowezekana kukabiliana na tatizo lakini juhudi zake zimekwamishwa na uongozi wa kiwanda ambao hauna ushirikiano na ofisi yake.

Anasema umefika wakati kwa mamlaka husika kuwa makini na kila mtu anayeingia nchini kwa lengo la kuja kuwekeza kwa kuhakikisha sheria zinafuatwa.

“Watu hawa inawezekana wakawa na vibali vyote vya mamlaka husika kuwaruhusu kufanya kazi wanayofanya, lakini je, walizipata kihalali? Hili bado ni kitendawili kwa sababu eneo hili si la viwanda,” anasema Richard.

Anasema sheria za uhifadhi wa mazingira zinasema kila mtu anayeishi Tanzania ana haki ya kuwa na mazingira safi na salama kwa manufaa yake na Taifa kwa ujumla.

“Usimamizi na utekelezaji wa sera na sheria husika unakabiliwa na changamoto mbalimbali, kama vile uwezo mdogo (rasilimali watu) na uhaba wa fedha kwa ajili ya utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya rasilimali za mazingira katika ngazi zote,” anasema Richard.

Anasema kwa ujumla, kuna uwezo mdogo wa usimamizi wa mazingira katika ngazi ya Serikali za Mitaa na kukuza uelewa wa jamii kuhusu sera na sheria husika bado ni changamoto. 

Anasema juhudi zaidi bado zinahitajika kwa Serikali za Mitaa na jamii husika katika usimamizi wa mazingira kupambana na usimamizi hafifu wa sheria za mazingira kwa jamii husika.

Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio, anasema anachokielewa yeye ni kuwa eneo hilo la Kilongawima ni makazi ya watu na si maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda.

“Hili la kuwapo kwa kiwanda katika eneo hilo ndiyo kwanza nalisikia kwako labda kwa sababu ya ugeni wangu katika ofisi hii, lakini nashukuru kwa kunipa taarifa hii; naahidi kulifuatilia na ni matumaini yangu ufubbuzi utapatikana,” anasema Urio.

Anasema kwa ujumla hakuna mtu asiyewataka wawekezaji, lakini kuna sheria na taratibu zilizowekwa kwao, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapambana na suala zima la uchafuzi wa mazingira.

Anasema sheria za uwekezaji ziko wazi kwa mwekezaji yeyote anayekuja nchini kuwekeza na kabla ya kuruhusiwa kuwekeza katika eneo lolote, ni lazima akubaliane na masharti yaliyowekwa na mamlaka husika ikiwamo utunzaji wa mazingira.

Afisa Raslimali Watu wa kiwanda hicho, Feisal Mohamed, alipoulizwa juu ya suala hilo anasema kwa kiwanda hakina matatizo na wananchi wanaolizunguka eneo husika linalolalamikiwa.

“Ndugu mwandishi, unajua kwa sasa biashara ni ushindani, yawezekana wanaovumisha haya mambo ni washindani wetu kibiashara lakini kiukweli hatuna matatizo na wananchi,” anasema Mohamed.

Kuhusu kubadili matumizi ya awali ya kiwanda anakiri kutokuwa na uhakika kama sheria na taratibu husika zilifuatwa na wakubwa ambao anasema wako nje ya nchi.

Mratibu wa Mazingira wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Jaffar Chimgege, anasema tatizo hilo halijafika ofisini kwake na kuahidi kulifanyia kazi suala tatizo hilo.

“Mtaa huo ulioutaja ninaufahamu ila sikumbuki kama eneo lile ni la viwanda, nakuahidi kulifuatilia tatizo hilo ili kubaini kama kuna tatizo na mwisho wa siku ukweli utafahamika,” anasema Chimgege.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Luhaga Mpina alipoulizwa juu ya matatizo yanayosababishwa na kiwanda hicho amekiri ofisi yake kutokuwa na taarifa zozote juu ya kiwanda hicho na kuahidi kulifanyia kazi.

“Nashukuru sana mwandishi kwa kunipa taarifa hizi mara moja nitahakikisha mimi mwenyewe nalifuatilia suala hili na kujua ukweli wake,” anasema Mpina.

Anasema pamoja na kuwa nchi inahitaji wawekezaji lakini maisha ya wakazi wa eneo husika ni muhimu kuliko kitu chochote kile.

Anasema sheria na taratibu zipo wazi kwa kila mwekezaji mwenye nia thabiti ya kuhitaji kuwekeza hapa nchini kwa hiyo hakuna haja ya kupigizana kelele na yeyote.

“Serikali haiwezi kumvumilia mwekezaji asiyezingatia sheria na taratibu zetu zinazotuongoza hapa nchini kwetu,” anasema Mpina.

By Jamhuri