Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, limeunda kikosi kazi kuchunguza tuhuma za baadhi ya Wachungaji na Wainjilisiti wa kanisa hilo, wanaotuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Kikosi hicho kimeundwa wiki iliyopita na Askofu wa Kanisa hilo, Dk. Frederick Shoo, ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la KKKT, kutokana na taarifa za kuwapo kwa baadhi ya watumishi hao wa kwenda kinyume na mafundisho ya Mungu.

Taarifa za uhakika ambazo JAMHURI imezipata na kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa Dayosisi hiyo, zinadai kuwapo kwa Mwinjilisti mmoja (jina linahifadhiwa) anayehudumu katika moja ya sharika za dayosisi hiyo, anayedaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Inadaiwa kuwa Mwinjilisti huyo amekuwa akiwatumia vijana wanaoendesha pikipiki kufanya nao mapenzi kisha huwalipa ujira wa kati ya Sh 15,000 hadi Sh. 20,000 kwa tendo moja na kwamba amewahi kukiri kujihusisha na ushoga.

Akizungumza na JAMHURI, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Ather Shoo, amesema kuwa kutokana na madai hayo kuwa mazito, ni vigumu kwa mkuu wao kuzungumzia tukio hilo kabla ya kuwa na taarifa sahihi.

Amesema kwamba anaomba kupewa muda wa wiki moja ili kikosi alichokiunda kuchunguza tuhuma kiweze kumaliza kazi yake na kuwa katika nafasi nzuri ya kutoa kauli kuhusiana na kashfa hiyo.

“Msimamo wa kanisa siyo wa dayosisi tu, ni KKKT kwa ujumla kwamba tabia hiyo haikubaliki na inakemewa, hivyo tunaomba mtupe wiki moja maana hatuwezi kujua kwa sasa kama vitendo hivyo vipo au havipo, ndiyo maana tumetuma watu wetu wakachunguze na baada ya hapo Baba Askofu atalitolea maelezo,” anasema Shoo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa miaka michache iliyopita, Mwinjilisti huyo aliwahi kukumbwa na kashfa hiyo baada ya kubanwa na mkuu wake wa kazi, ambaye ni Mchungaji Kiongozi katika usharika anaohudumu, aliweza kukiri kujihusisha na vitendo hivyo lakini aliomba msamaha na kuahidi kutorudia.

Baadhi ya Wachungaji (majina yanahifadhiwa) wamelidokeza JAMHURI, kuwapo na taarifa za baadhi ya wachungaji na wainjilisti kujihusisha na vitendo hivyo na kulitaka kanisa kutowaonea haya, kuwafichua ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.

“Ushoga upo na wanaofanya hivyo vitendo wanafahamika lakini huwezi ukalizungumzia kwa uwazi kwa sababu kufanya hivyo ni kulivua nguo kanisa na waumini wake ambao wamekuwa wakiwaamini viongozi wao,” anasema mchungaji.

Mchungaji avuliwa nguo na Polisi

Wakati hayo yakiendelea, utata umegubika tukio la mchungaji mmoja wa kanisa hilo ambaye mpaka sasa jina lake limefichwa, anayedaiwa kuvuliwa nguo na askari wanne wa Jeshi la Polisi kituo cha Bomang’ombe, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na kupigwa picha za utupu.

Mchungaji huyo anadaiwa kutendewa unyama huo katika moja ya nyumba za kulala wageni katika mji huo, katika tukio ambalo mpaka sasa bado linaacha maswali mengi ambayo jamii bado inahoji juu ya mazingira yaliyosababisha mchungaji huyo kuvuliwa nguo na kisha kupigwa picha za utupu.

Tukio hilo lilitokea Novemba mwaka jana ambako mchungaji huyo anadaiwa kuingia kwenye mtego ulioandaliwa na mwanaume mmoja aliyemhadaa mchungaji huyo kumuuzia pumba  na baada ya kufika katika mji huo mtu huyo alichukua chumba.

Taarifa zinapasha kuwa baada ya kuchukua chumba, alimwacha mchungaji huyo ndani ya chumba hicho kwa madai anakwenda kununua sigara na muda mfupi waliingia askari ambao walimshurutisha kuvua nguo na kuanza kumpiga picha za utupu.

Hata hivyo, mchungaji huyo alilazimika kutoa kiasi cha shilingi milioni 5.4 kwa askari hao kwa lengo la kuzima tukio hilo na kuachiliwa na baadaye kwenda kutoa taarifa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na baadaye kwa maofisa wa juu ya Jeshi la Polisi Mkoa.

Baada ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi juu ya tukio hilo, askari wanne wanaodaiwa kumtengenezea tukio la ushoga mchungaji huyo, walifutwa kazi mwishoni mwa mwaka jana huku tukio hilo likiacha maswali mengi kulingana na mazingira yake.

By Jamhuri