Milioni 950/- zilizotakiwa kulipwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama fidia ya Kiwanja namba 228, Kitalu K, Mivinjeni Kurasini jijini Dar es Salaam, zimezuiwa kwa takribani mwaka mmoja katika Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Temeke kutokana na mgogoro kati ya CCM na Shirika la Usimamizi wa Rasilimali za Reli (RAHCO) juu ya umiliki wa kiwanja hicho, uchunguzi wa JAMHURI umebaini

Fedha hizo ambazo hundi yake imetoka tangu mwaka jana mwezi wa pili ikiwa fidia ya kiwanja hayajafanyika. Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam aliandika barua ya zuio la kufanyika malipo hayo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ya tarehe 19/10/2015 yenye Kumb namba LD/163696/106 akieleza kuwa kiwanja hicho ni mali ya TRC (Rahco) na si CCM.

Kiwanja hicho ni miongoni mwa viwanja 92 vilivyotwaliwa na Serikali mwaka 2014 kupitia kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, kutoka kwa wamiliki wake wakiwamo CCM kwa barua Kumb namba MD/TMC/F.15/6/77 ya Desemba 12, 2014 kwa ajili ya shughuli za maendeleo chini ya Maeneo Maalum kwa ajili ya Uwekezaji wa Nje (EPZA).

 Hata hivyo, kiwanja hicho Rahco inadai kuwa ni chake na kipo kwa madhumuni ya kujengwa ‘Logistic Center’ kwa ajili ya reli ya Standard Gauge iliyopo kwenye mpango wa miradi ya Serikali ya awamu ya tano.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, amesema mgogoro huo unahitaji kuingiliwa kati na Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho, Rais John Magufuli, akidai Wizara inaonekana kupotosha umiliki wa kiwanja hicho na kwamba CCM haiwezi kukubali.

“Wizara wanasema kuwa kiwanja kile kinataka kutumiwa na Rahco kama Logistics Center katika ujenzi wa reli ya Standard Gauge. Mimi nilitamka nikawaambia sisi hatuna tatizo na hilo kwa sababu tulishakubali kuchukua fidia. Kinachogomba hapa ni kwamba Wizara wanataka tulipwe fidia ya majengo tu, sisi tunataka tulipwe fidia timilifu ya majengo na kiwanja,”anasema Madabida.

 Madabida anasema katika vikao muhimu vya usuluhishi, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi amekuwa mara nyingi akiwakilishwa na Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam, Nathaniel Mhonge, ambaye anamtupia lawama kuwa amekuwa akipotosha kuwa CCM imekubali kuwa eneo si lake katika barua zake (Kamishna) kwa Katibu Mkuu zinazotokana na majadiliano kati ya CCM, Wizara na Rahco. Barua hizo JAMHURI imeziona.

“Wizara wanasema kile kiwanja ni cha Rahco, hivyo sisi tunastahili kupokea fidia kutoka kwa Rahco. Hapana sisi ndiyo wamiliki. Nyaraka zote zinaonesha hivyo na hata Rahco walipojaribu kutaka kuleta ‘ujanjaujanja’ wa kukichukua kwa njia zisizofaa, tumepambana kikaendelea kuwa chetu,” anasema Madabida.

 Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Yamungu Kayandabila, alipoulizwa kuhusu mgogoro huu alikiri kuwa upo.

 “Mimi nina mwaka mmoja ofisini, hivyo mambo mengine siyajui vizuri. Nakupa Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam ili akueleze unayohitaji kuyafahamu maana yupo siku nyingi hapa na anauelewa vizuri mgogoro huo,” anasema Kayandabila.

Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhonge, anasema kiwanja hicho ni cha Rahco akitumia Barua ya Toleo ‘Letter of Offer ya tarehe 1/11/1995 yenye Kumb namba LD/168696/27/FMK ambayo CCM wanasema kuwa haina uhalali kisheria kutokana na Barua ya Toleo ya tarehe 14/08/2009 iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba Manispaa ya Temeke kwa Baraza la Wadhamini CCM yenye Kumb namba LD/TM/KR/228/14/TJM.

“Rahco ilikipata kiwanja hiki kutoka kwa Shirika la Ujenzi la ENIKON kwa Barua ya Toleo yenye Kumb LD/168691/1 ya tarehe 5/01/1994. Baada ya ofa hiyo kuonekana kuwa ilitolewa kimakosa ilibidi kimilikishwe kwa TRC ambayo sasa ni Rahco mwaka 1995. Hivi ndivyo vielelezo tunavyovitumia sisi kusema kuwa kiwanja si cha CCM bali ni cha Rahco,” anasema Mhonge.

 Hata hivyo, Madabida anasema kuwa CCM Tawi la Mivinjeni ilipata kiwanja kicho tangu mwaka 1986 na mwaka 1992, ilianza kukiendeleza kwa kujenga ofisi za tawi na mabanda ya biashara. Anasema CCM ilinunua kiwanja hicho kutoka kwa watu watatu kwa kuwalipa Sh 10,000 kila mmoja wao walikuwa wakifanya shughuli za kilimo katika kiwanja hicho.

Anawataja watu hao kuwa ni Lucas Mwembeli, Abdallah Mbaruku na Joseph Kitimbisi, ambapo mashahidi walikuwa J.J Guninita aliyekuwa Katibu wa Wilaya CCM Temeke na P.J Mosha aliyekuwa Katibu Msaidizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Nassib Mbaga, anakiri kuwa na hundi ya malipo ya milioni 950 ambayo yanatakiwa kulipwa kwa CCM japo hayajafanyika kutokana na zuio la Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam.

“Mimi nipo tayari kuwalipa CCM wakati wowote iwapo nitapata barua maalumu ya nani nimlipe kati ya Rahco ama CCM kutokana na zuio la mgogoro uliopo. Nashauri uende wizarani wakueleze zaidi maana wao ndiyo wameshikilia mgogoro huu na wamekwishakutanisha pande zote kwa ajili ya kupata suluhu,” anasema Mbaga.

Mkurugenzi wa Rahco, Masanja Kadogosa, alipoulizwa juu ya umiliki wa kiwanja hicho amesema ni mali ya Rahco. Hata hivyo, alivyoombwa nyaraka zinazoonesha umiliki wa Rahco kwa eneo hilo amesema kuwa zipo Wizara ya Ardhi.

“Nyaraka unaweza kuzipata Wizara ya Ardhi mimi hapa sina. Ninachoweza kukwambia ni kuwa kiwanja kile ni cha Rahco ila watu wamekuwa wabishi tu bila vigezo vya msingi. Kama unafuatilia hivi karibuni tumeingia mgogoro na wafanyabiashara wa Dodoma walioko eneo la reli wakidai ni lao,” anasema Kadogosa.

JAMHURI imefanikiwa kuiona barua ya Kadogosa kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi akiomba kupatiwa hati ya kiwanja hicho. Barua ya hiyo ni ya tarehe 11/11/2016.

1656 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!