Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezipongeza halmashauri tatu katika Wilaya ya Songea kwa kupata hati safi kwenye matokeo ya ukaguzi wa CAG unaoishia Juni 2022.

Halmashauri zilizopata hati safi katika wilaya ya Songea ni Madaba,Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Songea.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika Halmashauri hizo, kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani cha kujadili hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),Kanali Thomas amesema  hati safi ni matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mshikamano na ushirikiano kati ya watalaam na madiwani.

Hata hivyo kwa namna ya pekee ameipongeza Halmashauri ya Madaba kwa miaka sita mfululizo  kwa kupata hati safi na kuziagiza Halmashauri zote kuongeza bidi zaidi katika utendaji kazi kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kupata hati safi katika ukaguzi ujao wa CAG.

“Pamoja na kuwapongeza kwa kupata hati safi,mwenendo wetu wa kushughulikia hoja na mapendekezo ya CAG hauridhishi kabisa,kwa sababu bado  mapendekezo na hoja za nyuma za CAG hazifanyiwa kazi na kufungwa’’,alisema Kanali Thomas.

Ameuagiza uongozi katika Halmashauri hizo kuhakikisha hoja na mapendekezo yote yaliyotolewa na CAG yanafungwa na ukamilishaji wake ufanyike kabla ya Septemba 30 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa ameyaagiza mabaraza ya madiwani katika halmashauri hizo kusimamia miradi, kufuatilia kwa karibu utekelezaji  wa kuhakikisha hoja zote zinajibiwa na kuweka mikakati ya kuhakikisha hoja hizo hazijirudii tena.

Kanali Thomas ameagiza watumishi wote wanaozalisha hoja na kutumia fedha mbichi kuchukuliwa hatua za kinidhamu mapema .

Akizungumza kwenye mikutano hiyo Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile ameahidi kusimamia kikamilifu maagizo yote yaliyotolewa ikiwa ni Pamoja na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa ikiwemo ya uboreshaji elimu ya msingi BOOST inakamilika mapema.

Amesema katika kata ambazo zimepata miradi ya BOOST hadi sasa  utekelezaji wa ujenzi umefikia hatua ya kuezeka na kufanya umaliziaji.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komred Oddo Mwisho akizungumza kwenye mabaraza hayo ameziagiza Halmashauri hizo kupitia madiwani kusimamia kikamilifu ukusanyaji mapato na kuongeza vyanzo vya mapato ili kufikia malengo waliojiwekea.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea mheshimiwa Menas Komba ameahidi kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa kwa wakati  ambapo amesisitiza kuwa Halmashauri itasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ikiwemo kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani unaoingiza mapato makubwa kwa mkulima na halmashauri.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya CAG katika Halmashauri ya Manispaa ya  Songea
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Mheshimiwa Teofanes Mlelwa akizungumza kwenye  kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya CAG katika Halmashauri hiyo kilichofanyika mjini Madaba
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Songea wakiwa kwenye   kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya CAG katika Halmashauri hiyo kilichofanyika mji mdogo wa Peramiho Songea 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Mheshimiwa Menas Komba akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya CAG katika Halmashauri hiyo kilichofanyika mji mdogo wa Peramiho Songea

By Jamhuri