Na Mwandishi Wetu-Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi mkoani Arusha katika operesheni maalumu ya ukaguzi wa leseni za kuendesha vyombo vya moto na kuwafutia madaraja madereva 109 kwa kukosa sifa za madaraja hayo.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amebainisha kuwa zoezi hilo ni la hiari hadi Aprili 30, 2023 na linahusisha madereva wenye leseni zenye madaraja ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubeba abiria pamoja na mizigo.

ACP Masejo amefafanua kuwa katika ukaguzi huo madereva 522 walijitokeza kwa ajili ya kukaguliwa ambapo 109 walibainika kukosa sifa na kuelekezwa utaratibu wa kufuata ili kupata madaraja wanayoyahitaji.

Kamanda Masejo ametoa wito kwa madereva wote wenye leseni zisizokuwa na sifa hasa wanaondesha magari ya abiria na mizigo lakini pia kwa wale ambao tayari wamefutiwa madaraja yao kwenda kusoma udereva katika vyuo vya Serikali katika kipindi kilichobaki.

Aidha amebainisha kuwa baada ya kipindi hicho cha hiari kupita watafanya msako mkali kwa madereva wote waliokaidi ukaguzi huo.

Sambamba na hilo pia madereva wote pamoja na watumiaji wa vyombo vya moto wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na ajali.

Watuhumiwa saba wakamatwa wakiwa na meno ya tembo pamoja na Nyama pori

Katika tukio jingine jeshi la Polisi mkoani humo kupitia operesheni inayoendelea kwa nyakati tofauti limefanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa na meno mawili ya tembo.

ACP Masejo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Loshiri Lawai (35) mkazi wa Olkokola na James Samwel (45) mkazi wa Tengeru ambao walikamatwa huko katika Kijiji cha Shambasha wilayani Arumeru wakiwa na meno hayo ambayo walikuwa wameyapakia katika pikipiki Na. MC 509 BVG aina ya Kinglion.

Lakini pia jeshi hilo kwa kushirikiana na Askari wa usimamizi wa Wanyapori limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano wakiwa na nyama ya twiga na Pundamilia zikiwa na ngozi pamoja na vichwa viwili vya Pundamilia.

Kamanda Masejo amewataja waliokamatwa kuwa ni Richard Piniel (23), Japhet Philipo (30), Lameck Ezekiel (23) wakazi wa Ngusero, Peter Piniel (27) na Laila Issa (43) wakazi wa Morombo Jijini Arusha ambapo walikuwa na pikipiki zenye namba za usajili MC 141 CWL aina ya Sinoray, MC 983 CRG aina ya KingLion, MC 324 BXT aina ya Kinglion na bajaji aina ya Maxima namba MC 574 DBW.

Aidha uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekua wakijihusisha na biashara hiyo haramu, na wanaendelea kuhojiwa na pindi upelelezi utakapokamilika majalada yatapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi mkoa mkoani humo linawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuwataka watu wachache wanaojihusisha na matukio ya uhalifu.

By Jamhuri