Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BENKI ya NMB imeitambulisha akaunti mpya ya kidijitali kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya kijamii iitwayo ‘NMB Kikundi Account,’ iliyozinduliwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ambayo inajumuisha Bima ya Maisha kwa kila mwanachama na familia yake.

Uzinduzi wa NMB Kikundi Akaunti – ambayo ni rahisi, nafuu na salama kwa maendeleo ya vikundi na wanachama, unaakisi dhamira ya benki hiyo kuisapoti Serikali kutekeleza Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha, unaolenga kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki.

Akizungumza mbele ya Wakurugenzi wa Idara za Wizara yake, Dk. Gwajima aliipongeza NMB kwa ujio wa Kikundi Akaunti, aliyoitaja kama suluhisho na mbadala sahihi wa utoaji huduma kwa Vikundi vya kijamii vya kuweka akiba na kukopa, na kwamba ni zaidi ya ubunifu katika ustawi na maendeleo ya vikundi na wanachama wake.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa NMB Kikundi Akaunti ilihuduriwa na Badru Abdulnoor ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia wa wizara hiyo na Mkurugenzi wa Idara ya Makundi Maalum, Juma Samweli, na kuwakutanisha pamoja wanachama zaidi ya 500 kati ya milioni 1 wa iliyokuwa NMB Pamoja Akaunti.

“NMB Kikundi Akaunti ni zaidi ya ubunifu, hizi ni jitihada za wazi za NMB katika kusapoti juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, iliyojielekeza katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia taasisi za fedha.

“Lakini pia, kuzinduliwa kwa NMB Kikundi Akaunti – ambayo ni ya pamoja kwa wanachama wa vikundi, ni utekelezaji wa Malengo na Mkakati wa Serikali ya Rais Samia ya kuongeza Ujumuishwaji Wanawake na Makundi Mengine kwenye Huduma Jumuishi za Kifedha na kubwa zaidi usalama wa fedha zao.

“Imeelezwa hapa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, kuwa akaunti tunayoizindua leo sio tu suluhisho la changamoto mbalimbali za vikundi vya kijamii, bali pia imebeba huduma ya Bima ya Maisha kwa wanakikundi, hili ni jambo jema na la kibunifu linaloakisi dhamira njema ya benki kwa jamii,” alisema Dk. Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima (katikati), akizindua NMB Kikundi Akaunti iliyoboreshwa kidigitali. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na  kulia ni Afisa Mkuu wateja Binafsi na  Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi. (Na Mpiga Picha Wetu

Alikiri ya kwamba, Serikali inafurahishwa na juhudi za NMB zilizozaa akaunti hiyo, akiamini huduma hiyo inaenda kumaliza changamoto za Vyama vya Kuweka na Kukopa Vijijini (VSLA), Vyama vya Kijamii vya Akiba (SILC), Benki za Kijamii Vijijini (VICOBA), Vikundi vya Kijamii vya Akiba (CBSG) na Mashirika ya Kijamii (CBO).

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema NMB Kikundi Akaunti ni zao la maelekezo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuhamasisha taasisi za fedha kupunguza utoaji Huduma za Kifedha matawini, badala yake watumie mifumo mbadala ya kufanya miamala kwa njia ya kidijitali.

Alibainisha kuwa, katika kufanikisha hilo, ikafanya maboresho makubwa kupitia mrejesho wa wanachama wa vikundi 200,000 vyenye wanachama zaidi ya Milioni 1 wa iliyokuwa NMB Pamoja Akaunti iliyozinduliwa mwaka 2020, na kuzaa NMB Kikundi Akaunti, akaunti ya kidigitali yenye unafuu, urahisi na usalama katika matumizi.

“Ni kutokana na mabadiliko na maboresho hayo, kila mwanakikundi sasa anaweza Kuteleza Kidijitali na NMB Kikundi Akaunti, ikiwemo kufungua akaunti popote, kuchangia michango na kukopeshana, kuhamisha fedha kwa wanakikundi bila makato na kupata taarifa za kikundi kwa uwazi, na usalama wakati wote.

“Lakini pia, NMB Kikundi Akaunti itawawezesha wanakikundi kuchangia michango yao bila haja ya vikao wala kutembelea tawi la NMB, kuangalia salio na taarifa fupi ya kifedha ya kikundi, kubwa zaidi akaunti hii inajumuisha Bima ya Maisha, ikiwapa wanakikundi uhakika wa kifedha na amani ya akili kwa mwanachama na familia yake.”

“Mheshimiwa Waziri, sisi tunaamini NMB Kikundi Akaunti italeta matokeo chanya katika kurahisisha huduma za kibenki kwa vikundi na kuweka fedha za wanakikundi salama zaidi na tunatoa wito kwa wanachama wa vikundi rasmi na visivyo rasmi, kuichagua Benki ya NMB kama mshirika sahihi wa kifedha,” alisisitiza Zaipuna.

Please follow and like us:
Pin Share