Kwa mara ya kwanza upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo kwa watu wazima umefanyika kwa mgonjwa ambaye valvu yake ya moyo ya upande wa kushoto ilikuwa ikivujisha damu (severe mitral regurgitation).

Upasuaji huo umefanywa hivi karibuni na madaktari bingwa wa upasuajia wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao kutoka Serikali ya Watu wa China.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi  Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Williams Ramadhan alisema upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo umekuwa ukifanyika kwa watoto wenye shida za valvu lakini kwa watu wazima mgonjwa huyo amekuwa wa kwanza kurekebishiwa valvu yake kwani wagonjwa wengine wamekuwa wakiwekewa valvu za bandia.

“Upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo mara nyingi umekuwa ukifanyika upande wa watoto kwa mafanikio makubwa lakini haufanywi upande wa upasuaji wa moyo kwa watu wazima kwani matibabu hayo yanahitaji utaalamu wa hali ya juu lakini pia mafanikio huongezeka pale daktari husika anapokuwa amefanya idadi kubwa ya upasuaji huo”.

“Ukimfanyia mgonjwa upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo na usifanikiwe utahitaji kurudia kufanya upasuaji tena mara ya pili hivyo kumuongezea mgonjwa muda ya kukaa kwenye mashine na kumpa wasiwasi”, alisema Dkt. Ramadhani

Dkt. Ramadhani alisema mara nyingi kwasababu wataalamu wa JKCI wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watu wazima bado hawajatoa huduma hiyo kwa wagonjwa wengi wamekuwa wakifanya upasuaji wa kubadilisha valvu za moyo na si kurekebisha valvu za moyo.

“Tunaushukuru uongozi wa Taasisi kutuletea mtaalamu kutoka China anayefanya upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo kwa wagonjwa watu wazima ambao valvu zao zinaweza kurekebishwa na kupona ambaye kwa kipindi cha miaka miwili tutakachokuwa naye hapa atatuongezea ujuzi zaidi”, alisema Dkt. Ramadhan.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Serikali ya watu wa China Liu YiMin alisema upasuaji huo kwake umekuwa wa kwanza kuufanya tangu afike katika Taasisi hiyo na kuweza kubadilishana ujuzi na wataalamu wenzake wa JKCI.

Dkt. Liu alisema matibabu ya kurekebisha valvu za moyo humsaidia mgonjwa kuishi bila ya kutumia dawa za kuzui damu kuganda (Anticoagulants) katika maisha yake tofauti na mgonjwa ambaye valvu yake ya moyo imebadilishwa na kuwekewa ya bandia hulazimika kutumia dawa maisha yake yote ili kuzuia damu isigande

“Mgonjwa aliyebadilishiwa valvu za moyo uhitaji kutumia dawa ya warfarin hivyo kumlazimu kupima damu yake mara kwa mara kuangalia kama inaganda tofauti na mgonjwa huyu ambaye tumemrekebishia valvu yake hivyo haitaji kutumia warfarin”, alisema Dkt. Liu YiMin.

Dkt. Liu alisema wagonjwa waliobadilishiwa valvu za moyo wakati mwingine hupata tatizo la kuvuja damu hivyo kuwa katika hatari na kuhitaji kuonana na wataalamu wa afya mara kwa mara.

“Upasuaji huu wa kurekebisha valvu za moyo hasa kwa wanawake huwapa wagonjwa nafasi ya kutengeneza familia kwani mwanamke anapokuwa katika kipindi cha ujauzito hatakiwi kutumia dawa mbalimbali ikiwemo dawa ya warfarin”, alisema Dkt. Liu.

Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kurekebisha valvu ya kushoto ya moyo kutoka mkoani Mtwara Ismail Stambuli alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na shinikizo la damu kwa muda mrefu tatizo ambalo hakutegemea kama ingefikia kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.

Ismail alisema tatizo la moyo amekuwa nalo tangu utotoni na kuonyesha dalili moja ya kutokwa na jasho kwa wingi lakini kwasababu hakujua kama kutokwa na jasho kwa wingi ni dalili ya magonjwa ya moyo hakuwahi kufuatilia matibabu hadi sasa alipokuwa akisumbuliwa na typhoid mara kwa mara hivyo kulazimika kufanyiwa uchunguzi zaidi na kugundulika kuwa na tatizo la valvu ya kushoto ya moyo.

“Nawashukuru sana wataalamu wa JKCI kwa kugundua tatizo langu na kulitibu kwasababu sikuwa na dalili na ilikuwa hatari kwangu maana ningeendelea na maisha kama kawaida kumbe nina tatizo kubwa katika moyo wangu”, alisema Ismail.

By Jamhuri