Na Isri Mohamed
Watu wawili wameripotiwa kufariki dunia na wengine zaidi ya 80 kuokolewa wilayani Kilwa mkoani Lindi baada ya mvua kubwa iliyosababishwa na Kimbunga Hidaya kunyesha Mei 4, 2024 na kusababisha mafuriko.

Mbali na kusababisha vifo, pia yamesomba madaraja na kukata mawasiliano katika eneo la Somanga.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji, Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabije amesema marehemu hao wote wawili ni wakazi wa Kilwa mkoani Lindi, na mmoja ni mwanaume na mwingine mwanamke ila bado umri wao haujafahamika.

Wakati huohuo daraja moja limesombwa na maji na kusababisha mawasiliano kukatika kati ya mikoa ya kusini na Pwani.

Kimbunga Hidaya kimesababisha mvua kubwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara na Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani.

Hata hivyo mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jana imetangaza mwisho wa Kimbunga hicho kuanzia usiku wa saa tano na dakika hamsini na tisa Mei 4 2024, baada ya vipimo kuonesha kuwa kimbunga hicho kimepoteza kabisa nguvu yake baada ya kuingia Nchi kavu kupitia kisiwa cha Mafia.