Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la mitihani (NECTA) limetangaza kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita na Ualimu huku wakitoa rai kwa kamati za mitihani kuhakiksha usalama wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vituo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na baraza hilo.

Akizungumza wakati akitoa taarifa ya kuanza mtihani huo kwa waandishi wa habari leo Mei 5,2024 Jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji Said Mohamed amesema mtihani huo unatarajiwa kuanza Mei 6 na kukamilika Mei 24,2024.

“Mitihani ya kidato cha sita(ACSEE)na Ualimu ngazi ya cheti na Stashahada itaanza rasmi Mei 6 kwa Tanzania Bara na Zanzibar ambapo wa kidato cha sita utakamilika Mei 24 wakati wa ualimu utakamilika Mei 20 mtihani wa kidato cha sita utafanyika katika shule za sekondari 931 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 258 na vituo vya ualimu 99”,Amesema.

Amesema jumla ya watahiniwa 11,504 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2024 ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 104,449 na watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 9,055.

Akizungumzia kwa upande wa mtihani wa ualimu amesema jumla ya watahiniwa 11,552 wamesajiliwa ambapo kati yao watahiniwa 2766 ni ngazi ya Stashahada na watahiniwa 8,786 ni ngazi ya cheti ambapo kati yao wenye uhitaji maalumu wakiwa 12.

Akizungumzia maandalizi amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani husika,vitabu vya kujibia na nyaraka zote zinazohusu mtihani huo kwa Tanzania bara na Zanzibar.

Sambamba na hayo Dkt Mohamed amesema kuwa baraza halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakaebainika kujihusisha na kusababisha udanganyifu kwa mujibu wa sheria.

Aidha amewataka wasimamizi wa mitihani walioteuliwa kufanya kazi yao kwa weledi na uadilifu mkubwa na kuzingatia kanuni za mitihani,Taratibu na miongozo ya baraza waliyopewa ili mtahiniwa apate haki yake.

Please follow and like us:
Pin Share