Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji
MKUU wa wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle ametoa agizo kwa watu ambao bado wanaoishi kwenye maeneo yaliyozingirwa na maji ,mabondeni waondoke na kuhamia kwenye maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya usalama wao.
Akipokea misaada mbalimbali yenye thamani ya milioni 28 kutoka Taasisi ya WHO IS HUSSAIN, kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Rufiji, Gowelle alisema, Serikali inaendelea kutoa maeneo ya kutosha ili kuhakikisha wapo salama.
Alieleza ,kijiji cha Chumbi kimetoa eneo, kwasasa wanaendelea kulipima litakuwa na viwanja 500 kwa ajili ya makazi yaliyo salama.
Aidha Gowelle alieleza, wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) imetoa eneo Muhoro, na Serikali kutoa kwa wananchi ambapo vimetengwa viwanja 600 .
Alieleza, kazi kubwa inaendelea kufanyika kwani mvua bado zinaendelea kunyesha.
Vilevile alifafanua kwamba, katika kambi ya Chumbi kulikuwa na waathirika wa mafuriko 498 sasa wamebakia 311 ,kaya zilikuwa 117 kwasasa zimebakia 82.
“Watu wote 89,000 wengine wapo kwa ndugu, jamaa na marafiki,nao hao tunaendelea kuwawezesha kwasababu kwa hali ya kawaida kama mtu ukipokea kaya 3 zenye watu 11 alikuwa anakula debe mbili, hivyo kwasasa atahitaji debe 10 ,kwahiyo misaada hii tunayopokea tunashukuru Sana wadau hawa” alisema Gowelle.
Alisema, mafanikio hayo yametokana na mh Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha uwezo wake mkubwa katika kujenga mahusiano na Taasisi ndani na nje .
Gowelle alimpongeza Rais Samia kwa kutoa tani 300 za chakula, kupeleka vifaa tiba,madawa kupitia MSD kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohammed Mchengerwa kwa jitihada zake za kutafuta wadau,ambapo hadi sasa imefikia milioni 107.7 fedha ambayo wataenda kununulia mbegu ,mchakato umeanza ili baadae waathirika wanaojishughulisha na kilimo warejee kwenye kilimo na yeye amechangia milioni 50.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada kambi ya Chumbi, mratibu wa mradi wa Taasisi ya WHO IS HUSSAIN ,Mohsin Bharwani alisema , wametoa mchele kilo 2,000, magodoro 110, maharage 900,sukari 1,400 ,sembe 1,500,mafuta lita 1,200,pedi, miswaki na sabuni vote vina thamani ya Mil.28.
Alisema, WHO IS HUSSAIN inajishughulisha na kusaidia jamii katika mambo mbalimbali ikiwemo kujenga visima, shule.
“Wakati changamoto ya mafuriko inaanza tulimuona kwenye vyombo vya habari Mbunge wa jimbo Mchengerwa akitoa misaada na kuomba wadau kushirikiana na Serikali kuchangia waathirika “alisema Mohsin.
Mohsin alisema, wameguswa na kuanza kuchangishana na washirika wao wengine na kufanikiwa kupata misaada hiyo.