TABORA

Na Moshy Kiyungi

Miongoni mwa wanamuziki maarufu zaidi kuwahi kutokea nchini na kutikisa anga la muziki Afrika ni Mbaraka Mwinshehe Mwaluka.

Huenda kwa sasa ameanza kusahaulika lakini ukweli ni kwamba nyimbo zake kadhaa alizotunga au kuimba miaka ya 1970 bado zinavuma na kupendwa na mashabiki wa muziki nchini.

Mathalani, wimbo ‘Shida’ aliouimba miaka hiyo, umerudiwa na mwanadada Lady Jay Dee na kukubalika kwa mashabiki.

Januari 12, mwaka huu, mwamba huyu wa muziki ametimiza miaka 43 tangu alipofariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Makadara, Mombosa nchini Kenya, baada ya kupata ajali ya gari.

Mbaraka alikuwa nchini humo kwa shughuli zake za muziki akiwa pia amepanga kurekodi nyimbo kadhaa akiwa na bendi ya Super Volcano ya Morogoro.

Shuhuda wa ajali iliyotokea Januari 12, 1979 na kusababisha kifo cha mwanamuziki huyo, Zebedee Kinoka ‘Super Zex’, amewahi kusema kwamba Mbaraka alipata ajali akitokea Kisauni, jirani na Mombasa, alikokwenda kumtembelea mfanyabiashara wa Kitanzania aliyekuwa akimiliki hoteli.

“Nilipofika karibu na Kanisa la Kongoya niliona Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar kwa kasi kubwa, ikagongana na lori.

“Mimi pamoja na watu wengine tukakimbilia kwenda kushuhudia ajali ile. Mara moja nikamtambua Mbaraka. Nikawaambia wengine kuwa huyo ni Mbaraka Mwinshehe, mwanamuziki kutoka Tanzania,” anasema Super Zex.

Anasema yeye na watu hao wakaanza kukata mabati ya gari kumuondoa Mbaraka aliyekuwa hai lakini amebanwa miguu.

Baada ya kumtoa, wasamaria wema wakampeleka Hospitali ya Makadara, mjini Mombasa na Super Zex anasema:

“Nikawafuata wanamuziki wenzangu wa Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wameanza kupiga nyimbo za utangulizi pale Zambia Bar wakimsubiri Mbaraka.

“Sote tukaenda hospitali. Wataalamu wakatuambia tuchangie damu ya kumuongezea kiongozi wetu, Mbaraka.”

Ombi la kutoa damu kuokoa maisha ya Mbaraka halikupokewa kwa mikono miwili na wenzake, badala yake wakaanza kukwepa wakitoa visingizio mbalimbali.

Muda mfupi baadaye Mbaraka akaaga dunia akiwa na umri wa miaka 34 tu.

Mwili wake ukasafirishwa hadi mpakani mwa Tanzania na Kenya ulikopokewa na ndugu, jamaa, marafiki na maofisa wa Wizara ya Utamaduni.

Mwanamuziki huyu maarufu akazikwa siku chache baadaye kijijini kwao Mzenga, Kisarawe mkoani Pwani.

Kwa miaka kadhaa sasa, wadau wa muziki husherehekea Sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kumbukizi ya nguli huyu aliyeliletea sifa kubwa taifa kupitia muziki, akicharaza gitaa la solo, akitunga na kuimba nyimbo zenye ujumbe mahususi kwa jamii.

Mbaraka alizaliwa Juni 27, 1944 mjini Morogoro akiwa mtoto wa pili miongoni mwa watoto 12 wa familia yao.

Wadogo zake, Zanda na Matata, nao walikuwa wanamuziki; Zanda alikuwa mwimbaji wa nyimbo za Kizungu wakati Matata alikuwa akichanganya ‘drums’ katika bendi ya Morogoro Jazz.

Baba yao, mzee Mwinshehe Mwaluka, Mluguru wa Morogoro, alikuwa karani katika mashamba ya mkonge. Mama yake alikuwa Mngoni.

Historia inaonyesha kuwa babu yake Mbaraka alikuwa Mdoe kutoka Bagamoyo, aliyepelekwa na wakoloni katika Kijiji cha Mzenga, Kisarawe ambako alifanywa chifu.

Babu huyo alioa wake tisa na kupata watoto zaidi ya 50, akiwamo baba yake Mbaraka; mzee Mwaluka.

Enzi za uhai wake, Mbaraka aliongoza kwa ufanisi mkubwa bendi za Morogoro Jazz na baadaye Super Volcano.

Umahiri wake wa kucharaza gitaa la solo ulimfanya kupewa jina la utani la ‘International Soloist’.

Tungo za Mbaraka zimejaa maudhui mema na zilimpandisha chati hadi kuwa mmoja wa wasanii walioiwakilisha Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (Expo70) yaliyofanyika Osaka nchini Japan mwaka 1970.

Wasanii wengine wa Tanzania walioshiriki kwenye maonyesho hayo ni Morris Nyunyusa, mlemavu wa macho aliyekuwa na kipaji cha kupiga ngoma zaidi ya kumi kwa wakati mmoja.

Kikundi cha sanaa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Brass Band ya Polisi chini ya Afande Mayagilo pia walitoa burudani huko Japan.

Aliporejea nchini, Mbaraka akatunga wimbo wa ‘Maonyesho Japan’, akisimulia mafanikio waliyoyapata wasanii wa Tanzania, akiyataja makundi yaliyokwenda huko na mambo ya kuvutia yaliyowaacha hoi wenyeji, Japan na watu wa mataifa mengine walioshiriki.

Mbaraka alipata elimu katika Shule ya Kati ya Kisarawe mwaka 1963, baadaye akaenda Morogoro kuendelea na masomo, akaacha shule akiwa darasa la 10 na kujikita kwenye muziki.

Wanaomfahamu wanasema siku moja, mwaka 1965, wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao, Mbaraka alipita akiwa na begi lake.

Walipomuuliza anakwenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa darasani, akawajibu kuwa hataki tena shule ameamua kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha.

Inasemekana kuwa wanamuziki wale wakamsihi alale klabuni kwao apate muda wa kutafakari uamuzi wake wa kuacha shule, akakubali.

“Asubuhi iliyofuata wakapigwa na butwaa walipomuona akifanya mazoezi ya kupiga gitaa, kabla ya hapo walikuwa wakimfahamu kuwa ni mpulizaji wa filimbi,” simulizi hizo zinasema.

Kwa kuwa Morogoro Jazz hawakuwa na mpiga ‘rhythm’, wakamuomba Mbaraka aachane na safari ya Dar es Salaam ili abaki kwenye bendi hiyo. Hilo nalo akalikubali, na kujikuta akiwa ‘kibarua’ wa bendi hiyo.

Bendi hiyo ikaalikwa Dar es Salaam kupambana na Kilwa Jazz, Mbaraka akaona hiyo ndiyo nafasi yake, akagoma kuondoka kwa kuwa hakuwa akilipwa chochote.

Ikabidi busara za viongozi zitumike. Wakakubaliana kumlipa Sh 120 kwa mwezi. Kuona hivyo, mpiga solo aliyekuwa akilipwa Sh 150, naye akagoma kwenda Dar es Salaam kwa hoja kwamba mpiga rhythm hastahili kupata mshahara.

Mbaraka akawatoa hofu viongozi wake akiwaambia yeye atapiga gitaa la solo.

Safari ya Dar es Salaam ikaiva kwenda kukabiliana na Kilwa Jazz iliyokuwa na wanamzuki wakubwa kama akina Ahmed Kipande, Kassim Mapili, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ na Duncan Njilima.

Siku ya mpambano ikawadia, Mbaraka akakabidhiwa gitaa la solo, akapanda jukwaani na kuzicharaza nyuzi kwa umahiri wa kutisha katika nyimbo zote.

Morogoro Jazz ikaibuka mshindi na mara mshahara wa Mbaraka ukapandishwa hadi Sh 250 kwa mwezi! Kiwango cha juu kuwahi kutokea miaka hiyo.

Kipaji cha kuimba huku akipiga gitaa kilimtofautisha Mbaraka na wanamuziki wengi sana.

Baadhi ya myimbo alizotunga au kushiriki ni ‘Shida’, ‘Nateseka’, ‘Safari Siyo Kifo’, ‘Dina Uliapa’, ‘Maudhi’, ‘Penzi la Mashaka’, ‘Heshima kwa Vijana’, ‘Harusi Imevunjika’, ‘Mshenga No.1’ na ‘Nisalimie Zaire’. 

Miongoni mwa wanamuziki aliokuwa nao Morogoro Jazz ni Mzee Seif Ali, Tosi Malekela, Suli Bonzo, Kilongola, Lazaro Bonzo na Mpalanje. 

Wengine ni Kazingoma, Simaro Kasansa, Kasinde, Matata, Zanda Ngokoko, Athumani na Paschal.

Mwaka 1973 Mbaraka alijiengua Morogoro Jazz iliyokuwa ikipiga muziki kwa mitindo na kuunda bendi yake ya Super Volcano aliyoiongoza hadi mauti yalipomfika.

Binti yake, Taji Mbaraka, ndiye alifuata nyayo zake, akiimba na kuungurumisha gitaa la besi katika bendi ya Super Volcano.

Lakini inasemekana kwa sasa Taji ameachana na muziki na kuwa mfanyabiashara.

Mungu aipumzishe roho ya Mbaraka Mwinshehe pahala pema peponi. Amina.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0767331200 na 0784331200.

By Jamhuri