Arusha

Na Mwandishi Wetu

Halmashauri ya Jiji la Arusha imedhamiria kuinua sekta ya elimu kwa kuboresha mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia ili kuondoa daraja sifuri kwa wanafunzi wa kidato cha pili na nne kwa kutenga kiasi cha fedha kutoka mapato ya ndani.

Fedha zilizotengwa ni Sh bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari za Unga Ltd na Kalimaji pamoja na ujenzi wa madarasa mapya ya ghorofa katika shule za sekondari za Moivaro, Arusha Terrat, Unga Ltd na Shule ya Sekondari Elerai ambapo ujenzi wake umeshakamilika na kuanza kutumika.

Aidha, mkakati mwingine ni kutenga Sh milioni 98 kwa ajili ya kutoa motisha kwa walimu wa sekondari katika jiji hilo watakaofanya vizuri katika somo na kuwezesha wanafunzi kupata daraja ‘A’ katika matokeo ya kidato cha pili na nne ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayepata daraja sifuri.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. John Pima, amesema hatua hiyo ni katika kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya elimu nchini ambapo aliipatia halmashauri hiyo kiasi cha Sh bilioni 2.1 ambazo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 105, kutengeneza madawati 5,250 na ujenzi wa matundu 44 ya vyoo ambapo vyote vimeshakamilika na kukabidhiwa tangu mwezi Desemba mwaka jana.

“Baada ya kukaa na wenzangu, Baraza la Madiwani tukaona ni vema tukamuunga mkono Rais kwa vitendo badala ya kusema tu kwa maneno kuwa tunamshukuru. Ndiyo maana tukakaa na kupitisha Sh bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari na kuongeza vyumba vya madarasa kwenye baadhi ya shule pamoja na kutenga Sh milioni 98 kwa ajili ya kutoa motisha kwa walimu,” anasema Dk. Pima na kongeza:

“Yote hii ni katika kuhakikisha kuwa jiji letu linapanda kitaaluma, kama mwanafunzi atasoma katika mazingira mazuri yenye majengo mazuri, samani zipo, lakini pia walimu wataishi nyumba zilizo karibu na vituo vyao vya kazi, kama haitoshi pia tutawapa walimu motisha kwa watakaotoa daraja ‘A’ katika matokeo ya kidato cha pili na nne, ni kwa nini tupate daraja sifuri katika jiji letu?”

Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwenye sekta ya elimu jijini hapo umesababisha idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa shule za serikali kupanda kutoka 11,077 mwaka jana hadi kufikia wanafunzi 11,427 mwaka huu.

Aidha, uandikishaji wa wanafunzi wa awali kwa kipindi cha mwaka jana ulikuwa ni watoto 6,957 na kwa upande wa uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la saba kwa kipindi hicho ukiwa ni 12,037 ambapo kwa mwaka huu zoezi la uandikishaji wa wanafunzi hao bado linaendelea.

Amesema katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanasoma, wao kama jiji kwa kushirikiana na Baraza na Madiwani pamoja na wadau wake wa maendeleo wametoa msaada kwa wanafunzi zaidi ya mia nne walioshindwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na uduni wa maisha katika familia zao kuwapatia mahitaji ya shule ambayo ni sare za shule, mabegi kwa ajili ya kubebea madaftari, pea za viatu, taulo za kike pamoja na soksi.

Wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kubuni wazo zuri ambalo limegusa zaidi utu kwa kuangalia watoto wenye sifa na moyo wa kusoma lakini familia zao hazina uwezo wa kuwahudumia mahitaji ya shule kwa kuzingatia pia serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili yao katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na elimu bila malipo.

“Hii sasa ndiyo maana halisi ya kumuunga mkono Rais wetu Samia, niwapongeze sana jiji kwa kuanzisha hii programu na niwasihi iwe endelevu kila mwaka, na mimi nawaahidi kushirikiana nanyi bega kwa bega,” anasema Mtanda.

Katika uchangiaji huo Mkurugenzi wa Jiji, Dk. Pima pekee ametoa sare za shule kwa wanafunzi wote 413, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameahidi kuchangia madaftari 500 pamoja na taulo za kike 50 kwa muda wa miezi sita ambapo msaada mwingine umetokana na michango ya watumishi, watendaji, madiwani pamoja na wadau wa maendeleo wa jiji hilo.

Katika hatua nyingine, jiji hilo limepokea zaidi ya vitabu laki moja vya kiada na ziada kwa shule zote za  msingi za serikali zenye mchepuo wa Kiingereza na Kiswahili kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Dk. Pima amesema wamepokea jumla ya vitabu 107,644 ambapo wamevigawa kwa shule zote za msingi zilizopo katika jiji hilo, kwa maana ya shule zenye mchepuo wa Kiingereza pamoja na zenye mchepuo wa Kiswahili vya masomo mbalimbali.

Ameongeza kuwa pia vipo vitabu vya miongozo ya walimu, vitabu vya elimu maalumu pamoja na vitabu ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) na kwamba tayari ameshatoa maelekezo kwa walimu wakuu wa shule hizo namna ya kuvitunza ili vitumike kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Jiji la Arusha, Mwl. Reginald Richard, amesema kufuatia hatua hiyo ni wazi kuwa kiwango cha taaluma kitapanda na kusababisha jiji hilo kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya darasa la nne na saba ngazi ya taifa, kutoka nafasi ya pili waliyoshika katika matokeo hayo mwaka jana.

“Hili ni deni kwetu, kwani Mhe. Rais ametuwekea mazingira mazuri ya kuhakikisha sekta ya elimu inakua, niseme tu kuwa hata hii nafasi ya pili tuliyoshika ya matokeo ya darasa la saba mwaka jana si sawa, sisi tulipaswa kushika nafasi ya kwanza kitaifa, kwani hatuoni sababu ya kushindwa kutokana na kuwapo kwa miundombinu bora ya elimu,” amesema Mwl. Richard.

Amesema moja ya mikakati ya kuhakikisha kuwa jiji hilo pia linaongoza kitaifa ni pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji zitakazosaidia stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (K KK) pamoja na kudhibiti tatizo la utoro kwa wanafunzi, ambapo tayari wameshaweka mkakati na wazazi ili wanafunzi waweze kupata chakula cha mchana.

Aidha, amesema ameshatoa maelekezo kwa walimu hao kuweka utaratibu wa kuwaazimisha wanafunzi vitabu hivyo ili waweze kujisomea majumbani siku za mwishoni mwa wiki badala ya kuwaacha kutumia muda huo kucheza.

Mstahiki Meya wa jiji hilo, Maximilian Iraghe, amesema licha ya vitabu hivyo kuwasaidia wananfunzi katika masomo yao lakini pia vitatoa motisha kwa walimu katika ufundishaji, kwani hapo awali walimu hao walikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitabu vya miongozo na vya kufundishia.

Huu ni mwendelezo, kwani tayari tulishapokea Sh bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, madawati pamoja na matundu ya vyoo ambavyo vyote kwa pamoja vimeshakamilika na vimeanza kutumika mwaka huu, na sasa tumepokea vitabu ambavyo tumevigawanya kwenye shule zote za serikali za mchepuo wa Kiingereza na Kiswahili, bila kuwasahau wenye majitaji maalumu, MEMKWA na miongozo ya walimu, kwanini tusishike nafasi ya kwanza kitaifa,” amehoji Mstahiki Meya.

Baadhi ya walimu waliozungumza wakati wa upokeaji wa vitabu hivyo, Mwl. Zebedayo Mollel, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Themi pamoja na Mwl. Zukra Karunde,  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Daraja Mbili wamesema serikali itegemee mabadiliko makubwa kwenye suala la kitaaluma.

Wamesema awali kitabu kimoja kilikuwa kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya watano lakini kwa idadi ya vitabu walivyopokea kwa sasa kitabu kimoja kitatumiwa na mwanafunzi mmoja au wawili tu.

By Jamhuri