*Msekwa asema kuna waliojitokeza kutangaza majina yao

*Chenge, Dk. Tulia, Dk. Kashililah

 watajwa kumrithi Ndugai

DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Nani kurithi nafasi ya Spika wa Bunge baada ya Job Ndugai kujiuzulu Januari 6, mwaka huu, ni swali gumu kujibika ndani ya CCM.

Hadi kufikia Jumamosi ya wiki iliyopita, idadi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo walikuwa 70 katika vituo vya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar huku mmoja akishindwa kurudisha.

Kwanini idadi ya walioonyesha nia ya kurithi nafasi ya Ndugai imefikia 71 licha ya gharama ya fomu ya kugombea nafasi hiyo kuwa Sh 1,000,000, hili nalo ni swali gumu.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki, Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa, amesema idadi kubwa ya wana CCM waliojitokeza kwanza inaonyesha ni jinsi gani demokrasia ndani ya chama hicho ilivyo ya hali ya juu, lakini; “Mwisho atapatikana mtu mmoja tu atakayekwenda kupigiwa kura.”

Pia amesema kuna makundi mawili ya watu waliojitokeza kugombea nafasi hiyo; wanaotangaza majina yao na wenye nia ya kweli ya kutaka kushika nafasi hiyo.

“Kwa kweli kuna mmoja nimewahi kumuuliza anasema yeye anatengeneza CV yake ili ajulikane kwamba na yeye yumo, nadhani miongoni mwao hadi kuna wanafunzi, hao wanatafuta jina tu!

“Nadhani kuna kundi hilo la watafuta jina na kujulikana na kundi jingine lina nia kweli ya kugombea hiyo nafasi kwa lengo la kufanikiwa,” amesema.

Pia amesema idadi ya wagombea hao inaonyesha kuwa watu wanakubali kwamba demokrasia ndani ya CCM ni ya kweli, na chama hicho kimetoa nafasi watu wengi wagombee.

“Kwamba chama hakisemi uongo. Chama kimetoa siku tano. Siku tano wasingezitoa kama chama kisingekuwa na nia njema kingetoa siku moja tu, kisha kingesema tumefunga na wengine kwaheri, lakini kimetoa siku tano ili kutoa nafasi kwa watu wengi.

“Wamefanya hivyo wote wanaotaka waweze kujitokeza, inaonyesha nia njema ya chama kwamba kina nia ya kweli ya kutekeleza demokrasia ndani ya chama. Lakini mimi najua kwa sababu nimekulia uko kwamba chama hiki kina utaratibu mzuri wa kuchuja watu hatimaye watabaki watatu watapelekwa katika kikao cha uchaguzi na kura za kikao hicho zitatoa mmoja atakayekwenda kupigiwa kura na Bunge,” anasema.

Msekwa anasema yeye aligombea uspika katika mazingira kama hayo mwaka 1994 baada ya Spika Chifu Adam Sapi kujiuzulu kwa maradhi.

Anasema kutokana na maradhi Sapi alijiuzulu yeye akiwa ni Naibu Spika na wakati huo akagombea baada ya utaratibu wa ndani ya CCM kufanyika. Bungeni wagombea walikuwa wawili na yeye alishinda na mwaka uliofuata lilikuwa Bunge la vyama vingi, pia akagombea dhidi ya Chifu Abdallah Fundikira, naye akamshinda mwaka 1995.

Kuhusu sifa za atakayegombea nafasi hiyo, Msekwa, anasema zipo katika Katiba ya nchi zinazomtaka mtu mwenye sifa za kuwa mbunge, kwa mtu ambaye ni mbunge tayari au ana sifa za kuwa mbunge.

“Tusianze kubashiri bashiri, anayeweza kufanya hivyo ni Mungu peke yake ndiye anaweza kujua itakuwaje, tuwaache wabunge wetu watumie mamlaka yao ya kikatiba kumchagua spika. Kuhusu mihimili, mipaka ya kazi za mihimili iko katika Katiba na Katiba ndiyo inatuongoza wote,” anasema Msekwa baada ya kuulizwa iwapo Bunge na Utawala (Serikali) kuna mhimili mmoja wenye mzizi mrefu zaidi au la.

Ibara ya 63(2) inasema: “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”

Mwenyekiti wa Chama cha ADA-Tadea, John Shibuda, ametaja sifa za mtu anayepaswa kuwa Spika wa Bunge kuwa ukiondoa elimu na jinsia, lakini ni lazima awe anazijua kanuni za Bunge, uangalie haiba yake, uwezo wa kuongoza, kuunganisha wabunge na anayejua kutofautisha kazi za mihimili mingine.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki, Shibuda amesema Andrew Chenge, Stephen Masele, Dk. Thomas Kashililah, Sophia Simba na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson mmoja ana nafasi ya kuwa Spika.

Hata hivyo, amesema kauli ya Tulia aliyoitoa Ikulu wiki iliyopita wakati Rais Samia Suluhu Hassan anawaapisha mawaziri kwamba Bunge litaikosoa Serikali kwa nidhamu imemharibia.

“Kauli alizozitoa Tulia pale Ikulu ni za kudhalilisha mhimili wa Bunge. Utakuwaje Spika una macho kipofu na akili kipofu huku unakwenda kuongoza watu wenye macho ya kuona, kila mmoja amejinasibu anaweza,” amesema Shibuda na kuongeza:

“Mimi nadhani kujitokeza watu wengi wanampinga Tulia kwamba hawana imani naye, siri ya kujitokeza watu wengi ni pale alipochukua fomu watu wakawa na machukizo kutokana na kauli yake aliyoitoa Ikulu kwamba atakuwa na adabu kwa Rais.

“Hata Nyerere alishaonya adabu ikizidi unakuwa mtumwa, utiifu usiokuwa na mwiko ni utumwa, kwa hiyo zile ni kelele za kupinga asipatikane mtu wa hovyo, tunapaswa kusoma alama za nyakati kwa masilahi na hawana imani naye. Lini Rais Samia amewahi kulalamika kwamba Bunge halina nidhamu? Hajawahi kulalamika.”

Pia anasema hatarajii Chama chake cha ADA-TADEA, kuweka jina la mtu atakayegombea nafasi ya Spika.

“Sitarajii chama changu kuchukua fomu ya kugombea uspika. Tangu lini mbuzi akaingia katika zizi la simba halafu akatoka salama? Demokrasia tunaidhalilisha hapa Tanzania, hatutaki kujenga maana halisi ya demokrasia,” amesema Shibuda.

Mhadhiri Mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveri Lwaitama, amesema Katiba inaleta mkanganyiko wa kumpata mgombea binafsi mwenye sifa za kushika nafasi ya Spika.

Dk. Lwaitama ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa mkanganyiko huo unatokea pindi kila mgombea anapolazimika atokane na chama cha siasa.

“Suala hapa ni la facts. Kwanza, Katiba inaleta mkanganyiko kwamba ili mtu awe Spika lazima awe mwanachama wa chama fulani, majina yatapelekwa kwa anuani ya chama, yaani chama kitapeleka majina,” anasema.

Pia anasema kama isingekuwa hivyo ingeruhusu hata majaji au jaji mashuhuri mwenye sifa na weledi kwenda kuchukua fomu za kugombea uspika, lakini Katiba hairuhusu mtu binafsi.

Kuhusu vyama vingine vya siasa kupeleka jina la mgombea uspika anasema ni vigumu kufanya hivyo katika Bunge linalodhibitiwa na CCM, kwa kuwa lina wabunge wengi zaidi ya asilimia 90.

Pia anasema katika wanachama wote waliojitokeza hakuna anayemzidi Chenge, kwa sababu yeye licha ya kuwa mbunge wa siku nyingi, lakini amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Anasema licha ya Chenge kuwa na baadhi ya tuhuma zisizowahi kuthibitishwa mahakamani, atakayekuwa anazitoa atakuwa anamuonea.

“Kwa kweli Chenge ana vigezo vyote na hakuna anayemzidi, labda vitumike vigezo vingine vya pembeni visivyojulikana kwa mtu yeyote yule,” anasema Lwaitama.

Pia anasema Masele naye ana sifa za kuwa Spika kwa sababu anaweza kujenga hoja na amewahi kuwa katika Bunge la Afrika, hivyo ana uzoefu.

Kuhusu Dk. Tulia anasema ana sifa za kuwa Spika ingawaje hajawahi kutengeneza maisha yake ya siasa, bali ametengenezewa.

“Tulia ana uzoefu bungeni, lakini maisha yake ya siasa ametengenezwa badala ya kutengeneza mwenyewe. Amekuwa Naibu Spika kwa miaka mitano baada ya kuteuliwa kuwa mbunge.

“Zungu naye ana nafasi kwa sababu amekuwa bungeni kwa muda mrefu. Yaani nikitumia sifa za kawaida tu, na amekuwa mwenyekiti wa kamati mbalimbali kama mshauri,” anasema Lwaitama.

Makada wa CCM waliochukua fomu

Mbali na Chenge, Dk. Tulia, Masele, Sophia Simba na Dk. Kashililah, wengine miongoni mwa waliochukua na kurudisha fomu hizo ni Godluck Medee, Juma Chuma, Baraka Byabato, Festo John, George Nangale, Barua Mwakilanga, Zahoro Hanuna, Thomas Kirumbuyo, Angelina John, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, Patrick Nkandi, Hamidu Chamani, Emmanuel Sendama, Goodluck Mlinga, Bibie Msumi, Hilal Seif na Athumani Mfutakamba.

Wengine ni Mwenda Mwenda, Herry Kessy, Josephat Malima, Adamu Mnyavanu, Stella Manyanya na Andrew Kevela.

Wengine ni Dk. Simon Ngatunga, Tumsifu Mwasamale, Merkion Ndofi, Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi, Abwene Kajula, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu na Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka.

Wapo pia Profesa Handley Mpoki, Dk. Mussa Ngonyani, Hamisi Saidi, Asia Abdallah, Waziri wa zamani wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani, Abdulaziz Jaad Hussein, Samweli Magero, Rahim Rashid Ismail, Alex Mwita, Semistocles Rwegasira, Gragrey Nyalohal, Hatibu Mgeja, Dk. Linda ole Saitabau na Profesa Norman Sigalla.

Kwa mujibu wa Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni wa CCM Taifa, Solomon Itunda, miongoni mwa wanachama hao, wanaume wako 60 na wanawake wako 11. Mchakato ulianza Januari 10 hadi 15, mwaka huu kisha hatua nyingine za kumpata mwanachama mmoja wa kukiwakilisha chama hicho zitafuata.

Kuhusu ratiba ya chama hicho ya kumpata mgombea wa nafasi hiyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema mchakato huo utahitimishwa Januari 31, mwaka huu baada ya Januari 17, mwaka huu Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kukutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu (CC) ya halmashauri hiyo kuhusu wagombea hao.

Pia Januari 18 hadi 19, mwaka huu kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho na Kamati Kuu ya CCM itafanya kazi hiyo.

Kisha kabla ya Januari 30, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM itakaa na kuteua jina la mgombea uspika kwa tiketi ya CCM kwa mujibu wa Ibara ya 108(6)(n) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977, inayosema pamoja na majukumu mengine ya Kamati Kuu itakuwa na kazi ya;

“Kufikiria na kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama wa CCM wanaoomba kugombea nafasi ya Spika wa Bunge/Baraza la Wawakilishi, Meya wa Halmashauri ya Jiji/Manispaa.”

Vyama vya upinzani vingi vimeonyesha kutokuwa tayari kuweka wagombea kwa kitu abacho kiko wazi kwamba CCM ina wabunge zaidi ya asilimia 90, hivyo kumchangua Spika anayetokana na upinzani, uwezekano ni sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano.

842 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons